Tahadhari kuhusu matokeo ya kukiukwa haki za binadamu katika kipindi kingine cha urais wa Trump

Shirika la Human Rights Watch limetoa onyo kali likisema kuwa muhula wa pili wa urais wa Donald Trump ni tishio kubwa kwa haki za binadamu nchini Marekani na duniani kote, na kwamba taasisi huru na jumuiya za kiraia zinapaswa kumuwajibisha rais huyo mpya kuhusiana na suala hili.

Ripoti ya taasisi hii ya haki za binadamu inasema: “Kwa mujibu wa Shirika la Msamaha Duniani, Amnesty International, muhula wa pili wa urais wa Donald Trump huko Marekani ni tishio kubwa kwa haki za binadamu nchini humo na dunia nzima kwa ujumla. Wasiwasi huu umeibuliwa kutokana na historia ya Trump ya kukiuka haki za binadamu katika kipindi cha urais wake uliopita, ambayo ilionyesha kuwa ni muungaji mkono mkubwa wa weupe wanaojiona kubwa bora kuliko jamii nyingine na sera za kupinga demokrasia na haki za binadamu. Mbali na hayo, moja ya ahadi zake za kampeni za uchaguzi ni kuzingira na kuwafukuzwa mamilioni ya wahamiaji na kulipiza kisasi dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa.”

Onyo la shirika hilo la kutetea haki za binadamu kuhusu matokeo hatari ya urais mwingine wa Trump kuhusu haki za binadamu huko Marekani na ulimwenguni kote linatokana na utendaji wake mbaya katika uwanja huo. Wakati wa muhula wa kwanza wa urais wake kuanzia Januari 2017 hadi Januari 2021, Trump aliendeleza fikra na mitazamo ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani na kwa njia isiyo ya moja kwa moja aua hata katika baadhi ya matukio, alitangaza wazi madai ya ubora wa rangi nyeupe na kuwadhalilisha watu wa rangi nyinginezo au Walatino. Pia kwa kupiga marufuku Waislamu wa nchi kadhaa kuingia Marekani, Trump alitekeleza kivitendo mbinu ya ubaguzi wa kidini dhidi ya wahamiaji. Amnesty International imerekodi kesi kadhaa za Donald Trump kukiuka haki za binadamu katika muhula wake wa kwanza wa urais. Kesi hizo ni pamoja na juhudi zake za kuwafukuza wanaotafuta hifadhi na kuwatenganisha wanafamilia katika mpaka wa Marekani na Mexico, kuimarisha mitazamo ya kibaguzi dhidi ya jamii za watu weusi na jamii nyingine za walio wachache, kupitisha siasa za kuadhibu familia za kipato cha chini na kuwanyima huduma za afya huku akichochea ghasia za kubadilisha matokeo ya uchaguzi wa rais.

Donald Trump, rais mpya wa Marekani

Ripoti ya Human Rights Watch imeashiria rekodi ya udikteta ya Trump na kusema:

“Mradi wa  mwaka 2025 ni mpango wa serikali uliotayarishwa na washauri wa zamani wa kisiasa wa Trump na washirika wake, ambao unabainisha sera za kibaguzi na za kuudhi na ambazo huenda zikatekelezwa na serikali yake mpya. Licha ya kuwa amejitenga na mradi huo lakini matamshi yake yanathibitisha wazi uhusiano wake na mradi huu.” Trump pia amesisitiza kuwa atalipiza kisasi dhidi ya wapinzani wake wa kisiasa. Anapinga vikali ufadhili wa misaada ya kibinadamu na juhudi za kuwalinda raia katika mizozo na migogoro mikubwa. Wakati huo huo, uwezekano wa Trump kushirikiana na serikali zinazokiuka haki za binadamu unadhihirisha wazi hatari ya kuimarishwa serikali hizo na hivyo kuwadhuru zaidi watu na kuendeleza unyanyasaji na kutowajibishwa wahalifu na watendajinai ulimwenguni.

Upuuzaji wa Trump kuhusu suala la haki za binadamu na vilevile mtazamo wake wa kindumakuwili kuhusiana na suala hili katika uga wa kimataifa ni miongoni mwa visa muhimu katika rekodi yake nyeusi kuhusiana na suala la haki za binadamu. Alipoingia madarakani katika muhula wa kwanza wa urais wake, Donald Trump alitangaza waziwazi kuwa hangekuwa na uhusiano wowote na masuala ya ndani ya nchi washirika, hasa kuhusu haki za binadamu katika nchi hizo. Huu ndio mtazamo ule ule wa undumakuwili wa Washington kuhusu haki za binadamu, ambapo hufuatilia kwa karibu suala hilo katika nchi ambazo ni maadui au wapinzani wake, huku ikipuuza na kufumbia macho kabisa suala hilo katika nchi rafiki na washirika wake kama vile Saudi Arabia. Mojawapo ya mifano ya wazi kuhusu suala hili ni upuuzaji uliofanywa na utawala wa Trump kuhusu mauaji ya kikatili yaliyofanywa na utawala wa Saudi Arabia dhidi ya mwanahabari Jmal Khashoggi, mpinzani wa Mwanamfalme wa Saudia, Muhammad bin Salman. Licha ya Wasaudia  kukiri kuhusika na mauaji hayo ya kinyama lakini utawala wa Trump haukuchukua hatua yoyote ya kuiadhibu Saudi Arabia kwa kitendo hicho cha kikatili.

Magenge ya ubaguzi wa rangi nchini Marekani yanayoungwa mkono na Trump

Nukta ya kuzingatiwa hapa ni kwamba Donald Trump alijifanya kuwa mtetezi wa haki za binadamu na maslahi ya watu wa Iran katika machafuko yaliyoibuliwa nchini na maadui wa mfumo wa Kiislamu mwaka 2019. Donald Trump, akiwa na matumaini ya kufikia matakwa yake yasiyo halali dhidi ya Iran, aliunga mkono ghasia hizo za wachochezi na kuomba uungaji mkono wa jamii ya kimataifa kwa waibuaghasia hao. Wakati huohuo utawala wa Trump, baada ya kujitoa katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA mwaka 2018, ulipitisha sera ya mashinikizo ya juu kabisa dhidi ya Iran na kutekeleza vikwazo vikali na vya kikatili zaidi dhidi ya taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa njia hii ni wazi kuwa Trump anatumia suala la haki za binadamu kama chombo cha kuzishinikiza nchi zinazopinga ubeberu wa Marekani, na kwa upande mwingine kufumbia macho ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu unaofanywa na washirika wa Marekani ulimwenguni.