Tanroads yapangua watendaji kusuasua mradi wa BRT4

Tanroads yapangua watendaji kusuasua mradi wa BRT4

Dar es Salaam. Takriban wiki moja baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega kutoa maagizo ya kufanyika kwa uchunguzi dhidi ya mwenendo wa ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka (BRT), awamu ya nne, Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) imetangaza kufanya mabadiliko ya baadhi ya watendaji wa BRT. 

Mabadiliko hayo yanamhusu Mhandisi Mkazi wa Mradi huo wa BRT4 anayesimamia sehemu ya kwanza inayoanzia Maktaba – Mwenge – Ubungo jijini Dar es Salaam, Mhandisi Rajabu Iddi Rajabu pamoja na wataalamu wengine.

Akitoa taarifa hiyo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Japherson Nnko, ameeleza kuwa hatua hiyo imechukuliwa kutokana na mkandarasi anayetekeleza ujenzi huo kufumua barabara katika eneo jipya la Palm Beach, Upanga kabla ya kukamilisha kazi muhimu katika maeneo ya awali ya barabara hiyo kutoka Morocco – Mwenge hadi Nkunda.

Nnko alisema wameamua kuchukua hatua hiyo kutokana na maagizo ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega aliyoyatoa jijini Dar es Salaam Mei 16, 2025 baada ya kufanya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa mradi huo na kubaini uzembe uliosababisha usumbufu katika barabara hiyo ambayo ni kinyume na malengo ya mradi.

Katika pangua pangua iliyotangazwa jana, Tanroads imefanya maboresho ya usimamizi wa miradi ya BRT4 na ya kwanza ambapo Mhandisi Allen Natai atasimamia BRT awamu ya kwanza wakati Mhandisi Justin Moshi na Mhandisi Issa Mohamed watasimamia BRT awamu ya nne lengo likiwa ni kuhakikisha miradi hiyo inasimamiwa na kutekelezwa kwa karibu na ipasavyo.

Mhandisi Nnko ametumia taarifa hiyo ya jana kutoa rai kwa makandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa barabara hasa kwenye maeneo ya miji yenye changamoto ya msongamano wa magari kuhakikisha wanafanya kazi kwa mujibu wa utaratibu wa kimkataba na kufuata maelekezo ya mhandisi mshauri.

Aidha, amewataka wasimamizi kutoka Tanroads kuhakikisha wanawasimamia wahandisi washauri na makandarasi wanaotekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu nchini kwa karibu, ili kuhakikisha miradi hiyo inatekelezewa kwa wakati uliopangwa.

Ujenzi wa mradi wa BRT4 sehemu ya kwanza unatekelezwa na Mkandarasi China Geo – Engineering Corporation na kusimamiwa na Mhandisi Mshauri Kunhwa Engineering Consulting Company Ltd ambapo utakuwa na jumla ya vituo 18 vya mwendokasi.

Mradi huo ukikamilika unatarajiwa kupunguza msongamano wa magari katikati ya  jiji la Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *