
STRAIKA wa magoli aliyewahi kuwika na Simba, Yanga na sasa Meneja wa Singida Black Stars,Amissi Tambwe anaona uwezekanako wa Jonathan Sowah kufanya sapraizi kwenye ufungaji bora msimu huu.
Sowah amejiunga na Singida Black Stars dirisha dogo la usajili hadi sasa amecheza mechi sita na kupachika mabao saba kambani akiachwa mabao matano na kinara wa upachikaji wa mabao msimu huu ambaye ni Charles Ahoua akiingia kambani mara 12.
Akizungumza na Mwanaspoti, Tambwe aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara akiichezea Yanga msimu wa 2015/2016 alipofunga mabao 21 na rekodi hiyo imedumu kwa misimu minane ndani ya kikosi hicho hadi msimu uliopita ilifikiwa na kiungo, Stephane Aziz Ki, alisema Sowah ni mshambuliaji ambaye ana uchu wa mabao na ana malengo ya mafanikio.
Tambwe alisema Sowah ni mshambuliaji mzuri na hatari akiwa mbele ya goli na ni mpambanaji ambaye anauchu wa kuingiza mpira kambani kwa ubora huo anauwezo wa kuwafikia washambuliaji walio mbele yake huku akisisitiza kuwa licha ya kuanza kati kati ya msimu lakini ameonyesha uwezo mkubwa.
“Hajaachwa mbali na wafungaji bora hadi sasa ambao wamefunga mabao 10 kwa kasi anayoonyesha akiendelea nayo naamini anaweza kufikia mabao hayo kwasababu ni mchezaji ambaye anajicho la kuona goli na amekuwa akitamani kufunga kwenye kila mchezo akikosa nafasi anaumia,” alisema na kuongeza;
“Mechi sita amefunga mabao saba unajiuliza angeanza msimu angekuwa na mabao mangapi kwenye mechi zilizobaki akifunga bao kwenye kila mchezo anaweza akafunga mabao mengi na kufika mbali zaidi ya waliomzidi ambao wakipoteza nafasi hata moja anawaacha mbali.”
Nyota huyo aliyewahi kuichezea Simba ambayo pia aliwahi kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2013-2014 baada ya kufunga mabao 19, aliweka wazi Sowah ni mchezaji ambaye anauwezo wa kutengeneza nafasi na kujiweka katika nafasi za kufunga sio rahisi kupoteza nafasi na ndio maana amefunga mabao mengi zaidi ya mechi alizocheza.
Mbali na Tambwe kuzichezea Yanga, Simba ila timu nyingine aliyoichezea hapa nchini ni Singida Fountain Gate aliyoondoka mwaka 2022.
Sowah aliyefunga mabao saba katika Ligi Kuu Libya akiwa na Al Nasr msimu wa 2023/24, tayari ameanza kuonyesha uwezo kwenye kikosi cha Singida Black Stars akifikia rekodi yake mwenyewe kwenye mechi sita alizocheza hadi sasa.