
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), imetangaza mchakato wa uboreshaji wa daftari la kudumu la wapiga kura kwa Mkoa wa Dar es Salaam, unaotarajiwa kuanza Machi 17 hadi 20.
Mkoa huo ndio wa mwisho kukamilisha uboreshaji wa taarifa za wapiga kura, ukihitimisha safari ya miezi kadhaa ya shughuli hiyo iliyokuwa ikiendeshwa katika mikoa mbalimbali nchini.
Ni uboreshaji kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Japo tunatambua kuwa mchakato wa uboreshaji umekuwa na dosari ikiwamo ya tume kutoendesha shughuli ya uboreshaji mara mbili kama inavyotakiwa kisheria, tunaamini katika maeneo yote ilipopita wananchi walijitokeza kwa wingi kutimiza wajibu wao wa kikatiba. Tunaamini kwa Mkoa wa Dar es Salaam mwitikio unaweza kuwa mkubwa zaidi.
Kupiga kura ni haki ya msingi kwa kila raia wa Tanzania, na ni jambo muhimu linaloweza kuleta mabadiliko makubwa katika maendeleo ya taifa letu.
Kila raia anaposhiriki kwenye uchaguzi, anakuwa sehemu ya mchakato wa kuamua viongozi watakaoongoza taifa kwa kipindi fulani. Kwa hiyo, kushiriki katika upigaji kura ni njia moja wapo ya kuonyesha dhamira ya kushiriki katika uongozi na utawala wa nchi.
Tunachopaswa kukumbuka Watanzani ni ukweli kuwa upigaji kura unaleta demokrasia imara kwa kuwa unahakikisha kwamba maoni ya wananchi yanahusishwa katika uteuzi wa viongozi.
Hii inatupa sisi wananchi uwezo wa kuamua mustakabali wa taifa letu, kwa kutaka kile kinachopaswa kuwa kipaumbele cha Serikali yetu. Tunaposhiriki, tunatoa mchango katika kuunda utawala bora, na hivyo kuboresha huduma za kijamii kama elimu, afya, miundombinu na nyinginezo.
Aidha, kushiriki kwenye uchaguzi ni hatua muhimu katika kujenga jamii inayoheshimu haki na majukumu. Kila raia anaposhiriki, anahakikisha kwamba haki ya kupiga kura inatumiwa ipasavyo, na kwamba kila sauti ina maana kwa mustakabali wa Taifa letu.
Tuhitimishe kuwa upigaji kura ni sehemu muhimu ya mchakato wa maendeleo. Kwa kuchagua viongozi bora, tunahakikisha kwamba taifa letu linaongozwa na watu wenye maono na dhamira ya kuleta mabadiliko chanya.
Watanzania wanaposhiriki kwa wingi katika uchaguzi, wanahakikisha kuwa maendeleo ya nchi yanakwenda mbele kwa njia ya umoja na mshikamano.
Hivyo, kila mmoja wetu anapaswa kuelewa umuhimu wa haki hii na kuitumia ili kuleta mabadiliko chanya katika nchi yetu.
Kwa Mkoa wa Dar es Salaam ambao ndio unaofunga pazia la uandikishaji katika daftari la kudumu la wapiga kura, tunawahamasisha wananchi kujitokeza ili wawe na sifa ya kushiriki kwenye uchaguzi ujao.
Kama tulivyoeleza awali, tunasisitiza kuwa kila mmoja wetu hana budi kujiandikisha na kuwa na sifa ya kupiga kura.
Kwa umuhimu wa kipekee, hatuna budi kupaza sauti kwa Watanzania vijana ambao kwa sasa sote tunashuhudia namna wanavyotumia mitandao kueleza kero, malalamiko na kila aina ya kadhia wanazokumbana nazo maishani.
Wito wetu kwao ni kujitokeza sasa na kutumia haki yao ya kikatiba kupiga kura kwa wale ambao wanaamini wanaweza kuyafanyia kazi masaibu yao ambao kila uchao wamekuwa wakiyaanika mitandaoni, badala yake waitumie kura yao ambayo inatosha kuwa silaha muhimu ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini. Haitakuwa busara kama wataendelea kupaza sauti kwa njia tofauti.