Hisia za wadau wote wa mpira wa miguu Afrika leo zitaelekezwa jijini Rabat, Morocco ambako droo ya fainali za 35 za mataifa ya Afrika (AFCON) itafanyika ikihusisha timu 24 za mataifa yaliyofuzu.
Fainali hizo zitafanyika Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 hadi Januari 18, 2026, ambapo timu itakayotwaa ubingwa itafanikiwa kuondoka na kitita cha Doła 7 milioni (Sh17.8 bilioni).
Hafla ya uchezeshaji wa droo hiyo itafanyika katika kituo cha kimataifa cha Utamaduni cha Mfalme Mohammed V kilichopo Rabat, kuanzia saa 3:00 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.
Rabat ndio mji mkuu wa Morocco na unapakana na bahari ya Mediterranea kwa upande wa Kaskazini ukiwa na idadi ya watu inayokadiriwa kufikia milioni 1.8.
Ukumbi umechangamka
Kituo cha kimataifa cha utamaduni cha Mfalme Mohammed V kilianza kujengwa Oktoba 7, 2014 na mradi wa ujenzi wake ulikamilika rasmi 2021.
Hata hivyo, uzinduzi rasmi wa kituo hicho ulifanyika miaka mitatu baadaye kwa maana ya 2024 na tangu hapo hadi sasa umekuwa ukitumika kwa mikusanyiko mbalimbali mikubwa na ya kimataifa.
Kuna ukumbi wa ndani ambao una siti za kukaa 1,800 lakini kuna ukumbi wa wazi ambao unaweza kuhudumia watu 7,000 walioketi vitini.
Ujenzi wa kituo hicho ni utekelezaji wa wazo la Mfalme Mohammed VI wa Morocco ambaye aliagiza kujengwa kwa eneo ambalo litaonyesha utamaduni wa nchi hiyo lakini pia kutumika kwa matukio ya kisanaa.
Msanifu wa mchoro wa kituo hicho ni Zaha Hadid, Muiraq mwenye asili ya Uingereza ambaye alifariki dunia 2016.
Droo ya kibabe
Uzoefu wa timu zote 24 ambazo zitashiriki Afcon 2025 unafanya droo ya fainali hizo leo kusubiriwa kwa hamu na mamilioni ya wapenzi wa soka barani Afrika.
Katika hali ya upekee hakuna timu hata moja kati ya 24 zilizofuzu fainali hizo ambayo haijawahi kushiriki Afcon kwani zote zimewahi kucheza Afcon kwa nyakati tofauti.

Kutakuwa na vyungu vinne ambavyo vitatumika katika zoezi la upangaji wa makundi sita ya fainali hizo mwakani ambapo kila chungu kitakuwa na timu nane ambazo zimepangwa kwa kuangalia nafasi ambayo kila moja imekuwa nayo katika chati ya viwango vya ubora wa soka vya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).
Chungu cha kwanza kitakuwa na timu za Morocco, Senegal, Misri, Algeria, Nigeria na Ivory Coast huku chungu cha pili kikiwa na timu za Cameroon, Mali, Tunisia, DR Congo, Afrika Kusini na Burkina Faso.
Timu zilizopo katika chungu cha tatu ni Guinea Ikweta, Angola, Gabon, Uganda, Zambia na Benin wakati katika chungu cha nne kutakuwa na timu za Tanzania, Msumbiji, Comoros, Botswana, Zimbabwe na Sudan.
Kwa mujibu wa taratibu za uchezeshaji droo hiyo, timu zilizopita katika chungu kimoja haziwezi kupangwa katika kundi moja.
CECAFA kinyonge
Kanda ya soka ya baraza la vyama vya mpira wa miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) ndio inawakilishwa na timu chache zaidi katika fainali za Afcon 2025, kulinganisha na kanda nyingine za soka Afrika.
Ni nchi tatu tu kutoka Cecafa ambazo leo zitajua makundi na washindani ambao zitapangiwa katika Afcon 2025 ambazo ni Tanzania, Uganda na Sudan.
Kanda ya Afrika Kaskazini itawakilishwa na timu nne ambazo ni Misri, Algeria, Morocco na Tunisia.
Kusini mwa Afrika watawakilishwa na timu saba ambazo ni Angola, Afrika Kusini, Comoros, Zambia, Msumbiji, Zimbabwe na Botswana.
Kanda ya kati itawakilishwa na timu nne ambazo ni Cameroon, Guinea Ikweta, Gabon na DR Congo na kanda ya Magharibi mwa Afrika itakuwa na timu sita ambazo ni Nigeria, Mali, Senegal, Burkina Faso, Benin na Ivory Coast.
Mastaa kujazana
Ni tukio ambalo litashirikisha kundi kubwa la wadau wa soka kama vile viongozi wa soka wa nchi wanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), makocha wa timu za taifa, waandishi wa habari za michezo pamoja na nyota wa zamani wa soka kutoka barani Afrika.
Baadhi ya nyota wa zamani ambao watakuwepo kwenye hafla hiyo ni Essam El Hadary, Patrick Mboma, Momo Sissoko, Chris Katongo, Aymen Mathlouthi na Gervinho.
Matumaini ya Tanzania
Baada ya kwenda AFCON mara tatu huko nyuma bila kuvuka hatua ya makundi, Taifa Stars leo inaomba Mungu ipangwe kwenye kundi mchekea tofauti ya huko nyuma, ikiwa na matumaini kuwa ikitokea hivyo kwa sasa inaweza kwenda hatua ya mtoano kutokana na kikosi chake ilichonacho kwa sasa.
“Tanzania sasa ni tofauti na huko nyuma, kikosi kimebadilika na kina wazoefu wengi, ukitazama mara zote ambazo tulikuwa tukishiriki michuano hii tulikuwa hatuna wachezaji wenye uzoefu wa kutosha kimataifa, lakini sasa utakubaliana nami kuwa hali hiyo haipo tena kila mmoja ana uzoefu kwa kuwa ameshashiriki michuano mbalimbali.
“Naamini sasa tunaweza kufanya vizuri zaidi kwa kundi lolote ambalo tunaweza kupangwa, wazo la kwanza iwe kuvuka kwenye makundi,” alisema kocha msaidizi wa Simba, Selemani Matola.
Timu mkao wa kula
Kipa na nahodha wa Afrika Kusini, Ronwen Williams alisema kuwa anaisubiria droo kwa hamu na timu yake iko tayari kupangwa na timu nyingine yoyote kwenye hayo mashindano.
“Tunaifurahia na tunaisubiria kwa hamu. Jambo la muhimu na kubwa sasa ni kwamba tupo miongoni mwa timu 10 bora na tumewekwa katika chungu cha pili na itaenda kuwa ngumu kwa kundi lolote ambalo tutapangwa kwa sababu haya ndio mashindano bora zaidi katika bara hili,” alisema Williams.