Takukuru yabaini kasoro mifumo ya sekta ya afya

Geita/Songwe. Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Geita imebaini kasoro katika uchambuzi wa mifumo ya sekta ya afya, huku baadhi ya watumishi wakihusishwa na masuala ya rushwa.

Miongoni mwa kasoro hizo ni maabara za binadamu kutoa huduma bila kusajiliwa, wajawazito kutakiwa kubeba glavu na mipira ya kitandani.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Geita, Azza Mtaita amesema hayo leo Novemba 12, 2024 alipotoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha miezi mitatu iliyopita.

Amesema katika Halmashauri ya Mji wa Geita wamebaini baadhi ya mabaara zina wataalamu ambao hawajasajiliwa.

Amesema zipo maabara zinazotoa huduma ambazo haziruhusiwi ikiwamo kuchoma sindano na kufanya vipimo vya Utra Sound kinyume cha taratibu na kuwa na vifaa vilivyozuiwa kutumika kwenye maabara.

Pia, amedai baadhi hazilipi mapato kwa halmashauri hivyo kuwa na deni la Sh11 milioni.

Kutokana na hayo, Takukuru imemuagiza mratibu wa maabara wa halmashauri hiyo kuzifunga maabara zote zisizosajiliwa na kuchukua hatua kwa wataalamu wake ambao hawajasajiliwa na wanaotumia vifaa visivyoruhusiwa.

Katika Hospitali ya Wilaya ya Chato, baadhi ya watumishi wamebainika huwapokea wagonjwa na kuwahudumia kinyume cha miongozo ya afya.

“Tumebaini wapo watumishi wanaomba na kupokea fedha kinyume cha utaratibu, huku wajawazito wakitakiwa kuja na glavu na mipira inayotumika wakati wa kujifungua jambo ambalo siyo sahihi. Tumebaini pia, dawa zinazobaki au pale mgonjwa anapobadilishiwa dawa hubaki wodini,” amesema.

Wilayani Nyang’hwale, Takukuru imebaini uwepo wa mianya ya rushwa kwa baadhi ya wagonjwa kutolipia gharama za matibabu dirishani hasa nyakati za usiku, mwishoni mwa wiki na siku za sikukuu.

Imebainika kuwa, taarifa za ununuzi wa dawa na vifaatiba katika vituo vya kutolea huduma za afya hazifiki kwenye kamati za usimamizi kinyume cha mwongozo unaoelekeza taarifa za ununuzi zitatengenezwa kuainisha ununuzi uliofanyika na taarifa zisomwe kwenye kamati za usimamizi ya kituo kwa lengo la kuweka uwazi na uelewa kwa pamoja wa matumizi ya fedha za Serikali.

Takukuru imebaini ukusanyaji wa mapato ya NHIF na CHF umekuwa na changamoto hasa katika kupata malipo vituo vinapoomba kulipwa fedha zinazodai na taarifa hizo kutowasilishwa kwenye kamati ya usimamizi wa vituo kwa wakati.

Mratibu wa maabara katika halmashauri hiyo, Piensia Kajwahula amesema tayari wameanza kufanyia kazi maelekezo waliyopewa na Takukuru.

Amesema wamechukua vifaa vilivyobainika kutumika kwenye maabara kinyume cha utaratibu.

Amesema baadhi ya maabara zimetozwa faini kwa kufanya kazi bila leseni, akisema nane zimelipa na kupatiwa leseni, nyingine zikiendelea na taratibu ili zipatiwe.

Kajwahula amesema idara yake itaendelea kufanya ukaguzi wa kushtukiza ili kuwabaini wanaofanya kazi kinyume cha utaratibu.

Kuhusu ufuatiliaji wa utekelezaji wa miradi ya maendeleo, Takukuru imesema miradi 26 yenye thamani ya zaidi ya Sh9.6 bilioni imefuatiliwa na kati ya hiyo 13 imebainika kuwa na upungufu.

Imesema imebaini miradi mitatu yenye tamani ya Sh2.9 bilioni ina upungufu kwenye matumizi ya fedha na tayari wameanza uchunguzi.

Akizungumzia utekelezaji wa programu ya Takukuru Rafiki, amesema imesaidia wananchi wa Kata ya Mwingiro wilayani Nyang’hwale, ambako wananchi 226 wamelipwa fidia ya Sh7.2 bilioni na mgodi wa Barrick Bulyanhulu waliokuwa wakidai maeneo yao kuchukuliwa na mgodi kwa zaidi ya miaka 20 iliyopita kwa ajili ya utafiti wa madini bila kuwalipa fidia.

Wakati huohuo, Takukuru Mkoa wa Songwe imewaonya wagombea wa uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024 kuhusu vitendo vya rushwa.

Kamanda wa Takukuru mkoani humo, Frida Wikesi ametoa onyo hilo alipozungumza na waandishi wa habari kutoa taarifa ya kipindi cha kuanzia Julai hadi Septemba 2024.

Wikesi amesema kupitia Takukuru Rafiki baadhi ya wananchi wamesema wanapewa pombe ili wawachague wagombea kwa nafasi wanazogombea kitendo ambacho kinahatarisha kupatikana viongozi wasio na vigezo.

Wikesi amesema rushwa katika uchaguzi husababisha kuchaguliwa viongozi wasio wadilifu ambao muda mwingi huutumia kwa shughuli binafsi badala ya kuleta maendeleo kwa wananchi.

“Kueleke uchaguzi huu baadhi ya maeneo mkoani Songwe tumeambiwa wagombea wanatoa rushwa ya pombe kushawishi wananchi wawachague, tunakemea vikali na watakaokutwa watachukuliwa hatua,” amesema.

Amesema madhara ya rushwa kipindi cha uchaguzi ni chanzo cha kupatikana viongozi wasio na maadili, wasiozingatia misingi ya haki, usawa, uwazi, uwajibikaji na uzalendo.

“Takukuru imejipanga kuhakikisha inakabiliana na kudhibiti viashiria vya rushwa kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Novemba 27, 2024, huku wananchi wakitakiwa kushirikiana na Takukuru kutoa taarifa za viashiria vya rushwa,” amesema.

Amesema wamejipanga kutoa elimu ya rushwa kwa wananchi kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa ili wafahamu madhara ya kuchagua viongozi kwa njia ya rushwa.

Magidalena Mwazemba, mkazi wa Vwawa amesema tabia ya kupewa pombe na wagombea imekuwa endelevu kipindi cha uchaguzi, wakilenga kuwashawishi wananchi wawachague kumbe ni kosa kisheria.