Tanzania kuvuna ujuzi wa Japan ujenzi wa miundombinu

Dar es Salaam. Tanzania inatarajia kujifunza teknolojia ya Japan ya ujenzi wa kisasa wa miundombinu katika maeneo korofi, yakiwamo yanayoathiriwa na majanga kama vile tetemeko.

Hayo yatafanyika kupitia kongamano la uwekezaji katika miundombinu kati ya Tanzania na Japan linalotarajiwa kufanyika Oktoba 3, 2024 jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Gilead Teri na Balozi wa Tanzania nchini Japan, Baraka Luvanda wameeleza hayo leo Oktoba mosi, 2024 katika mkutano na waandishi wa habari.

Kongamano hilo linakwenda kufanyika wakati ambao Tanzania inashuhudia ukuaji wa uwekezaji katika miradi mbalimbali nchini katika robo ya mwaka (Julai hadi Septemba 2024) kufikia 256 kutoka 137 mwaka uliotangulia.

Balozi Luvanda amesema tayari washiriki 60 kutoka kampuni tofauti wameshafika nchini kuhudhuria kongamano hilo.

Washiriki hao ni wanachama wa Chama cha Miundombinu kati ya Japan na Afrika ambao wamejikita katika ujenzi wa miundombinu hasa upande wa Afrika.

Amesema kuna fursa ya kutengeneza miundombinu ya muda mrefu kupitia kongamano hilo, akitoa mfano wa miundombinu iliyojengwa nchini Japan yenye uwezo wa kuhimili majanga.

“Kampuni hizi nyingi zinashughulika katika ujenzi wa barabara, viwanja vya ndege na bandari. Watakuwa hapa Oktoba 3 kwa ajili ya mkutano huu na wataendelea kuwapo hadi watakapokutanishwa na kampuni na taasisi za umma zinazohusika na ujenzi,” amesema.

Balozi Luvanda amesema anaamini kutokana na kongamano hilo uwekezaji unaofanywa na Japan utaonekana kuimarika kwenye ripoti za utendaji wa robo ya mwaka ujao.

“Baada ya mkutano huu huenda kuanzia Januari lile jedwali la uwekezaji alilokuwa analisema mkurugenzi likaonekana kupaa,” amesema.

Amesema pia kutakuwa na mikutano mbalimbali itakayowakutanisha washiriki hao kutoka Japan na watu waohusika na ujenzi wa miundombinu nchini.

Awali, Mkurugenzi wa TIC, Teri amesema kongamano hilo litakuwa fursa kwa Tanzania.

“Tutaweza kujifunza teknolojia ya kisasa ya ujenzi wa miundombinu katika maeneo magumu ikiwamo yale yanayosumbuliwa na majanga kama matetemeko ya ardhi,” amesema.

Kuhusu ongezeko la miradi iliyosajiliwa kati ya Julai hadi Septemba, mwaka huu amesema ukuaji umetokana na kuitambua sekta ya uwekezeji kama nyenzo ya kukuza uchumi na kuondoa umasikini ndani ya Watanzania.

“Mazingira bora ya uwekezaji yaliyowekwa, pia sheria, taratibu na utendaji kazi wa taasisi za Serikali zinazosimamia na kuwezesha mazingira ya uwekezaji nchini,” amesema.

Amesema kazi kubwa imekuwa ikifanywa na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali kwani wao ndio wanaoleta wawekezaji nchini.