Dar es Salaam. Alizaliwa akiwaona baba na mama wakiishi pamoja. Licha ya kuwa familia yao haikuwa na uwezo mkubwa kiuchumi, walikuwa na furaha na waliishi kwa upendo.
Hali iliendelea hivyo hadi alipofikisha miaka saba ambapo wazazi wake walitengana na yeye na ndugu zake wengine kubaki na mama yao.
Maisha yalianza kubadilika, baba hakuwa tena sehemu ya maisha yake, mama ndio akawa kila kitu kwake hadi pale alipoolewa tena.
Huyu ni Khamis Shuweri akisimulia namna kutengana kwa wazazi wake kulivyomfanya apoteze mwelekeo wa maisha, hadi kujihusisha na makundi yasiyofaa na hatimaye kudondokea kwenye biashara ya dawa za kulevya huko visiwani Zanzibar alikozaliwa na kuishi.
Shuweri ambaye kwa sasa ni baba wa watoto watano anasema hatamani kuona watoto wake wanapitia maisha aliyopitia yeye hali inayomfanya kusimama imara kuhakikisha wanakuwa katika misingi bora ya malezi ya familia.
“Tulishazoea kuna baba na mama lakini sasa mama yuko peke yake, mimi na dada yangu tukapelekwa kwa babu mzaa mama maisha yetu mapya yakaanza huko. Kwa kuwa babu alikuwa akiishi peke yake, sisi tukawa wasaidizi wake dada akipika chakula mimi naangalia mifugo.
Baada ya muda mama aliolewa lakini bado tuliendelea kuishi na babu, nikiri kwamba babu hakuwa na uangalizi mkubwa dhidi yetu nikaanza utundu ambao haukuwa mzuri. Bahati haikuwa upande wetu babu alifariki ikabidi twende kwa mama,”
Anasema huo ukawa mwanzo wa maisha mapya, alikwenda kuishi kwa baba wa kambo,licha ya kuwa hakupitia mateso kutoka kwa baba huyo kuna wakati aliliona pengo la kumkosa baba.
“Haikuchukua muda mrefu baba yetu wa kambo akapata uhamisho wa kikazi na kutakiwa kuhamia mkoani Mbeya. Kipindi hicho nilikuwa darasa la sita, sikukubaliana na maelekezo ya kuhama nikawaambia wao waende mie nitabaki niendelee kusoma.

Kwa sababu tulikuwa tukiishi jirani na mama yangu mdogo, hoja yangu ikakubaliwa lakini kumbe lilikuwa kosa kubwa. Nilipata uhuru ambao uliniingiza kwenye matatizo makubwa na kuvuruga kabisa mwelekeo wa maisha yangu”anasema Shuweri.
Akiwa darasa la sita akaanza kujihusisha na biashara ya kutembeza mitumba baada ya kushawishiwa na rafiki yake aliyekuwa akifanya biashara hiyo.
Anasema alianza kwa kutembeza nguo za mitumba baada ya kutoka shuleni lakini kadiri alivyokuwa akipata pesa akawa anashawishika wakati mwingine kukwepa masomo.
“Siku nyingine nikawa siendi shule kabisa nauza mitumba, hapa nikaanza kujihusisha na makundi yasiyofaa. Zile fedha nilizokuwa napata nikajikuta naanza kuvuta bangi.
“Iliendelea hivyo kwa muda kidogo na nilipofika darasa la saba nikawa tayari nimeshakolea, nikaamua kuacha shule rasmi sasa nikawa kwenye maisha ya uraiani. Haya yote niliyafanya kwa sababu sikuwa na mwongozo, maisha yangu nilikuwa nayaendesha mwenyewe,”.
Aliendelea na biashara ya mitumba huku akijihusisha na mchezo wa mpira wa miguu, siku moja akiwa mchezoni, alikutana na rafiki yake ambaye alimtambulisha kwenye ulimwengu wa dawa kulevya za viwandani.
“Nakumbuka tulikuwa na mechi sasa kuna mshkaji wangu alikuwa anachezea timu nyingine, baada ya mchezo kuisha tukawa tumetafuta chimbo tunavuta bangi. Alinipa bangi aliyotengeneza nilipovuta nilihisi ina kitu tofauti. Kesho yake nilipomuuliza kulikuwa na kitu gani kwenye ile bangi ndipo aliponieleza kwamba ilichanganywa na brown powder.
“Nilishtuka sikuwahi kufikiria kwamba kuna siku ningevuta unga, lakini nilipofikiria ule msisimko niliopata ikabidi nimuombe tena na hatimaye akanielekeza sehemu ninayoweza kupata,”anasimulia.
Huo ndiyo ukawa mwanzo wa Shuweri kutumia dawa za kulevya, kwa kuwa shughuli zake zilikuwa mjini akawa anaagizwa na wenzie waliokuwa shamba hivyo kila siku akawa anarudi na kete za watu kadhaa.
“Unajua habari mbaya husambaa sana, wahuni wengi wakajua kwamba kwenda kwangu mjini ni rahisi kuwabebea unga wakawa wananiagiza, wakaendelea kuambiana nikajikuta natakiwa kubeba kete nyingi kwa ajili ya marafiki.
“Nilifanya hivyo kwa muda nikaona kwanini nisifanye biashara, yaani niwe nachukua mzigo halafu nafunga mwenyewe nawauzia kete washkaji. Nikaanza hiyo biashara vijana wavuta unga wote wakawa wanajua mzigo unapatikana kwangu. Habari zangu zikafika polisi nikaanza kuwindwa,’’ anasema.
Hali hiyo ikamfanya na yeye atafute mbinu za kujilinda ili asiingie mikononi mwa polisi kwa sababu tayari alishakuwa tegemezi kwa familia yake.
“Hakuna mtu kwenye familia yetu aliyeamini kama nauza dawa za kulevya, nilikuwa mwepesi kusaidia kila nilipohitajika na hata wadogo zangu kule Mbeya nilikuwa nagharamia mahitaji yao yote ya shule. Familia nzima ilijua nafanya yote hayo kutokana na biashara ya mitumba.
“Sasa hawa polisi kuanza kunifuatilia niliona kama kikwazo hivyo nikaweka watu wangu kuanzia jirani na kituo cha polisi hadi njia ya kufika nyumbani kwangu ili wanipe taarifa kila wanapoona gari la polisi linakuja uelekeo wa kwangu.
Kwa njia hiyo haikuwahi kutokea operesheni yoyote ya kumkamata yeye iliyofanikiwa kwani alikuwa na uwezo wa kutoroka kabla askari kumfikia. Aliendelea kuwakwepa kwa namna hiyo huku akizidi kujenga himaya yake.
Alitokaje huko
Baada ya kuwa anatafutwa kila kona Zanzibar akakimbilia jijini Dar es Salaam, haikumchukua muda mrefu kabla ya kupata ajira kwenye ofisi ya kuosha magari.
Alifanya kazi hiyo huku akiendelea na matumizi ya dawa za kulevya lakini kifo cha dada yake kilimfanya afikirie mara mbili kuhusu matumizi ya dawa hizo haramu.
“Nilipata taarifa kuwa dada yangu kipenzi anaumwa saratani na amelazwa hospitali, lakini unga ulinifanya nisifikirie kwenda kumuangalia hospitali licha ya kuambiwa kwamba ananiulizia.
“Dada yangu alikaa hospitali hadi anafariki sijakanyaga, siku niliyoambiwa amefariki ndiyo nikashtuka na kuona kuna mahali hizi dawa zinanipeleka sio kuzuri.Niliumizwa mno na kifo cha dada yangu nikaona hii ndiyo inaweza kuwa sababu ya mimi kuacha nikaanza jitihada za kutafuta usaidizi wa kuacha,” anasema na kuongeza:
“Haikuwa rahisi kila nilipojaribu nilishindwa nikajikuta narudi tena kutumia hadi siku moja nilipoenda Zanzibar na kukutana na rafiki yangu mmoja aliyenipeleka sober house. Rafiki yangu huyu tulikuwa tunavuta unga wote hapo awali lakini safari hii nilimuona amebadilika anaonekana ana afya njema, ndipo nilipomueleza changamoto ninayopitia.
Huo ndio ukawa mwanzo wa safari ya Shuweri kutoka kwenye uraibu wa dawa za kulevya, akaanza kupata matibabu na ushauri nasaha uliowezesha kumjenga kisaikolojia na kujiondoa kabisa kwenye matumizi ya dawa hizo.
Ni miaka 15 sasa tangu aachane na matumizi ya dawa za kulevya sasa amekuwa miongoni mwa vinara wanaowanasua vijana kutoka kwenye uraibu wa dawa hizo ambazo zinagharimu na kuharibu maisha ya vijana wengi.
Kupitia shirika lake la New Vision of Life Society lililopo Mapinga wilayani Bagamoyo, Shuweri anatoa elimu ya ushauri nasaha kwa vijana wanaotumia dawa za kulevya na kuwanusuru vijana wa rika balehe wasiangukie kwenye uraibu huo.
“Kuna uwezekano mkubwa kwa watoto na vijana walio huru kujikuta wakiingia kwenye matumizi ya dawa za kulevya, tunawaelimisha wasifike huko huku tukisisitiza pia wazazi na walezi kuwaangalia watoto wao. Mimi niliyopitia sitamani apitie mtoto au kijana mwingine. Mapito hayo yalinifanya hata nichelewe kuanzisha familia lakini nashukuru sasa ni baba nina mke na watoto,”