Tabora yaachana na Kocha Mkongomani, yamchukua Mzimbabwe

UONGOZI wa Tabora United, umefikia makubaliano ya kuachana na kocha mkuu wa timu hiyo, Anicet Kiazayidi huku nafasi yake ikichukuliwa na Mzimbabwe, Genesis Mangombe.

Haijafahamika sababu za kuvunjwa kwa mkataba wa kocha huyo raia wa DR Congo ambaye hivi karibuni alirejea nchini kwao kwa ajili ya kufanya kozi ya refresh.

Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Tabora United, kimeliambia Mwanaspoti kuwa uongozi wa timu hiyo na kocha huyo wamefikia makubaliano ya pande zote mbili kuvunja mkataba.

“Siwezi kuzungumza sababu za kuachana na kocha aliyepita ambaye ameisaidia timu yetu kuwa kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo hadi sasa, ninachoweza kusema ni makubaliano ya pande zote mbili.

“Hata tuliyemleta ni kocha mzuri, hivyo tunaamini atatuvusha katika malengo yetu kwa msimu huu kwani tunatamani kumaliza nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu,” alisema mtoa taarifa huyo.

lipotafutwa Kocha Kiazayidi kuzungumzia suala hilo, alisema amefikia uamuzi huo kwa makubaliano ya pande mbili, huku akisita kueleza wazi kwa kina sababu zilizomfanya kuondoka ndani ya timu hiyo.

Kwa upande wa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tabora United, Charles Obiny alisema kuna taratibu za kiuongozi zinaendelea juu ya hilo na zitakapokamilika wataweka wazi, hivyo mashabiki na wadau wa timu hiyo waendelee kuwapa sapoti kwa michezo ijayo.

Tabora United ilimchukua Kiazayidi Novemba 2024 kuziba nafasi ya Mkenya Francis Kimanzi aliyeondolewa baada ya timu hiyo kuwa na mwenendo mbaya katika Ligi Kuu Bara msimu huu.

Wakati hayo yakiendelea, taarifa zinabainisha kuwa Mangombe tayari yupo nchini ambapo anaweza kutambulishwa muda wowote kuanzia sasa baada ya kumalizika kwa taratibu zote za kimkataba ambapo amekubali kuinoa timu hiyo hadi mwisho wa msimu huu.

Taarifa zinasema kuna uwezekano mkubwa wa Mangombe kushuka na msaidizi wake mmoja atakayeungana naye kwenye majukumu yake ndani ya Tabora United.

Kwa sasa Tabora United ipo nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara baada ya kucheza mechi 23 ikifanikiwa kukusanya pointi 37, ikishinda mechi 10, sare saba na vipigo sita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *