Tanzania kama ilivyo kwa nchi zingine za Kusini mwa Jangwa la Sahara ina idadi kubwa ya mifugo ya asili kuliko iliyoboreshwa. Hivyo, kaya zinazojishughulisha na ufugaji zinafuga mifugo ya asili.
Kwa mujibu wa Sensa ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ya Mwaka 2019/20, jumla ya kaya zilizojihusisha na ufugaji wa mifugo zilikuwa 2,747,910, ambapo kati ya hizo kaya 2,683,454 zilikuwa Tanzania Bara na 64,456 zilikuwa Tanzania Visiwani kati ya kaya 12,007,839 zilizopo Tanzania (11,659,589 Tanzania Bara na 348,250 Tanzania Visiwani). Hata hivyo, kwenye kipindi hicho sekta ya mifugo ilichangia asilimia 7.1 kwenye pato la Taifa.
Lakini pia Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa wingi wa mifugo ikitanguliwa na Ethiopia huku nafasi ya tatu ikishikwa na Sudan ambapo takwimu zinaonyesha Tanzania kuna jumla ya ng’ombe 36.6 milioni, mbuzi 26.6 milioni na kondoo 9.1 milioni, kuku wa asili 45.1 milioni, kuku wa kisasa 52.8 milioni na nguruwe 3.7 milioni.
Kwa muktadha huo, Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhakikisha inakuza sekta ya mifugo nchini kwa kuziwezesha taasisi zilizo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ili kuongeza pato la uzalishaji na kuboresha kipato na maisha ya wafugaji.
Kwa mujibu wa sheria ya TALIRI kifungu cha 5 kifungu kidogo cha 6 (i–iii) taasisi hiyo imepewa mamlaka ya; (i) kuibua, kufanya na kuendeleza tafiti za sayansi za msingi na kutumia matokeo ya tafiti za msingi kukuza teknolojia za ufugaji, (ii) kushirikiana na wanasayansi wa ndani na nje ya nchi kuibua tafiti zinazolenga kuongeza tija na matokeo chanya kwa nchi yetu na (iii) kuweka na kuimarisha mifumo ya ushauri elekezi na ushirikiano kati ya TALIRI na taasisi zinazoendana na tafiti za mifugo.
Katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya awamu ya sita bajeti ya maendeleo ya TALIRI imeendelea kuongezeka kwa asilimia 27.
Ambapo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo TALIRI ilitenga bajeti ya Sh 1 bilioni kwa mwaka wa fedha 2021/2022 kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya utafiti, ununuzi wa vifaa shamba ambavyo kwa kiasi kikubwa vimeboresha shughuli za uibuaji wa teknolojia bora za mifugo na kutekeleza miradi ya utafiti kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
Bajeti hiyo imeeendelea kupanda hadi kufikia Sh 4.67 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na hivyo kuwezesha utekelezaji wa kazi za utafiti na kuimarisha mashirikiano na wadau wengine katika mnyororo wa utafiti ndani na nje ya nchi.
Rais wa awamu ya sita amekuwa na ari kubwa ya kuimarisha muhusiano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na nchi mbalimbali ambazo zimekuwa ni wadau wa maendeleo katika sekta ya mifugo na kutoa misaada iliyochangia utekelezaji wa tafiti kwa kusaidia kazi za kuibua na kusambaza matokeo ya teknolojia bora za mifugo ambapo katika kipindi hicho, taasisi ilifanikiwa kupokea jumla ya Sh 5.63 bilioni kutoka kwa wadau wa maendeleo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya utafiti.

Shamba la ekari 250 la malisho yaliyoboreshwa aina ya Cenchrus ciliaris lililopo TALIRI Kongwa.
Miradi hio ni pamoja na mradi wa maziwa faida unaolenga kuongeza thamani ya mnyororo wa ng’ombe wa maziwa nchini, mradi wa AADGG unaolenga kuboresha mbari za ng’ombe wa maziwa, mradi wa Enviro cow unaolenga kufanya utafiti wa ng’ombe wa maziwa mwenye tija na kuzalisha hewa kidogo ya joto (Methane). Mradi huu unajikita katika kuhakikisha mazingira yanalindwa kwa kuzingatia ufugaji wenye tija.
Mradi wa BBT wenye lengo la kuwajengea uwezo vijana ili wapate ujuzi wa ujasiriamali katika ufugaji na unenepeshaji mbuzi ili kupunguza tatizo la ajira, mradi wa TPGS ambao unafanya utafiti juu ya tathimini na uchambuzi wa kimuonekano (vina saba) kwa kuku wa asili jamii ya Horas, mradi wa AMR unaolenga kufuatilia udhibiti wa usugu wa vimelea sugu vya magonjwa dhidi ya dawa.
Miradi mingine ni; mradi wa RESSCOMM II unaoshughulika na mambo ya kiikolojia kwa lengo la kusaidia wafugaji kuzalisha kwa tija kwenye mazingira kame, mradi wa SUPPLING unaotoa mafunzo kwa vijana wajasiriamali wenye taaluma ya mifugo ili kuchochea kasi ya utoaji wa huduma za ugani kwa njia ya kidigitali kupitia mpango wa atamizi na mradi wa PREVENT ambao unawajengea uwezo wataalamu wa mifugo kutumia mbinu shirikishi jamii na ugani kwa lengo la kuhimiza na kuwezesha uchanjaji kuku wenye ufanisi kwa wakati huu na ujao. Miradi hii imeweza kunufaisha zaidi ya wafugaji 7,000 nchini.
Kadhalika taasisi imeendelea kutekeleza shughuli zake za kawaida kupitia fedha za makusanyo ya ndani na ruzuku ya matumizi mengineyo kutoka Serikali Kuu ambapo imefanikiwa kuwa na ongezeko la bajeti ya fedha za matumizi mengineyo kutoka Sh 1.4 bilioni kwa mwaka wa fedha 2023/2024 hadi Sh 1.45 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/2025.
Katika kuongeza wigo wa kufanya utafiti na kuongeza tija na uzalishaji wa teknolojia zinazolenga kupunguza changamoto za wafugaji, TALIRI imefanikiwa kuanzisha kituo cha Kanda ya Magharibi kiitwacho TALIRI Nsimbo (Halmashauri ya Nsimbo mkoani Katavi) kinachohudumia mikoa ya Katavi, Kigoma, Tabora na Rukwa. Uwepo wa kituo hiki unawezesha wadau/wafugaji wa Kanda ya Magharibi kupata teknolojia bunifu zinazoendana na Kanda hiyo.
Mafanikio mengine ya TALIRI ni kukamilisha utafiti na usajili wa aina tano za mbegu za malisho ya mifugo zikiwemo Cenchrus ciliaris (TALIRICENCH 1), Medicago sativa (TALIRIALFA 1), Desmodium intortum (TALIRIDESMO 1), Macroptilium atropurpureum (TALIRIMACRO 1) na Chloris gayana (TALIRICHLO 1) huku mkakati ukiwa ni kuzalisha kwa wingi mbegu hizo na kuzisambaza kwenye maduka ya pembejeo za kilimo.
Aidha, katika mwaka wa fedha unaoendelea 2024/2025 TALIRI imepanga kutekeleza miradi ya maendeleo kwa fedha kutoka Serikali Kuu yenye gharama za kiasi cha Sh 1.4 bilioni ambayo utekelezaji wake unaendelea ukiwemo, mradi wa kuendeleza Kituo cha Kanda ya Magharibi TALIRI Nsimbo, Uchimbaji na ujenzi wa miundombinu ya maji katika vituo vinne vya TALIRI Nsimbo, TALIRI West Kilimanjaro, Msowero na Mnima, Ujenzi wa mabanda ya mbuzi, Uzalishaji wa mbegu za malisho zilizothibitishwa, vyakula vya mifugo kwa ajili ya BBT na ujenzi wa ukarabati wa miundombinu ya mifugo katika vituo vya TALIRI kikiwemo kituo cha Tanga, Mpwapwa, Mabuki, Uyole, Naliendele, West Kilimanjaro na Kongwa. Miradi mingine ya utafiti inayotekelezwa kwa fedha za wadau wa maendeleo ni miradi ya Maziwa Faida, AADGG, Enviro Cow na TPGS.
Ili kuhakikisha wafugaji wanaendelea kupata teknolojia bora za malisho na mbegu bora za malisho TALIRI imeendelea kuhamasisha na kutekeleza kwa vitendo kampeni ya TUTUNZANE MVOMERO iliyoanzishwa na Mhe. Rais Dk Samia Suluhu Hassan ikiwa na maana ya mkulima wa mazao kumtunza mfugaji na mfugaji kumtunza mkulima wa mazao yenye lengo la kuondoa migogoro baina ya wafugaji na wakulima wa mazao.
Katika utekelezaji wa mipango ya baadae ya taasisi kwa mwaka ujao wa fedha 2025/2026 TALIRI imepanga kutekeleza vipaumbele vya utafiti katika maeneo yafuatayo; kilimo cha malisho na uzalishaji wa mbegu za malisho, mbari za mifugo, vyakula vya mifugo, afya ya mifugo, virutubisho asilia, tabia nchi na haki za mifugo na kuwajengea uwezo wataalamu.