Tahadhari ya DKA kwa wagonjwa wa kisukari

Diabetes Ketoacidosis au kwa kifupi DKA, ni hali hatari inayotokea watu wenye ugonjwa wa kisukari, hasa aina ya kwanza.

DKA hutokea pale ambapo mwili hauna insulini ya kutosha, na kuacha kutumia sukari kama chanzo cha nishati na hivyo kulazimika kutumia mafuta kama chanzo cha nishati, jambo linalosababisha ongezeko la ketoni kwenye damu.

Ketoni ni asidi zinazoweza kufanya damu kuwa na tindikali nyingi, hali inayoweza kusababisha matatizo makubwa kiafya na hata kifo endapo haitatibiwa kwa haraka.

Maambukizi au magonjwa mengine kama vile homa kali, nimonia, au maambukizi ya njia ya mkojo yanaweza kuongeza mahitaji ya insulini mwilini.

Pia, msongo wa mawazo na uchovu mkubwa. Hali hizi zinaweza kuathiri uzalishaji na matumizi ya insulini mwilini.

Ulaji wa vyakula visivyo na uwiano mzuri wa virutubisho. Ikiwa mtu anakula vyakula vyenye wanga kwa wingi bila insulini ya kutosha, sukari ya damu inaweza kupanda haraka. Matumizi ya dawa fulani kama zile za diuretics na corticosteroids, zinaweza kuathiri viwango vya sukari ya damu.

Dalili za DKA huanza polepole, lakini huweza kuzidi kwa haraka endapo hazitatambuliwa mapema.

Dalili hizo ni pamoja na kiu kikali na kukojoa mara kwa mara, kichefuchefu na kutapika, maumivu ya tumbo, kutoa sauti wakati wa kupumua au kupata shida ya upumuaji, kuhisi kukosa hewa.

 Kupumua na kujisaidia haja ndogo yenye harufu ya tofali za kuchoma au matunda yaliyooza, uchovu mkubwa na kuchanganyikiwa.

Pia ngozi kuwa kavu, midomo na koo kukauka, mapigo ya moyo kwenda kasi.

Kuepuka DKA ni muhimu kuchukua hatua madhubuti, ikiwamo kudhibiti kiwango vya sukari, kwa kupima sukari mara kwa mara. Kumbuka kuangalia viwango vya sukari ya damu mara kwa mara husaidia kutambua mabadiliko mapema. Jua kiwango cha ketoni kwenye damu au mkojo sambamba na kutumia insulini ipasavyo kama daktari alivyoelekeza. Kunywa maji ya kutosha, kwani maji husaidia kupunguza hatari ya kuongezeka kwa ketoni mwilini. Ukiona dalili zozote za DKA, wahi hospitalini kwa matibabu kabla hali haijawa mbaya.

DKA ni hali inayohitaji uangalizi wa karibu na hatua za haraka ili kuzuia au kuepuka madhara makubwa.

Kwa watu wenye kisukari wanapaswa kufuata mwongozo wa matibabu, kufuatilia viwango vya sukari, na kuwa makini wanapohisi dalili zozote za DKA, hasa zile za mwanzo kabisa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *