
Dar es salaam. Karibu watu 9,000 wamepoteza maisha duniani kote katika njia za uhamiaji mwaka 2024.
Vifo hivyo vinatajwa kuufanya mwaka 2024 kuwa mbaya zaidi kwa wahamiaji, Umoja wa Mataifa umesema mwishoni mwa juma huku ukiita ‘janga lisilokubalika na linalozuilika’.
“Angalau watu 8,938 walifariki katika njia za uhamiaji duniani kote mwaka 2024. “Huu ni mwaka wa tano ambapo idadi imefikia kiwango cha juu zaidi,” Shirika la Uhamiaji la Umoja wa Mataifa (IOM) lilieleza.
Naibu Mkurugenzi wa IOM, Ugochi Daniels amesema “Janga la kuongezeka kwa idadi ya vifo vya wahamiaji duniani kote halikubaliki na linazuilika,”
Daniels amesema wanaopotea ni binadamu na kupotea kwao ni janga. “Idadi halisi ya vifo na kutoweka kwa wahamiaji kuna uwezekano mkubwa wengi hawajaandikwa kwa sababu ya uhaba wa vyanzo rasmi,”
Asia, Afrika na Ulaya zilikuwa na idadi kubwa zaidi ya watu wanaokufa ambapo kwa mwaka 2024 pekee walifariki wahamiaji 5253 mtawalia.
Jumla ya watu 2,452 walirekodiwa wakifa katika Bahari ya Mediterania, lango kuu kwa wale wanaojaribu kufika Ulaya.
Data za mwisho hazijapatikana kwa Marekani, lakini takwimu hadi sasa zinaonyesha watu 1,233 walifariki.
Hii ilijumuisha vifo 174 vya wahamiaji wanaovuka msitu wa Darien kati ya Colombia na Panama.
Msitu wa Darien ulikuwa kati ya njia kuu ya uhamiaji kwa watu wanaojaribu kufika Marekani.
Lakini kutokana na idadi hiyo kubwa inaonyesha haja ya mifumo ya kutosha ya utafutaji na uokoaji pamoja na njia salama na za kawaida za uhamiaji.
“Hizi njia wanazotumia kwa sasa ni hatari.”
Ulimwenguni kote, vifo kutokana na vurugu viliendelea kuenea kwa watu wanaohama. Mwaka 2022, asilimia 10 ya vifo vyote vya wahamiaji vilivyoorodheshwa vilitokana na vurugu.
Mwaka 2024, hii ilitokana kwa kiasi kikubwa na vurugu dhidi ya wale walio safarini huko Asia, na karibu watu 600 kupotea katika njia za uhamiaji kote Asia Kusini na Kusini-mashariki.
“Ongezeko la vifo ni hatua mbaya, lakini ukweli kwamba maelfu bado hawajatambuliwa kila mwaka ni janga zaidi,” amesema Julia Black, mratibu wa mradi wa wahamiaji waliopotea unaosimamiwa na IOM.