
ZINAPOCHEZA Simba na Yanga zinakuwa na rekodi mbalimbali na vitu vya kuvutia kutokana na ukongwe wa klabu hizo tangu Ligi ya Tanzania ilipoanzishwa mwaka 1965.
Katika dabi ya keshokutwa, kuna vitu vingi ambavyo mashabiki wanatarajia kuviona mojawapo ni timu ipi itatangulia kucheka na nyavu na dakika 90 zitaishaje. Mwanaspoti limekusanya takwimu za bao la kwanza kwa misimu saba ya mwisho iliyopita ambapo kuna mechi zilizomalizika kwa sare, suluhu na mojawapo ikivuna pointi tatu.
Msimu 2018/19
Yanga 1-1 Simba (Oktoba 28)
Mechi ya Oktoba 28 Yanga 1-1 Simba, dakika ya 58 Shiza Kichuya ndiye aliyeipa uongozi Simba kabla ya dakika ya 60 Obrey Chirwa kusawazisha ikiwa ni tofauti ya dakika tatu. Lakini katika mzunguko wa pili Simba ilishinda bao 1-0 Yanga (Aprili 29) ikilinda bao na kuvuna pointi tatu.
Msimu 2019/20.
Simba ilianza kufunga kupitia kwa Meddie Kagere na ikaongeza morali ikapata bao la pili lililofungwa na Francis Kahata, ambapo Yanga haikukata tamaa kwani Balama Mapinduzi alianza kufunga bao la kwanza wachezaji wakapata nguvu hadi likapatikana la kusawazisha kupitia kwa Mohamed Issa ‘Banka’ na dakika 90 zikamalizika kwa sare ya mabao 2-2. Hiyo ilikuwa Junuari 4, lakini mzunguko wa pili Yanga 1-0 Simba (Machi 8) na ikalinda bao hilo hadi dakika 90.
Msimu wa 2020/21
Mchezo uliopigwa Novemba 7, 2020 Yanga ilikuwa ya kwanza kucheka na nyavu, lakini Simba haikukubali unyonge ikasawazisha na mechi ikamalizika kwa sare ya bao 1-1, huku mechi ya mzunguko wa pili Simba 0-1 Yanga (Julai 3).
Msimu wa 2021/22
Msimu wa 2021/22 haukuwa wa kufungana kuanzia mzunguko wa kwanza Simba 0-0 Yanga (Desemba 11) na Aprili 30, Yanga 0-0 Simba na kufanya mtaani kusiwe na kelele za kutambiana.
Msimu wa 2022/23
Mchezo wa Oktoba 23 Simba ndiyo ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia kwa Augustine Okrah katika dakika ya 15, lakini Yanga ikasawazisha dakika ya 45 kupitia kwa Stephane Aziz Ki, huku mzunguko wa pili Simba 2-0 Yanga (Aprili 16).
Msimu wa 2023/24
Dabi ya Novemba 5, 2023; Simba 1-5 Yanga ambayo ilionekana kucheza kwa ubora zaidi kuliko mtani wake na bado mzunguko wa pili haukuwa mzuri Msimbazi ambapo Yanga ilishinda mabao 2-1 (Aprili 20) – mabao ya Yanga yalifungwa kipindi cha kwanza na Stephane Aziz Ki kwa penalti katika dakika ya 20 na Joseph Guede ile ya 38, huku Simba ikifunga bao la kufutia machozi dakika ya 74 kupitia Freddy Michael.
Msimu wa 2024/25
Katika msimu huu mechi ya kwamba ilikuwa Simba 0-1 Yanga (Oktoba 19), ushindi Jangwani ukitokana na bao la kujifunga la Kelvin Kijili. Kwa sasa inasubiriwa mechi ya mzunguko wa pili kujua nani ataibuka mbabe dhidi ya mwingine msimu huu.
WASIKIE HAWA
Kiraka wa zamani wa Simba, Erasto Nyoni ambaye kwa sasa anacheza Namungo anasema: “Presha ya mashabiki ndio inayofanya mechi za Simba na Yanga zionekane za kipekee, kwa uzoefu wangu hazijawahi kuzoeleka. Timu inayokuwa inatangulia kufunga inakuwa inajiamini zaidi pia inakuwa chachu kwa iliyofungwa kujituma zaidi na anaweza akamaliza mshindi.”
Kwa upande wa beki wa zamani wa Yanga, Oscar Joshua anasema: “Utakuwa mchezo mgumu, kikubwa wachezaji waweke akili katika mchezo na mambo ya nje ya uwanja wawaachie mashabiki.”