Taifa Stars na mtihani wa vigogo Afcon 2025

Droo ya makundi ya Fainali za Mataifa ya Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2025 itafanyika leo huko Rabat, Morocco kuanzia saa 3:00 kwa muda wa Afrika Mashariki.

Timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ni miongoni mwa timu 24 zinazosubiria kwa hamu droo hiyo ili kufahamu kundi itakalokuwepo na wapinzani ambao itapangwa nayo katika fainali hizo zitakazofanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026.

Katika droo ya leo, Taifav Stars itawekwa katika chungu cha nne ambacho pia kitakuwa na timu za Comoro, Msumbiji, Botswana, Sudan na Zimbabwe

Kutakuwa na vyungu vinne vyenye timu sita kila kimoja ambapo kila chungu kitatoa timu moja ya kuunda kundi na kwa mujibu wa utaratibu wa uchezeshaji wa droo, timu za chungu kimoja haziwezi kupangwa katika kundi moja.

Upangaji wa timu katika vyungu hivyo umezingatia nafasi ya kila nchi kwenye viwango vya ubora vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (Fifa) ambapo timu zilizo juu zimewekwa katika vyungu vya mwanzo na zilizo chini zimewekwa katika vyungu vya mwisho.

Kwa maana hiyo, Taifa Stars katika kundi lolote ambalo itapangwa, itakutana na timu ambazo zimekuwa zikifanya vizuri katika mashindano mbalimbali barani Afrika kwa vile yenyewe imepangwa katika chungu cha mwisho ambacho ni cha nne.

Taifa Stars itapangwa katika kundi ambalo litakuwa na timu moja kutoka chungu cha kwanza, moja kutoka chungu cha pili na nyingine moja kutoka chungu cha tatu.

Chungu cha kwanza kitakuwa na timu za Morocco, Senegal, Misri, Algeria, Nigeria na Ivory Coast huku chungu cha pili kikiwa na timu za Cameroon, Mali, Tunisia, DR Congo, Afrika Kusini na Burkina Faso.

Timu zilizopo katika chungu cha tatu ni Guinea Ikweta, Angola, Gabon, Uganda, Zambia na Benin.

Taifa Stars iliposhiriki fainali za Afcon kwa mara ya kwanza mwaka 1980, ilipangwa katika kundi A ambalo lilikuwa na timu za Nigeria, Misri na Ivory Coast na iliposhiriki mara ya pili mwaka 2019 ilipanmgwa katika kundi C ambalo liliundwa na timu za Algeria, Senegal na Kenya.

Katika fainali zilizopita za 2023, Taifa Stars ilipangwa kundi F na timu za DR Congo, Zambia na Morocco.