Dar es Salaam. Je, umewahi kuona vituo maalumu vya kukusanya taka za kielektroniki mtaani kwako?
Licha ya Sheria ya Kanuni ya Usimamizi wa Mazingira (Udhibiti na Usimamizi wa Taka za Vifaa vya Umeme na Elektroniki) ya 2021 kifungu cha 12 (2) kuzitaka mamlaka za Serikali za mitaa kuhakikisha taka za vifaa vya kielektroniki zinadhibitiwa ipasavyo, hali ni tofauti.
Kanuni zinataka taka hizi kutenganishwa na aina nyingine za uchafu na zinakusanywa kwenye vituo vilivyoidhinishwa, pia mamlaka itazingatia kuratibu mafunzo juu ya udhibiti wake.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa miezi mitatu katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam umebaini taka hizi kwa kiwango kikubwa hazitenganishwi na nyingine kwa mujibu wa sheria, si wananchi wala wazalishaji wenye uelewa wafanye nini na taka hizi.
Tatizo la mwanzo ni utenganishaji wa taka, kwani siyo tu kanuni bali hata Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, kifungu 114 (a) kinazitaka mamlaka ya Serikali za Mitaa kuhakikisha aina tofauti za taka, mabaki au uchafu, zichambuliwe na kutenganishwa kwenye chanzo chake, lakini jambo hili halifanyiki.
Kwa mujibu wa sheria na kanuni, mamlaka zinapaswa kutoa elimu kwa jamii kuhusu udhibiti wa taka hizo. Hali ya mtaani haiakisi haya.
Uelewa wa wananchi
Kwenye ukusanyaji taarifa kwa wananchi swali la msingi lilikuwa unafanyaje na kifaa chako cha kielektroniki kinapoisha muda wake wa matumizi au kuwa kibovu na hakifai tena kutumika? Hapa vilikusudiwa vifaa kama pasi, simu, televisheni na vifaa vingine.

Jesika Jackson, mkazi wa Mtaa wa Maruzuku Buguruni anasema: “Natupa kwenye taka nyingine. Gari la manispaa hukusanya.”
“Napeleka kwa fundi ikishindikana naacha huko. Vingine natupa jalalani,” anasema Gideon Mafumbo, mkazi wa Mbezi Luis.
Mkazi wa Yombo Dovya Shuleni, Abdulkarim Mketo anasema vifaa vya umeme vinavyoisha matumizi huwa anakwenda kuwauzia mafundi kwa kukubaliana fedha kidogo kwa kuamini kuna vipuri wanaweza wakavihitaji kwa matumizi.
“Kifaa changu kinachotumia umeme muda wake wa matumizi ukiisha kama TV au redio huwa nawauzia mafundi, unakuta labda kimeungua kifaa na fedha ya kununulia sina huwa nampelekea fundi ananipoza kidogo,” anasema na kuongeza kwamba, kuna wakati anaweza kupeleka kifaa chake kwa fundi kutengeneza lakini fundi akataja kitu kilichoharibika hana fedha ya kwenda kununua huwa wanaingia makubaliano.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mkazi wa Mbande Kisewe, Idrisa Nasri akisema akinunua redio au TV matumizi yake yakiisha huwa anakwenda kuiuza kama kifaa chakavu au kutupa.
“Kuna vifaa kama havihitajiki nakwenda kutupa dampo lakini kuna vingine kama chuma naenda kuwauzia wanaonunua ambao wanapita mitaani na matangazo wananunua vifaa chakavu,” anasema.
Kauli ya mafundi
Kwenye maeneo mbalimbali mjini ni kawaida kukuta mafundi wa vifaa vya kielektroniki wakiwa na marundo ya vifaa hivyo.
Fundi redio wa Tandika, Jumanne Omary anasema vifaa visivyotumika kama saketi na mifuniko hukusanywa na kutupwa dampo kwa kushirikiana na magari ya taka.
Anasema changamoto ni wateja kuleta vifaa bila maandalizi na kuviacha kwa muda mrefu bila kufuatilia, hali inayosababisha ofisi zao kuonekana zimejaa.
Anasema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huwakadiria mapato makubwa kwa kuzingatia idadi ya vifaa vilivyopo, licha ya kwamba vingine ni mali ya wateja waliovitelekeza.
“Wateja wengine hukaa miaka bila kufuatilia vifaa vyao hali inayotufanya kuonekana tumejaza mizigo,” anasema.
Fundi wa kompyuta katika Soko la Machinga Complex, Mahudu Edmund anasema vifaa vilivyoharibika wanavitumia kama vipuri vya kutengenezea kompyuta zingine au kuboresha iliyoharibika.
“Vifaa ambavyo vinakuwa vimepoteza mvuto au matumizi kwa maana kuwa havifai kuna watu wanaovinunua kama saketi na kuzichakata,” anasema.
Anaeleza vifaa vya kieletroniki vimetengenezwa kwa kutumia madini mbalimbali akitaja mfano wa saketi, ambayo ndani yake kuna chuma, dhahabu na zinki.
“Wanaonunua wanakwenda kuzisaga kwa kuzitenganisha madini yanakwenda kwake na aina nyingine kwake kwa ajili ya matumizi mengine tofauti,” anasema.

Anasema kompyuta zimetengenezwa kwa madini ya nikeli na kobati ambayo yakisagwa yanatengeneza vifaa vya majumbani kama redio, TV na vikombe.
“Kuna watu wanakuja kukusanya, mafundi tunakwenda kuwauzia wao kwa bei za kawaida kuanzia Sh3,000,” anasema.
Kwa upande wake, Aman Nyela, fundi mashine za kudurufu karatasi eneo la Mchinga Complex, anasema mashine zikichoka kuna vifaa huwa wanawauzia watu chuma na plastiki.
“Vitu vingi kwenye mashine huwa tunauza kwa bei ya chini ili kupunguza mzigo ofisini, vifaa vya plastiki watu wananunua na kwenda navyo Zambia sijajua wanaenda kufanyia nini.
“Saketi tunawauzia raia wa China kwa sababu hatuna teknolojia ya kuzirekebisha. Zikiharibika zinarundikwa ikifikia kiasi fulani Wachina wanapelekewa,” anasema.
Nyela anasema katika mashine hakuna kitu kinachopotea, akieleza kuna wateja wanatekeleza vifaa vyao baada ya kubaini wanatakiwa kutoa kiasi kikubwa cha kununua vipuri.
“Wanaotekeleza ni wale wanaoleta wakiamini mashine itapona kwa asilimia 100 kwa mwonekano wa nje lakini unakuta ndani panya, mende waliingia na kufanya uharibifu,” anasema.
Anasema wanapotajiwa gharama kwa ajili ya kununua vipuri wakibaini inahitajika fedha kubwa huvitelekeza na wengine huwataka waitumie kama skrepa (bidhaa kuukuu).
Fundi simu katika eneo hilo, Joseph Jackson anasema asilimia kubwa ya vifaa vya simu vinavyoharibika ni vioo ambavyo wakivitoa huviweka kwenye vyombo vya kukusanyia taka.
“Tunatupa kwenye uchafu kwa kuwa hakina matumizi tena, wakipita wanaokusanya uchafu hubeba. Baadhi huwa wanapita kununua vifaa,” anasema.

Anasema Tanzania hakuna sehemu ya kutupa taka za kieletroniki kama ilivyo kwa mataifa yaliyoendelea au kama inavyofanyika kwa chuma chakavu.
“Kuna vifaa kama hizi saketi tunawauzia Wachina lakini zinazobaki tunazitupa kwenye vyombo vya taka na wabeba taka wanakuja kuchukua,” anasema.
Hali halisi mtaani
Licha ya yaliyoelezwa, uchunguzi wa Mwananchi umebaini vifaa vingi vinatelekezwa au kutupwa kwenye magari ya taka.
Mathalani eneo la Machinga Complex wilayani Ilala, ukiingia kwenye vyumba ambavyo mafundi wanatengeneza bidhaa hizo kuna mabaki mengi yamehifadhiwa na upande wa nje yamerundikwa kama uchafu.
Hali halisi ni kuwa, iwapo kuna vifaa vinavyouzwa ni kiwango kidogo, vingi vikibaki kama uchafu na hawajui sehemu ya kwenda kutupa.
Ofisi za mafundi ambazo zipo katika ghorofa zinazopakana na ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) upande wenye viwanja vya mazoezi, kuna marundo ya taka hizo.
Itaendelea kesho