
Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema itazuia uingizaji wa mazao na bidhaa za kilimo kutoka nchi za Malawi na Afrika Kusini kuanzia Jumatano Aprili 23, 2025 endapo vikwazo kwa Tanzania miongoni mwa nchi hizo vitaendelea.
Taarifa hiyo imetolewa na Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe leo Alhamisi Aprili 17, 2025 kupitia mitandao yake ya kijamii huku akisema amefanya jitihada mbalimbali na nchi husika ili kuondoa vikwazo hivyo bila mafanikio.
“Serikali imepokea taarifa rasmi kuwa Serikali ya Malawi imezuia kuingia kwa mazao ya kilimo kutoka Tanzania, yakiwemo unga, mchele, tangawizi, ndizi na mahindi. Hatua hii imeathiri moja kwa moja shughuli za wafanyabiashara wetu wanaosafirisha bidhaa hizo kwenda Malawi.
“Ni vyema ifahamike kuwa kwa kipindi cha miaka mitano, Serikali ya Tanzania imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali kufungua soko la ndizi Afrika Kusini bila mafanikio. Hali hii inafanana na changamoto tulizopitia kwa zaidi ya miaka 10 katika kufungua soko la parachichi, hadi pale tulipoamua kuchukua hatua za kulinda masilahi ya nchi yetu,”ameandika Bashe.
Bashe ameendelea kuwandika kuwa: “Kutokana na hali hii, na baada ya juhudi zote za kidiplomasia kufanyika bila mafanikio, ninapenda kuwataarifu yafuatayo: Kwanza, iwapo Serikali ya Malawi na Afrika Kusini hazitabadilisha msimamo wao kufikia Jumatano ijayo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Kilimo itazuia uingizwaji wa mazao na bidhaa zote za kilimo kutoka nchi hizo mbili.
“Pili, Mizigo ya bidhaa za kilimo kutoka Malawi na Afrika Kusini haitaruhusiwa kupita ndani ya mipaka ya Tanzania, kuelekea bandari ya Dar es Salaam au nchi nyingine yoyote, hadi zuio hilo litakapoondolewa.”
“Tatu, usafirishaji wa mbolea kwenda Malawi utasitishwa, ikiwa ni sehemu ya hatua za kulinda masilahi ya wakulima na wafanyabiashara wa Kitanzania.”ameandika.
Bashe ameendelea kuandika: “Wasafirishaji wote wa Kitanzania wanaosafirisha bidhaa za kilimo, ninawashauri kuacha kupakia bidhaa hizo mpaka hapo Malawi na Afrika Kusini watakapobadilisha msmamo wao. Wafanyabiashara walioweka order za apples, machungwa, na bidhaa nyingine ambazo hununuliwa Afrika kusini, ninawashauri kuacha kwa sasa kwani hatutoziruhusu kuingia Tanzania mpaka hapo Afrika Kusini itakapotufungulia soko la ndizi.
“Ninathibitisha kuwa kama waziri mwenye dhamana, nimewasiliana kwa njia mbalimbali na Waziri wa Kilimo wa Malawi bila mafanikio ya kupata majibu rasmi.”
Amemalizia kwa kuandika kuwa, “Hatua hizi ni za kulinda heshima ya nchi yetu, uchumi wa wakulima wetu na usawa katika biashara za kikanda.”