Tabora Utd Vs Singida BS kuchezwa kesho saa 4 asubuhi

Dar es Salaam. Mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Tabora United dhidi ya Singida Black Stars uliokuwa uchezwe leo Novemba 24 kwenye Uwanja wa Ally Hassan Mwinyi Tabora umeahirishwa baada ya mvua kubwa kunyesha na kusababisha uwanja kujaa maji.

Kutokana na kadhia hiyo, mchezo huo umepagwa kuchezwa kesho Jumatatu Novemba 25, 2024 saa 4:00 asubuhi.

Akithibitisha kuahirishwa kwa mchezo huo kamishna kutoka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Said Mkai amesema wamefanya jitihada za kuhakikisha mchezo huo unachezwa lakini imeshindikana.

“Mchezo nambari 94 kati ya Tabora United dhidi ya Singida Black Stars tumeuahirisha baada ya mvua kubwa kunyesha na uwanja kujaa maji, tumeukagua mimi, waamuzi pamoja na wachezaji tukagundua kwamba mchezo hauwezi kuchezwa sababu ya maji kujaa na kusababisha mpira kushindwa kudunda.

“Tumefanya jitihada za kutoa maji ili mchezo uweze kuchezeka  lakini mvua inakata na kuongezeka hivyo kwa mujibu wa kanuni ya 17 kifungu kidogo  cha 30, kinachohusu taratibu za mchezo tumeuahirisha huu mchezo mpaka kesho Novemba 25, 2024 saa 4:00 asubuhi kwenye uwanja huuhuu,” amesema na kuongeza Mkai.

Baada ya kuahirishwa kwa mchezo huo Mwananchi lilishuhudia Askari polisi wakimwagwa uwanjani kwa lengo la kuhakikisha hakuna vurugu zinazoweza kutokea kwenye uwanja huo na baada ya watu kutawanyika askari hao waliondoka kwakua hakuna changamoto yoyote iliyotokea.

Mkai amesema makubaliano ya mchezo huo kuahirishwa yamefikia kwa timu zote mbili kushirikishwa na kuamua uahirishwe.