
Jana, gazeti la Mwananchi lilikuwa na taarifa kuhusu biashara ya vyuma chakavu inavyochochea kuwapo kwa matukio ya uhalifu maeneo mbalimbali nchini.
Biashara hiyo imechochewa na kuwapo viwanda vya kurejeleza vyuma na kutegeneza bidhaa mbalimbali zikiwamo nondo, hivyo watafutaji wa bidhaa za vyuma hutumia mbinu mbalimbali zikiwamo za kihalifu kama wizi wa miundombinu barabarani, vifaa vya majumbani na hata uvunjaji wa misalaba makaburini ili kupata bidhaa hizo.
Hali hii inatishia maendeleo, usalama, na mali za raia pamoja na kusababisha hasara kubwa kwa Taifa. Wizi huu pia unaathiri miundombinu muhimu kama barabara, madaraja, na mifumo ya maji.
Uhalifu huo unaelezwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) na Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) kuwa unasababisha hasara kubwa kwenye miradi ya maendeleo, ikiwamo kung’olewa kwa alama za barabarani, taa za usalama, na kingo za madaraja.
Pamoja na kuwepo kanuni za mwaka 2019 zinazodhibiti biashara ya vyuma chakavu, changamoto ya wizi na uharibifu wa mali za umma bado ipo na inasababisha upotevu mkubwa wa rasilimali na kuzuia maendeleo endelevu.
Serikali inapaswa kuchukua hatua madhubuti kudhibiti tatizo hili kwa kuweka sheria kali zaidi na kuhakikisha utekelezaji wa kanuni unafuatiliwa kikamilifu.
Ni ukweli kwamba Serikali pekee haiwezi kudhibiti changamoto hii, hivyo ni muhimu wananchi nao kuwa sehemu ya ulinzi wa miundombinu. Wananchi wanatakiwa kuwa na uchungu na uharibifu wa miundombinu kwa kuwa athari zake ni kubwa kwa maendeleo na maisha ya kila siku.
Miundombinu kama barabara, mifumo ya maji, na umeme ni kiini cha uchumi na ustawi wa jamii. Uharibifu wake huongeza gharama za matengenezo na huvuruga huduma, hali inayoweza kusababisha ajali, uhaba wa maji, na changamoto ya umeme ya mara kwa mara.
Wananchi wakiwa na uchungu na kukemea uharibifu huu, watachangia kulinda mali za umma na kujenga Taifa imara na lenye maendeleo endelevu kwa faida ya wote na vizazi vijavyo.
Jambo hili likifanyika kwa ukamilifu wake litafanikisha wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka kuhusu, hali itakayosaidia polisi na viongozi kuchukua hatua za haraka.
Pia, ni muhimu kuhakikisha wanunuzi wanahakiki asili ya vyuma wanavyonunua, na kwa wanaokiuka sheria, hatua kali zichukuliwe dhidi yao.
Hivyo, tunaona pia ni wakati mwafaka kuwapo adhabu kali kwa wauzaji na wanunuzi wa mali za wizi, hatua ambayo tunaamini inaweza kuzuia ama kupunguza uhalifu huo.
Hayo yakifanyika na elimu kwa umma ikitolewa, itahamasisha raia na jamii kwa ujumla kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa za wahalifu.
Wanunuzi wa vyuma wanapaswa kutambua kwamba kila chuma cha wizi wanachonunua ni kiini cha kuharibu miundombinu ya umma, hivyo ni muhimu kuwajibika kimaadili na kuhakikisha biashara hiyo haivunji sheria.
Hii pia iwe fursa ya kuboresha miundombinu kwa kutumia vifaa ambavyo si rahisi kuibwa, kama nguzo za zege na alama za barabarani zisizo za chuma. Jambo hili litasaidia kupunguza hasara ya mara kwa mara kwa Taifa na kuhakikisha miundombinu ya umma inakuwa salama.