
DAKIKA 90 za Tabora na Kagera Ijumaa hii katika robo fainali ya FA zina maana kubwa. Ni mechi itakayopigwa ndani ya Al Hassan Mwinyi majira ya saa 10 ambayo kwa yeyote atakayefungwa ni kama msimu wake wa mafanikio umeishia hapo.
Ni mechi ambayo yoyote atakayeshinda ataendeleza ndoto za kuwania kombe pekee msimu huu kwani kwenye Ligi Kuu Bara uwezekano wa kitakwimu wa timu hizo kubeba ubingwa wa Ligi ni finyu zaidi. Tabora ambao wako nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi wakiwa na pointi 37, wanaweza kwenda kileleni kama Simba,Yanga zitapoteza mechi zao zote na wao kushinda zote.
Robo hiyo, itaamua nani bora kati ya timu mwenyeji Tabora United dhidi ya Kagera Sugar ambayo itaingia ikiwa mnyonge kutokana na kufungwa michezo miwili ya ligi msimu huu.
Timu hizo zinakutana zikiwa na mabenchi mapya ya ufundi huku Kagera Sugar ikiwa na faida kubwa kwani tayari kocha wao Juma Kasema kawaongoza kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora wakiitandika Namungo mabao 3-0 huku kwa upande wa Tabora United kocha Genesis Mangombe utakuwa mchezo wake wa kwanza.
Rekodi za jumla zinainyima nafasi Kagera Sugar kufurukuta mbele ya Tabora United ambayo ni msimu wake wa pili tangu imepanda daraja kwenye mechi nne walizokutana wenyeji wameshinda mara mbili huku Kagera ikishinda mara moja na suluhu moja.
Lakini ukiondoa ubora wa Tabora United ikishinda mechi mbili za Ligi Kuu Bara safu yao ya ushambuliaji haina makali sana kwani kwenye mechi mbili walizoshinda imepachika mabao matatu ikianza na ushindi wa mabao 2-1 na ushindi wa 1-0 wakati kwa upande wa Kagera ushindi wao mmoja walishinda mabao 3-0.
Mchezo wa kwanza kwa timu hizo kukutana ilikuwa Oktoba 30, 2023 hakukuwa na mbabe kati yao mchezo uliisha kwa suluhu, Aprili 17, 2024 Kagera Sugar ikiwa ugenini ilishinda mabao 3-0, Machi 11, 2024 Tabora United iliibuka na ushindi wa bao 1-0 na mchezo wa Februari 11 mwaka huu imeitandika Kagera mabao 2-1.
Kocha mkuu wa Kagera Sugar Juma Kaseja, alisema wamejiandaa vizuri kuhakikisha wanashinda mchezo huo na kutinga robo fainali huku akiweka wazi kuwa hawatarajii mchezo rahisi wamejiandaa kupambania nafasi ili kuweza kusonga hatua inayofuata.
“Tumejiandaa vizuri, najua tunakutana na timu ngumu na nzuri lakini malengo yetu ni kuingia robo fainali ya mashindano haya tutaingia kwa kumuheshimu mpinzani wetu tunatambua wanatimu nzuri na ya ushindani. Hivyo lazima tupambane tushinde,” alisema Kaseja ambaye ni kipa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars mwenye rekodi za kuvutia.
Kocha wa Tabora United, Mangombe alisema wako vizuri tayari kwa mchezo huo na malengo yao ni kupata matokeo ambayo yatawafanya wasonge hatua inayofuata na anatarajia mchezo mzuri na wa ushindani.
“Malengo yetu ni kufika fainali na huwezi kufika huko bila kufika kwanza robo fainali halafu nusu. Sasa tunataka tuifunge Kagera Sugar. Tutatumia vizuri uwanja wetu wa nyumbani tumejiandaa vyema kuhakikisha ndani ya dakika 90 tunakuwa bora zaidi yao.” alisema.
Kagera Sugar ipo nafasi ya 14 kwenye ligi baada ya kucheza mechi 23 ikikusanya pointi 19.