Tabia hii ya vijana Dodoma idhibitiwe mapema

Binadamu tunaishi kwa maisha ya mchakamchaka kama ngiri wa mwituni ambao hukimbizana kila uchwao ili kutafuta riziki ya kuwafanya waendelee kuishi.

Maisha ya mtu asiyekuwa na ajira rasmi yanahitaji ujanja, wakati mwingine maarifa hata kabla ya kutumia nguvu ili mradi afanikiwe kupata mkate wa kusogeza siku na tarehe.

Inaweza kuwa ni ubunifu katika kutumia fursa zinazowazunguka vijana ili mradi watumie jasho lao kutengeneza kipato, ili tu wasionekane kwamba wamekaa bila kazi, ingawa kwa upande mwingine ni hatari.

Kuna mtindo umezuka kwa vijana katika siku za hivi karibuni na wanaoutumia, wanapata fedha nyingi kwa siku hata wakati mwingine kuwa zaidi ya wale wanaojiita kuwa wameajiriwa.

Katika maeneo ya vijijini ambako barabara za lami hazijafika, umezuka mtindo wa vijana kutafuta fedha kwa mtindo wa kuziba mashimo na kisha kusubiria wapita njia ili wawape fedha.

Kwa miaka ya hivi karibuni mpango huo ulikuwa ukiendeshwa zaidi na watoto wa umri wa miaka 10 hadi 14 na mara nyingine walifanya hivyo siku za mapumziko ya wiki.

Kwa siku za hivi karibuni kumekuwa na tofauti, watu wazima wa umri wa kati ya miaka 20 hadi 35 ndio wanaofanya kazi na kwa sasa kumekuwa na kiwango ambacho kinakusanywa, tena baadhi ya maeneo imekuwa ni kwa kutumia nguvu na vitisho.

Mfano mzuri ni barabara ya kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) – Nghong’ona – Muungano ambayo inapita katika vilima.

Unapopita njia hiyo kwa mtu anayetumia usafiri wa pikipiki ni muhimu kujiandaa walau kuwa na Sh1,500, kwani lazima ukutane na vituo visivyopungua vitatu au zaidi ambavyo vijana wamesimama na kufunga njia wakitaka malipo ya Sh500 ili uruhusiwe kupita.

Bei hizo hutofautiana, kwani wakati mwenye pikipiki akitakiwa kulipa Sh500, mtu anayetumia gari, yeye analazimika kulipia Sh1000 kila ataposimamishwa, huku watembea kwa miguu wakiachwa kupita bila shida.

Kuna mambo yanatatiza kuhusu usalama wa watumiaji wa njia hizo na miongoni mwayo, ni kitendo cha kusimama kwenye kona mahali ambako ni mbali na mwingiliano wa watu, lakini kwa siku hizi wanazuia njia kwa mawe.

Uko wapi usalama wa watu pale wanapofunga barabara kwa mawe makubwa na kuweka miiba ili wakilipwa wafungue njia?

Kuna kila sababu ya kuzuia mpango huu, kwani unafuga majambazi watarajiwa. Mashimo yanayozibwa hata kama ingekuwa kwa namna gani, hayana madhara yoyote kwa watumiaji wa njia hizo.

Hakuna matengenezo ya kuziba shimo kwa ndoo moja au mbili za udongo halafu unakaa kutwa nzima kukusanya pesa kutoka kwa watu wanaopita wakati mwingine kwa mara ya kwanza na hawajui mpango unaofanyika huko.

Tarura na Polisi watupie macho kuangalia barabara hii ambayo inaonyesha dalili za wazi kuwa inaweza kugeuka kichaka cha wezi na waporaji, kwa kutumia mgongo wa kuziba mashimo.

Hii ni njia moja tu, lakini mtindo wa aina huu umeenea karibu maeneo mengi nchini, hasa barabara za vijijini maeneo yanayotajwa kuwa ni korofi, ingawa kwenye maeneo korofi kweli hawawezi kuziba, badala yake wanachagua maeneo ambayo vifaa vya kazi ni jembe na chepe kwa ajili ya kusogeza udongo tu.

Nguvu wanazotumia vijana hao zinapaswa kuhamishiwa katika maeneo mengine kwa ajili ya kusaidia Taifa kwenye suala la uchumi na hasa katika kilimo, kwani wengi wanaofanya kazi hiyo wako vijijini.

Huu ni ubabaishaji mtupu kwa wananchi wanaotumia njia hizo, wanalazimishwa kufanya vitu ambavyo haviko kabisa, badala yake wanataka kutengeneza migogoro na ugomvi.

Nani ana mamlaka ya kusema wafunge barabara, tena maeneo ya porini wakati wanajua wapitanjia wanaotumia maeneo hayo wengi ni watu wenye uhitaji? Kuwa na pikipiki au gari siyo kigezo cha kumuonyesha mtu kwamba anamiliki fedha.

Jambo hili na mambo yanayofanana na haya yakemewe na kuzuiwa ili kuwaondolea hofu wapitanjia, na kama kuna haja ya kufanya hivyo Serikali itangaze wazi kuwa wanaopitia njia hizo, wanapaswa kulipia, tena kuwe na kituo kimoja siyo kusimama kwenye mapori.

Utafutaji wa fedha una njia nyingi, lakini njia hii siyo sawa na si salama, kwani kunaweza kuibuka watu wengine wasio waungwana wakatumia mwanya huo kufanya matukio makubwa, yakiwemo ya utekaji.