
Siku tano baada ya Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora kufungiwa, uongozi wa Tabora United umeuchagua Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza kwa mechi yake ya nyumbani dhidi ya JKT Tanzania, Machi 7, 2025.
Taarifa ya Tabora United imefafanua kuwa timu hiyo inahamia CCM Kirumba huku uongozi wake ukiendelea na juhudi za kuuboresha Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi.
“Uongozi wa timu ya Tabora United, unapenda kuwajulisha umma, mashabiki na wadau wa mpira wa miguu kuwa utatumia Uwanja wa CCM Kirumba uliopo jijini
Mwanza kama Uwanja wa nyumbani katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya JKT Tanzania, utakaochezwa siku ya ljumaa Machi 07, saa
16:00 kamili jioni.
“Tabora United FC itatumia Uwanja huo kutokana na kufungiwa kwa Uwanja wa
Ali Hassan Mwinyi ambao ulikuwa ukitumika kwa michezo yetu ya nyumbani.
Aidha tunapenda kuwatoa hofu mashabiki zetu kuwa, uongozi kwa kushirikiana na
serikali ya mkoa pamoja na wadau mbalimbli tunaendelea na ukarabati wa uwanja ili uweze kutumika kwenye michezo yetu ya ligi kuu iliyobakia. Viongozi tunawaomba mashabiki zetu waendelee kutuunga mkono katika mchezo ambao utachezwa siku ya ljumaa CCM Kirumba Jijini Mwanza,” imefafanua taarifa hiyo ya Tabora United.
Uamuzi wa kuufungia Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ulitangazwa mara baada ya kumalizika kwa mechi ya Ligi Kuu ambayo wenyeji Tabora United waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Dodoma Jiji wiki iliyopita.
“Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeufungia uanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora kutumika kwa michezo ya Ligi kwa kukosa vigezo vya kikanuni na sheria za mpira wa miguu.
“Miundombinu ya uwanja huo haikidhi matakwa ya Kanuni kama ilivyoainishwa kwenye masharti ya Kanuni ya Leseni za Klabu. Kufuatia uamuzi huo, timu zinazotumia uwanja huo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia uwanja mwingine kama Kanuni inavyoelekeza mpaka uwanja wao utakapofunguliwa, baada ya kufanyiwa marekebisho na kukaguliwa na TFF.
“TFF inazikumbusha Klabu zote kuendelea kutunza na kuboresha miundombinu ya viwanja,” ilifafanua taarifa ya TFF.
Katika mchezo huo wa Tabora United dhidi ya Dodoma Jiji FC, nyasi za Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi zilionekana kukauka kwenye maeneo mengi ya uwanja na kuupa muonekano usiovutia.
Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi umekuwa ngome imara ya Tabora United kwani idadi kubwa ya pointi zake msimu huu imechukulia hapo. Timu hiyo imecheza mechi 11 za Ligi ikiwa hapo ambapo imepata ushindi mara tano, imetoka sare nne na imepoteza michezo miwili.