
Moshi. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kilimanjaro, imezuia Sh329 milioni zilizopangwa kutumika kununua jenereta mbili kwa ajili ya iliyokuwa Mamlaka ya Uendeshaji na Uendelezaji wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KADCO), baada ya kugundua kuwa hazina ubora unaotakiwa.
Akizungumza kuhusu ripoti ya robo ya kwanza ya mwaka leo Jumatatu, Novemba 11, 2024 Naibu Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kilimanjaro, Sabas Salehe, amesema jenereta hizo zilikuwa na matatizo, ikiwemo injini zenye kutu na sehemu nyingine kupakwa rangi tu, ili kuficha hali yake.
“Tulipofanya ufuatiliaji, tulibaini kuwa Kadco ilikuwa inakusudia kununua jenereta mbili kutoka Kampuni ya African Power Machinery (APM) kwa gharama ya Sh328.4 milioni,” amesema Salehe.
Amefafanua kuwa jenereta hizo zilizowasilishwa zilikuwa na kasoro kama vile nyaya tofauti na injini zilizochakaa.
“Kuna maeneo kwenye jenereta yalikuwa yamepata kutu na mengine yalikuwa yamepakwa rangi,” ameongeza Salehe.
Pia, amesema Takukuru Wilaya ya Hai iliingilia kati ili kuzuia malipo hayo kufanyika kwa kampuni hiyo na kuokoa fedha hizo.
Katika hatua nyingine, Salehe amewasihi wananchi wa Mkoa wa Kilimanjaro kutoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa, ili hatua za kisheria zichukuliwe.
Amesema Takukuru imeweka mikakati ya kudhibiti vitendo vya rushwa kuelekea uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusu makosa ya rushwa kwa jamii na kukusanya taarifa za wanasiasa na wananchi wanaojihusisha na rushwa.
“Tunaendelea kukusanya taarifa za wanasiasa na wananchi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa kwenye uchaguzi, na tunatoa wito kwa wananchi kuwafichua wanaojihusisha na vitendo hivyo,” amesema Salehe.
Aidha, amesema Takukuru imefanya ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za umma kwenye miradi 38 ya maendeleo katika wilaya zote saba za mkoa huo yenye thamani ya zaidi ya Sh20.4 bilioni katika sekta za afya, maji, elimu, na ujenzi wa barabara.
Ameongeza kuwa kati ya miradi hiyo, miradi tisa yenye thamani ya Sh10.2 bilioni ilibainika kuwa na upungufu na Takukuru imeshauri nini kifanyike.
“Pia kwenye miradi miwili yenye thamani ya Sh6.081 bilioni tulitoa ushauri wa kipi kitekelezwe na tayari wahusika wamefanyia kazi ushauri huo na sasa inaendelea kutekelezwa, lakini kuna mradi mmoja tunaendelea kuuchunguza,” amesema kiongozi huyo.