Taifa Stars yaweka rekodi sita Afcon 2025

Dar es Salaam. Rekodi tano zinaisubiria timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwenye fainali za mataifa ya Afrika (Afcon) 2025  baada ya ushindi wa bao 1-0 nyumbani juzi dhidi ya Guinea ulioihakikishia tiketi ya kushiriki fainali hizo.

Bao pekee la Saimon Msuva, liliifanya Taifa Stars kumaliza hatua ya makundi ya mashindano ya kuwania kufuzu fainali hizo ikiwa na pointi 10 nyuma ya vinara DR Congo iliyomaliza ikiwa na pointi 12 na kuzifanya timu hizo mbili kukata tiketi ya kwenda Morocco ambako fainali hizo zitafanyika kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 16, 2026.

Kuna rekodi tano ambazo zinaweza kuwekwa, kufikiwa au kuvunjwa na Taifa Stars yenyewe au wachezaji wake katika fainali hizo za Afcon 2025 ambazo zitakuwa za nne kwa Tanzania kushiriki baada ya kufanya hivyo katika fainali za 1980, 2019 na 2023.

Ikiwa Taifa Stars itafanikiwa kuingia hatua ya 16, itaweka kwa mara ya kwanza rekodi ya kuvuka hatua zaidi ya makundi kwenye fainali hizo kwani kabla ya hapo, awamu tatu za nyuma iliposhiriki, haikuwahi kufanya hivyo, mara zote ikimaliza ikiwa mkiani kwenye kundi.

Rekodi nyingine ambayo Stars ina kibarua cha kuifikia au kuivunja ni ya kwake yenyewe ambayo ni ya kukusanya idadi kubwa ya pointi katika hatua ya makundi ya fainali hizo zaidi ya mbili ilizopata katika fainali za 2023 zilizofanyika mwaka huu huko Ivory Coast ambazo ni nyingi zaidi ilizowahi kupata katika awamu moja ya fainali hizo.

Mwaka 1980, Taifa Stars ilimaliza ikiwa na pointi moja, mwaka 2019 haikupata kitu na fainali za 2023 ikapata pointi mbili.

Kama atapata fursa ya kushiriki fainali zijazo za Afcon, Saimon Msuva atakuwa na kibarua cha kuboresha rekodi yake ya kuwa mchezaji wa Taifa Stars aliyefunga bao katika fainali nyingi tofauti za Afcon ambapo zitakuwa ni fainali zake za tatu kufunga bao baada ya kufanya hivyo katika fainali za 2019 na 2023.

Lakini pia kama atafunga, Msuva ataweka rekodi nyingine ambayo itakuwa ni ya nne kuihusu Taifa Stars kwenye Afcon ambayo ni ya kuwa mchezaji aliyeifungia idadi kubwa zaidi ya mabao kwenye fainali hizo.

Kwa sasa, Msuva analingana na nyota wa zamani wa Taifa Stars, Thuweni Ally, kila mmoja akifunga mabao mawili.

Rekodi ya tano ni ya mchezaji aliyecheza idadi kubwa ya dakika katika kikosi cha Taifa Stars kwenye fainali za Afcon ambayo hadi sasa inashikiliwa na kipa Aishi Manula ambaye kama ataitwa atakuwa na kibarua cha kulishawishi benchi la ufundi kumpa nafasi ya kucheza ataiendeleza zaidi kwa viloe hadi sasa ameshacheza kwa dakika 450 katika mecho tano za mashindano hayo.

Rekodi ya saba inawindwa na nyota saba ambayo ni ya kuwa wachezaji wa Taifa Stars walioichezea timu hiyo katika awamu tatu tofauti za Afcon ambao ni Aishi Manula, Feisal Salum, Himid Mao, Mbwana Samatta, Saimon Msuva, Mohammed Hussein na Mudathir Yahya.

Stars mdomoni mwa vigogo

Uwepo wa idadi kubwa ya timu ambazo ziko nafasi za juu kwenye chati ya ubora wa soka wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) utaifanya Taifa Stars kuangukia chungu cha nne katika droo ya upangaji makundi ya fainali hizo.

Kupangwa katika chungu cha nne kutaifanya Taifa Stars kukutana na timu tatu ngumu katika kundi lake mojawapo ikiwa ni lazima iwe iliyowahi kutwaa ubingwa wa fainali hizo.

Chungu cha kwanza kitakuwa na timu za Morocco, Senegal, Nigeria, Misri, Ivory Coast na Tunisia na chungu cha pili kitakuwa na timu za Algeria, Mali, Cameroon, Afrika Kusini, Burkina Faso na DR Congo.

Timu zitakazokuwa katika chungu cha tatu ni Guinea ya Ikweta, Gabon, Zambia, Uganda, Angola na Benin na chungu cha nne ambacho kitakuwa na Tanzania, timu zingine zitakazokuwepo ni Comoro, Zimbabwe, Sudan, Botswana na Msumbiji.

Mwaka wa kihistoria

Kufuzu kwa Taifa Stars Afcon kunaufanya mwaka 2024 kuwa wa kihistoria kwa timu za taifa za Tanzania kuanzia za wakubwa hadi za wadogo.

Ni mwaka ambao pia timu ya taifa ya wanawake ‘Twiga Stars’ imefuzu fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake huku pia timu ya taifa ya vijana kwa umri chini ya miaka 20 ikifuzu fainali za Afrika kwa vijana wa umri huo.

Pia timu ya taifa ya soka la ufukweni ya Tanzania ilifuzu na kushiriki fainali za Afrika ambazo zilifanyika mwaka huu huko Misri.

Noti juu ya noti

Kwa kujihakikishia kufuzu Afcon 2025, Taifa Stars imepata bonasi ya Shilingi 700 milioni kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Ushiriki tu kwenye Afcon 2025 utaifanya Taifa Stars ioge noti hata kama itaishia hatua ya makundi ya fainali hizo.

Ifahamike timu inayoishia hatua ya makundi ikishika mkia, inapata kiasi cha Dola 400,000 (Sh 1.1 bilioni) huku timu bingwa ikipata kitita cha Dola 7 milioni (Sh 19 bilioni).

Wachezaji kicheko

Nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alisema kuwa mafanikio ya Taifa Stars kufuzu Afcon ni matokeo ya juhudi za nchi nzima.

“Nina furaha sana na tiketi hii ya Afcon inawahusu Watanzania wote. Unapokuwa na mashabiki wakati wote unahisi una watu nyuma na unapata nguvu. Haikuwa rahisi lakini tumepambana hadi dakika ya mwisho,” alisema Samatta.

Mshambuliaji Saimon Musva alisema kuwa wamejipanga kuhakikisha hawaishii katika hatua ya makundi kama ilivyowahi kutokea hapo nyuma.

“Tulisema hii mechi ni fainali na hakuna utetezi wowote wa kuwapa mashabiki kama hatutofuzu. Ni furaha kwa nchi, wachezaji na Watanzania wote. Tumefuzu Afcon ila safari hii hatutaki kuishia tena kwenye makundi,” alisema Msuva.

Timu 24 zilizofuzu Afcon 2025

Morocco (Mwenyeji)

Burkina Faso

Equatorial Guinea

Ivory Coast

Afrika Kusini