Takriban watu 51 wameuawa na wanamgambo wa CODECO kaskazini-mashariki mwa DRC

Takriban watu 51 wameuawa na watu wenye silaha wenye uhusiano na wanamgambo wa CODECO kaskazini-mashariki mwa DRC, eneo ambalo vurugu za kijamii hutokea mara kwa mara, shirika la habari la AFP limenukuu siku ya Jumanne vyanzo vya ndani na vya kibinadamu.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumatatu, wanamgambo wa CODECO (Ushirika wa Maendeleo ya Kongo) “waliwaua watu 51”, wengi wao wakiwa raia waliokimbia makazi yao, katika miji mitatu jirani katika jimbo la Iuri, kiongozi wa mashirika ya kiraia katika eneo la Djugu ambalo linajumuisha miji hii, Jules Tsuba, ameliambia shirika la habari la AFP.

“Hii bado ni ripoti ya muda kwa sababu utafutaji wa watu walionusurika unaendelea, kuna nyumba 43 zimechomwa, na waathiriwa wengine walichomewa kwenye nyumba zao. Kuna majeruhi wapatao kumi,” almeema Bw. Tsuba.

Idadi ya vifo na mazingira ya mashambulizi haya, ambayo yalifanyika takriban kilomita 80 kaskazini mashariki mwa Bunia, mji mkuu wa mkoa, yalithibitishwa kwa shirika la habari la AFP na vyanzo kadhaa vya kibinadamu.

Wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC (MONUSCO) walijaribu kuingilia kati ili kuzuia mauaji haya, kulingana na vyanzo hivyo. hata hivyo MONUSCO haikujibu mara moja ombi la AFP.

“Vikosi vya kijeshi vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, pamoja na washirika wao, viliingilia kati, na kitendo hiki kilipunguza uharibifu,” amesema msemaji wa jeshi la Kongo katika mkoa huo, katika ujumbe uliotolewa kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne.

Wanamgambo wa CODECO wanadai kutetea masilahi ya jamii ya Lendu, hasa inayojumuisha wakulima, dhidi ya jamii ya Hema, hasa wafugaji.

Mauaji ya Jumatatu yaliripotiwa kujibu shambulio la wanamgambo wa Zaire, ambao wanadai kutetea jamii ya Hema, katika mji unaopatikana katika eneo hilo siku yaJumamosi, kulingana na vyanzo vya kibinadamu.

Mkoa wa Ituri unakumbwa tangu mwaka 2017 na mzozo kati ya wanamgambo wa kijamii, ikiwa ni pamoja na CODECO na kundi la Zaire, ambao umesababisha vifo vya maelfu ya raia na watu wengi kuyahama makazi yao.

Mgogoro wa hapo awali kati ya wanamgambo wa kijamii huko Ituri ulisababisha vifo vya maelfu ya watu kati ya 1999 na 2003, hadi kuingilia kati kwa kikosi cha Ulaya, Operesheni Artemis, chini ya amri ya Ufaransa.

Ituri iko kaskazini mwa mikoa miwili ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini, ambako kundi linaloipinga serikali la M23 na washirika wake katika vikosi vya Rwanda, ambao wameteka maeneo makubwa ya eneo hilo kutoka mikononi mwa jeshi la Kongo katika miaka ya hivi karibuni, wameongeza kasi ya harakati zao katika wiki za hivi karibuni na kuendelea kusonga mbele katika mkoa wa Kivu kusini.