
TIMU ya taifa ya vijana ya kriketi ina matumani ya kuendelea kufanya vyema katika michuano ya vijana wa chini ya miaka 19 ambayo inanza kuchezwa mjini Lagos, Nigeria mwishoni mwa juma hili.
Tanzania itafungua na Uganda kwenye Uwanja wa TBS Cricket Oval uliopo jijini Lagos, ambao ndiyo mahakama ya michuano hii ambayo itaanza rasmi siku ya Jumamosi, Machi 28 na kuhitimishwa Aprili 6 mwaka huu.
Michuano hii ambayo inashirikisha mataifa sita, ni kwa ajili kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia kwa vijana itayofanyika miezi ya mwisho wa mwaka huu.
Michuano ya mwaka huu inashirikisha timu kutoka mataifa ya Kenya, Uganda, Tanzania, Namibia, Sierra Leone, na wenyeji Nigeria.
“Vijana wamefanya mazoezi ya muda mrefu kupitia michuano mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kama Ligi B ya Hong Kong, Super League ya Dar na michuano ya vijana ya Pasaka ya iliyofanyika hivi karibuni nchini Uganda. Michuano hii imewapa vijana wetu mazoezi ya kutosha,” alisema Ateef Salim, msemaji wa chama cha Kriketi nchini (TCA).
Ikiwa nchini Uganda ambako ilipiga kambi, timu ya vijana ilicheza mechi tatu za kujipima nguvu na wenyeji na kushinda mbili na kupoteza moja.
Tanzania itaanza kampeni yake kwa kucheza na Uganda siku ya Jumapili Machi 29 mwaka huu kabla ya kuwakabili wenyeji Nigeria katika mchezo unaofuata Machi 30.
“Tulikutana na Uganda U19 mara mbili jijini Kampala na tumeshinda mechi zote mbili. Naamini tutakutana na timu ile ile na wachezaji wale wale tuliocheza nao michuano ya Pasaka,” ametanabaisha msemaji huyo wa TCA.
Tanzania itacheza mechi yake ya tatu na Namibia kwenye uwanja huohuo Aprili 1 mwaka huu.
Aprili 3, Tanzania itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya Kenya katika mchezo wake wa nne.
Mechi dhidi ya Sierra Leone Aprili 5 mwaka huu, ndiyo itakayohitimisha kampeni ya Tanzania kutaka kufuzu tena michuano ya dunia mwaka huu.