
Mfumo wa elimu nchini unalenga kuwawezesha wanafunzi kupata maarifa, ujuzi, na stadi za maisha ili kuwaandaa kwa maisha ya baadaye.
Hata hivyo, uwepo wa daraja sifuri katika matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne umekuwa kikwazo kwa wanafunzi wengi katika safari yao ya elimu na maisha kwa ujumla.
Serikali inapaswa kuangalia uwezekano wa kufuta daraja hilo kwa sababu kadhaa muhimu.
Mwanafunzi anapoanza safari ya elimu, kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha nne, ni dhahiri anapata maarifa na ujuzi mbalimbali.
Hata wale wanaopata alama za chini wanakuwa wamejifunza mambo fulani yanayoweza kuwa na manufaa katika maisha yao. Kutangaza mwanafunzi fulani amepata daraja sifuri ni sawa na kusema hajajifunza chochote, jambo ambalo si kweli.
Daraja sifuri linawaathiri wanafunzi kisaikolojia kwa sababu linawafanya wajione watu waliokosa uwezo wa kujifunza. Hii inaweza kusababisha baadhi yao kukata tamaa na kuacha kabisa kufikiria fursa za elimu au maendeleo ya maisha yao.
Endapo mfumo wa tathmini utarekebishwa ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayepata daraja sifuri, wengi wataendelea kujitahidi kuboresha matokeo yao kwa njia nyingine kama mafunzo ya ufundi, kozi fupi, au elimu ya watu wazima.
Kwa sasa, wanafunzi wanaopata daraja sifuri hukosa fursa ya kujiendeleza kielimu, kwani taasisi nyingi za elimu ya juu na vyuo vya ufundi zinakataa kuwachukua.
Hii inawazuia wale ambao wangependa kusoma zaidi, hata katika fani hazipimwi kwa msingi wa alama za mtihani wa taifa pekee. Iwapo Serikali itaondoa daraja sifuri, wanafunzi wataweza kuendelea na masomo yao kupitia mfumo mbadala kama vile elimu ya watu wazima, vyuo vya kati, au kozi za ufundi zinazohimiza ujuzi wa vitendo.
Siyo kila mwanafunzi ana uwezo sawa wa kuelewa masomo ya darasani kwa njia ya kawaida ya kufundishwa. Wengine wana vipaji katika sanaa, michezo, au ujuzi wa vitendo kama useremala, ushonaji, na uhandisi wa mitambo midogo.
Mfumo wa elimu unapaswa kuwa shirikishi kwa kutoa nafasi kwa kila mwanafunzi kulingana na uwezo wake, badala ya kuwahukumu kwa mfumo mmoja wa tathmini.
Elimu ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa lolote.
Taifa lenye watu wengi wasio na nafasi ya elimu kwa sababu ya matokeo duni ya mitihani linapunguza wigo wa maendeleo yake. Kwa kufuta daraja sifuri, Tanzania inaweza kusaidia kuwapa vijana wake nafasi ya pili ili wajifunze kwa njia mbadala na hatimaye kuchangia maendeleo ya jamii na uchumi wa nchi.
Nchi nyingi zimebadilisha mfumo wao wa tathmini ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayehisi kutengwa kwa sababu ya matokeo duni. Kwa mfano, baadhi ya nchi zinatumia mfumo wa alama unaolenga kupima uwezo wa mwanafunzi kwa mtazamo mpana zaidi.
Tanzania inaweza kujifunza kutoka kwa mifumo hii na kutengeneza mbinu mbadala za kupima uwezo wa wanafunzi.
Ni wazi kuwa familia nyingi huathirika pale mtoto wao anapopata daraja sifuri kwa sababu ya hisia kwamba ameshindwa kabisa katika maisha.
Tunashauri haya tukirejelea sera mpya ya elimu ambayo inatoa wigo mpana wa elimu msingi ikihesabika ni kuanzia darasa la kwanza hadi kitado cha nne, tukiendelea na daraja sifuri wataumia.