
Huenda ikawa ni jambo la kushangaza kwa wengi, lakini ukweli usiopingika ni kwamba Tanzania inaongoza katika uwekezaji nchini Kenya, licha ya kuwa nayo bado inaendelea kutafuta fursa zaidi za kuvutia wawekezaji wa ndani na wa kimataifa ili kukuza uchumi wake.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikiweka mikakati mbalimbali ya kuboresha mazingira ya biashara, ikiwa ni pamoja na kupunguza vikwazo vya uwekezaji, kuimarisha utawala wa kodi, na kuongeza uwekezaji katika sekta za kimkakati kama kilimo, nishati, madini, na utalii.
Ongezeko la uwekezaji wa Tanzania nchini Kenya ni ishara kwamba makampuni na wafanyabiashara wa Kitanzania wameongeza uwepo wao katika soko la Kenya, wakitumia fursa zilizopo kuwekeza katika sekta mbalimbali.
Takwimu za hivi karibuni zinaonyesha kuwa wawekezaji wa Kitanzania wamewekeza mtaji mkubwa nchini Kenya, wakipita hata baadhi ya mataifa ambayo kihistoria yamekuwa mstari wa mbele katika uwekezaji ndani ya nchi hiyo jirani.
Ongezeko la uwekezaji huo linaashiria kuongezeka kwa mvuto wa uchumi wa Kenya kwa wawekezaji wa kanda na wa kigeni, licha ya migogoro ya kibiashara inayoendelea kati ya Kenya na Tanzania kuhusu vikwazo visivyo vya kiforodha (NTBs).
Takwimu za hivi karibuni kutoka Sekretarieti ya EAC zinaonyesha kuwa Tanzania ilikuwa mwekezaji mkubwa zaidi nchini Kenya kati ya mwaka 2018 na 2023, ikiwa imewekeza jumla ya Dola 72.45 milioni (Sh192.85 bilioni) kwenye miradi 19. Tanzania ilifuatwa na Uganda, iliyowekeza Dola 36.91 milioni (Sh98.25 bilioni) na Rwanda Dola 3.69 milioni Sh9.82 bilioni.
Kwa mujibu wa takwimu zilizomo katika ripoti ya Biashara na Uwekezaji ya EAC ya mwaka 2023, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) ziliwekeza Dola 2.01 milioni na dola 250,000 mtawalia nchini Kenya katika kipindi husika, huku Sudan Kusini ikiwekeza dola 190,000.
Hata hivyo, wawekezaji wakuu nchini Kenya walitoka sehemu nyingine za dunia, wakiwekeza kiasi kikubwa cha dola 3.75 bilioni kwenye uchumi wa Kenya katika kipindi hicho.
Wawekezaji wanaweka fedha zao zaidi katika sekta muhimu kama uzalishaji wa bidhaa (manufacturing), uchukuzi, mawasiliano na uhifadhi, fedha na bima.
Sekta nyingine ni ardhi na huduma za biashara, kilimo, uvuvi, misitu na uwindaji, biashara ya jumla na rejareja, utalii na ujenzi.
Kwa ujumla uwekezaji wa ndani katika EAC ulipungua kwa asilimia 5.6 hadi dola milioni 567.17 mwaka 2023 kutoka dola milioni 600.78 mwaka 2022, huku idadi ya miradi ikishuka kutoka 76 hadi 72 katika kipindi hicho, kwa mujibu wa ripoti hiyo.
Uganda ilivutia uwekezaji mkubwa zaidi ndani ya EAC wenye thamani ya dola milioni 280.74, ingawa ulikuwa pungufu kutoka dola milioni 391 mwaka 2022, ikifuatiwa na Burundi iliyovutia dola milioni 155.18.
Miradi ya uwekezaji wa Burundi ndani ya EAC iliongezeka kutoka miradi miwili hadi minne, huku thamani yake ikipanda kutoka dola milioni 1.9 mwaka 2022 hadi dola milioni 155.18 mwaka 2023.
Uingiaji wa uwekezaji wa ndani ya EAC nchini Rwanda uliongezeka hadi dola milioni 55.16 kutoka dola milioni 46.78, huku idadi ya miradi ikiongezeka kutoka 15 hadi 18.
Ripoti inaonyesha kuwa uwekezaji wa Kenya ndani ya EAC ulipungua hadi dola milioni 1.32 mwaka 2023 kutoka dola milioni 22.6 mwaka 2022, huku ule wa Tanzania ukishuka hadi dola milioni 74.77 kutoka dola milioni 138.5 katika kipindi hicho.
Licha ya ongezeko la wawekezaji wa Kitanzania kwenye uchumi wa Kenya, nchi hizi mbili bado zinakabiliwa na migogoro ya kibiashara kuhusu vikwazo visivyo vya kiforodha (NTBs) vinavyodhoofisha biashara kati yao.
Nchi hizi mbili ziliafikiana kushughulikia angalau NTBs 14 kufuatia mkutano kati ya Rais William Ruto na mwenzake wa Tanzania, Samia Suluhu, mwaka 2023.
Mkutano huo ulizingatia masuala 14, sita kutoka Tanzania na nane kutoka Kenya na kutoa mwongozo wa kuyatatua. Hata hivyo, kati ya hayo 14, ni matatu tu yaliyotatuliwa kikamilifu.
Tanzania inaendelea kuikatalia Kenya kibali cha kuingiza bidhaa za kuku na mazao yake, ikiwemo vifaranga wa siku moja, mayai ya kuatamia, na nyama.
Wiki iliyopita, Tanzania iliweka ushuru mpya wa ulinzi kwa mayai, bidhaa za maziwa na nyama, pamoja na bidhaa za viwandani kama biskuti, hatua ambayo Kenya inadai imekiuka kanuni za umoja wa forodha wa EAC na kupunguza mapato ya mauzo ya nje.
Vita hivi vipya vya ushuru vinatishia kufungua upya mfululizo wa mvutano wa kibiashara kati ya nchi hizi mbili.
Chama cha wazalishaji wa Kenya (KAM) kimesema kuwa Tanzania imeweka ushuru wa asilimia 25 kwa mauzo ya nje ya mayai ya kuatamia kwenda Kenya, kinyume na utaratibu wa Umoja wa Forodha wa EAC.
Kenya na Tanzania zimekuwa zikijihusisha na migogoro ya mara kwa mara ya kibiashara kuhusu vikwazo vya ushuru na visivyo vya ushuru, jambo linalosababisha mara kwa mara uingiliaji kati wa mawaziri husika na hata viongozi wakubwa wa nchi.
Licha ya migogoro hiyo, takwimu zinaonyesha kuwa wawekezaji wa Kitanzania bado wanaiona Nairobi kama eneo la kuvutia kwa biashara.
Matajiri kadhaa wa Kitanzania kutoka Dodoma wamewekeza kwa kiasi kikubwa nchini Kenya, baadhi yao wakinunua kampuni za Kenya.
Miongoni mwa wawekezaji mashuhuri wa Kitanzania nchini Kenya ni Rostam Aziz ambaye kupitia Taifa Gas anajenga kiwanda cha gesi ya kupikia na maghala ya kuhifadhi tani 30,000 Mombasa, mradi wenye thamani ya Ksh16.9 bilioni ($131 milioni). Ally Awadh naye anajenga mradi kama huo lakini wa tani 10,000.
Awadhi ndiye mwanzilishi wa Lake Oil ya Tanzania, ambayo ilinunua kitengo cha rejareja cha mafuta cha Hashi Energy ya Kenya kwa kiasi kisichofichuliwa mwaka 2017.
Familia ya mfanyabiashara mkubwa wa Tanzania, Abdallah Nahdi, kupitia Amsons Group, pia imenunua kampuni ya saruji ya Bamburi kwa makadirio ya dola 180 milioni.
Mwaka 2017, wawekezaji wa Kitanzania Aunali na Sajjad Rajabali walinunua hisa milioni 30.2, sawa na asilimia 2.06 ya umiliki wa kampuni ya mafuta ya Kenokobil, na kuwa miongoni mwa wenye hisa wakubwa wa kampuni hiyo.
Mwaka 2016, Benki ya Tanzania, Bank M, ilikuwa benki ya kwanza kutoka nchi jirani kuinunua taasisi ya kifedha ya Kenya kwa kununua asilimia 51 ya hisa za Benki ya biashara ya Oriental.
Biashara katika nchi nyingine
Takwimu za Benki ya Uganda zinaonyesha kuwa katika mwaka ulioishia Juni 2024, Uganda iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola 4.17 bilioni (Sh10.98 trilioni) kutoka Soko la Pamoja na Mashariki na Kusini mwa Afrika (Comesa) na sehemu nyingine za Afrika, ambapo karibu nusu ya bidhaa hizo zilikuwa kutoka Tanzania.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Mamlaka ya Mapato ya Uganda (URA), Uganda huagiza dhahabu, chuma cha pande zote au chuma kisichochanganywa, karanga na chupa kutoka Tanzania.
Dhahabu inachangia zaidi ya nusu ya bidhaa zinazoingizwa Uganda kutoka Tanzania. Takwimu za URA zinaonyesha kuwa Uganda iliagiza dhahabu yenye thamani ya Sh1.08 trilioni mwaka 2023.
Data zinaonyesha kuwa asilimia 42.56 ya bidhaa zinazoingizwa Uganda kutoka ndani ya Afrika katika mwaka ulioishia Juni 2024, zilikuwa kutoka Tanzania, ikilinganishwa na asilimia 19.55 kutoka Kenya na asilimia 6.43 kutoka Afrika Kusini.
Kwa takwimu hizo, Tanzania iliipiku Kenya kama chanzo kikubwa zaidi cha bidhaa za Uganda, ikionesha mabadiliko katika biashara, hasa ndani ya Afrika. Ikumbukwe kuwa Kenya ndilo taifa namba moja kiuchumi ndani ya EAC.
Kwa muda mrefu Kenya imekuwa mshirika mkuu wa kibiashara wa Uganda, lakini taarifa zinaonyesha kwamba nchi hiyo yenye uchumi mkubwa zaidi Afrika Mashariki, sasa iko nafasi ya pili baada ya Tanzania kwa kuwa chanzo kikubwa cha bidhaa zinazoingizwa Uganda kutoka ndani ya Afrika.
Kufuatia hatua hiyo, Rais William Ruto aliisifu Tanzania alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya miaka 25 ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) jijini Arusha Novemba 29, 2024, akikiri kupungua kwa nafasi ya Kenya kama kinara wa biashara ya kanda na kupongeza maendeleo ya Tanzania.
“Ninaipongeza Tanzania kwa kuipiku Kenya katika bidhaa na huduma tunazofanya biashara ndani ya Afrika Mashariki. Kenya ilikuwa nchi inayoongoza kwa bidhaa na huduma katika ukanda huu. Leo, Tanzania imeipita Kenya,” Ruto alisema.
Mwenendo wa biashara kati ya Tanzania na Kenya
Mwaka 2023 Kenya ilirejesha nafasi yake katika biashara baina yake na Tanzania, baada ya kuipoteza mwaka uliopita.
Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) iliyochapishwa Desemba 31, 2023 inaonyesha, Kenya iliuza bidhaa zake nchini kwa asilimia 31, zaidi ya kiwango ambacho Tanzania iliuza kwao, ikiwa ni tofauti na mwaka uliotangulia ambapo Tanzania iliuza katika nchi hiyo kwa asilimia 10 zaidi.
Hiyo ikiwa na maana kuwa, bidhaa za Sh1.06 trilioni ziliingizwa nchini kutoka Kenya ikilinganishwa na bidhaa za zaidi ya Sh724.32 bilioni za Tanzania zilizouzwa nchini kwao mwaka 2022/2023.
Habari hii kwa mara ya kwanza iliripotiwa na tovuti ya gazeti la The East African, Machi 28, 2025.