
KUSHINDA mechi ya ufunguzi wa michuano ya ICC League B dhidi ya Italy na tatu nyingine zinazofuata, ndio azma kuu ya timu ya Tanzania katika ligi hii kimataifa inayoanza kuchezwa rasmi ijumaa hii nchini Hong Kong.
Ikiwa na matumaini makubwa ya ‘kupindua meza’ nchini Hong Kong, timu ya Tanzania ambayo iliagwa rasmi na mwenyekiti wa Chama Cha kriketi nchini Dr. B.S. Sreekumar, imepania kufanya vizuri katika hatua ya pili ya mashindano haya na kufuta aibu ya kufanya vibaya katika hatua ya awali ya michuano iliyochezwa Uganda ambako Tanzania ilipoteza michezo yake yote.
“Naomba Watanzania wote tuwaunge mkoni vijana wetu ili wafanye vizuri zaidi katika michuano hii na kuipa kriketi ya Tanzania hadhi kubwa kimataifa,” alisihi mwenyekiti huyo wa TCA.
Timu ya wachezaji 14 na viongozi wawili ndiyo iliyoko nchini Hong Kong na juma hili imekuwa na mazoezi ya kina ili kuhakikisha inakuwa na uimara wa kukabiliana na upinzani kutoka timu yoyote, kwa mujibu wa msemaji wa Chama cha Kriketi nchini(TCA), Ateef Salim.
“Vijana wameondoka wakiwa wameiva barabara baada ya mazoezi ya muda mrefu jijini Dar es Salaam,” alisema Salim.
Kwa mujibu wa ratiba ya mashindano, mechi zote za ICC Ligi B zitachezwa katika viwanja vya Kowloon na Mission Road Ground kilichopo katika mji wa Mong Kok ambacho mechi yake ya ufunguzi itakuwa kati ya Uganda na Bahrain.
Tanzania itacheza mechi yake ya pili dhidi ya Bahrain tarehe 9 Februari katika uwanja wa Mission Road Ground mjini Mong Kok wakati katika uwanja wa Kowloon Singapore na Uganda zitakuwa kibaruani.
Tanzania itaingia tena uwanjani Februari 12 kupambana na wenyeji Hong Kong katika uwanja wa Mission Road.
Tanzania itakuwa na kibarua kingine tarehe 15 Februari, safari hii ikimenyana na Uganda katika uwanja wa Mission Road.
Tanzania itamaliza ratiba yake tarehe 16 Februari kwa kupambana na Singapore katika uwanja wa klabu ya Kowloon mjini Kowloon
Wachezaji waliopo Hong Kong kwa ajili ya michuano hii ni Ally Mpeka Kamote, Akhil Anil Amal Rajeevan, Arshaan Ayzaz Jessani, Ivan Ismail Suleiman, Khalid Amiri Juma na Kassim Nassoro.
Wengine ni Laksh Bakrania, Mohamed Kitunda, Mohamed Simba, Mohamed Yunus Issa, Mukesh Maker, Rajendra Assure na Sivara Selvaraj.
Timu itaongozwa na Mwalimu Pushpa Kumar na Adil Kasam ambaye ni meneja wa timu.
Katika michuano iliyofanyika nchini Uganda mwaka jana, Tanzania ilicheza michezo minne na ilipoteza michezo yote, hali ambayo TCA haitaki ijirudie tena nchini Hong Kong.