
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limewaua au kuwakamata magaidi 69 wanaohusishwa na shirika la ujasusi la Israel, Mossad, wakati wa mazoezi makubwa ya kukabiliana na ugaidi kusini mashariki mwa nchi.
Msemaji wa mazoezi hayo yaliyopewa jina la “Mashahidi wa Usalama”, Jenerali Ahmad Shafaei, amesema leo Ijumaa kwamba jumla ya magaidi 23 wameuawa na wengine 46 wametiwa mbaroni katika operesheni mbalimbali tangu Jeshi la Nchi Kavu la IRGC lilipoanzisha zoezi hilo katika mkoa wa Sistan na Baluchestan.
Magaidi saba pia wamejisalimisha katika kipindi hicho.
“Ukweli usiopingika kuhusu magaidi ni kwamba wanategemea nguvu za madola ya kibeberu, hasa huduma za kijasusi za utawala mbovu na habithi wa Israel,” amesema Jenerali Shafaei.
Ameongeza kuwa: “Kwa bahati mbaya, silaha na zana za magaidi ni miongoni mwa silaha za kisasa zaidi duniani. Huu ni ushahidi wa utegemezi wao mkubwa.”
Afisa huyo ameeleza kuwa wanachama kadhaa wa timu hizo za kigaidi zilizovunjiliwa mbali hawakuwa raia wa Iran na walikuwa wameajiriwa na mashirika ya kijasusi ya kigeni kutekeleza hujuma na ugaidi ndani ya Iran.
Tarehe 26 Oktoba askari kumi wa Iran waliuawa katika shambulio la kigaidi katika wilaya ya Gohar Kuh wilaya ya Taftan katika mkoa wa Sistan na Baluchestan.