
Mwaka 1995, mwanasaikolojia na mwandishi wa makala za sayansi, Daniel Goleman alichapisha kitabu kilicholeta wazo jipya kuhusu uwezo wa kuzitawala hisia “emotional intelligence.”
Kitabu hicho kilionyesha kwamba kuzielewa na kuzitawala hisia kunaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa sana katika mafanikio yetu.
Pia, hisia zina uhusiano mkubwa na jinsi watu wanavyofikiri kuhusu hisia na tabia za mwanadamu kwa ujumla.
Lakini, uwezo wa kutawala hisia unatambuliwaje katika maisha ya mtu ya kila siku?
Katika miaka miwili iliyopita, nimekuwa nikiulizwa swali hilo, nilipokuwa ninafundisha watu mbalimbali kwenye warsha, semina na makongamano. Katika kusoma na kutafuta zaidi kuhusu uwezo wa mtu kuzitawala hisia zake, nimegundua baadhi ya matendo yanayoonyesha jinsi uwezo wa kuzitawala hisia unavyoonekana katika maisha yetu halisi na ya kila siku.
Hapa ninakuchambulia tabia 13;
Unafikiria kuhusu hisia
Uwezo wa kutawala hisia unaanza na kile tunachoita kujitambua na kutambua jamii yako, uwezo wa kutambua hisia (na athari zake) kwako na kwa watu wengine.
Utambuzi huo unaanza kwa kufikiria, unajiuliza maswali, ni hisia gani zina nguvu sana kwako.
Udhaifu wako ni nini?
Hisia ulizonazo zinaathirije mawazo na uamuzi unaofikia?
Ni nini kinachowachochea wengine kusema na kufanya?
Kutafakari maswali kama hayo kutakusaidia kuwa na uelewa ambao utakusaidia kuutumia kwa faida.
Kutulia kunamaanisha kuchukua muda kidogo wa kufikiri kabla ya kusema na kutenda.
Hii itakusaidia usivurugwe na hali na itakusaidia usitoe ahadi haraka.
Kwa maana nyingine, kutulia kutakuzuia kufanya uamuzi wa kudumu kutokana na hisia za muda ulizonazo kwa wakati huo, yaani kwa kukurupuka.
Kutawala mawazo yako
Huwezi kudhibiti mambo mengi yanayotokea ambayo hugusa hisia zako. Kwa kujitahidi kutawala mawazo yako, unajizuia mwenyewe usiwe mtumwa wa hisia zako, unajiruhusu mwenyewe kuishi kulingana na malengo na thamani yako.
Unafaidika unapokosolewa
Hakuna mtu anayefurahia kuambiwa makosa yake. Lakini unajua kwamba kukosolewa ni fursa ya kujifunza, hata ikiwa umeambiwa kwa njia mbaya. Na hata ukosoaji usipokuwa na msingi, bado unakupa fursa ya kujua mawazo ya watu wengine.
Unakuwa mkweli
Kuwa mkweli hakumaanishi kusema kila kitu kujihusu kwa kila mtu, wakati wote.
Inamaanisha kusema unachomaanisha, maanisha unachosema na shikamana na maoni na kanuni hii zaidi ya kitu kingine chochote. Unajua kwamba si kila mtu atathamini maoni na hisia zako. Lakini kuna wale ambao watayathamini.
Unawahurumia wengine
Uwezo wa kuonyesha huruma, ambao unahusiana na kuelewa mawazo na hisia za wengine, unakusaidia kuwa na uhusiano mzuri na wengine.
Badala ya kuwapuuza na kuwahukumu wengine, jitahidi kuona mambo mengi mazuri kwao.
Unawapongeza wengine
Binadamu wote wanapenda kutambuliwa na kuthaminiwa. Unapowapongeza wengine, unatosheleza kiu hiyo na kujenga sifa ya kuaminika.
Hii inaanza kutokea pale unapotambua mazuri ya watu wengine. Kisha, unawapongeza kwa mambo mazuri waliyoyafanya, kwa kufanya hivyo unawachochea watu wengine kuwa bora na wafanye vizuri zaidi.
Unajibu kwa njia nzuri
Mwitikio hasi unachangia kuumiza hisia za wengine. Kwa kutambua hili, kudhibiti hisia kunakuzuia kukosoa pale unapojibizana na wengine, hivyo mpokeaji anaona hilo kuwa msaada badala ya kuwa madhara. Hata kama hisia zako zimechafuka na unaona unashindwa kujizuia, bado unaweza kujitahidi kujibu kwa staha pasipo kuropoka, kutukana, kukejeli au kumshushia mwingine hadhi yake.
Unaomba msamaha
Inahitaji nguvu nyingi na ujasiri kusema samahani. Lakini kufanya hivyo kunaonyesha kwamba wewe ni mnyenyekevu, sifa ambayo itawavutia watu wengine kwako.
Uwezo wa kutawala hisia utakusaidia kujua kwamba kuomba msamaha, mara zote hakumaanishi kwamba umekosea. Inaamisha kwamba unathamini uhusiano kuliko kupambania hadhi yako.
Unasamehe na kusahau
Kubaki ukiwa na kinyongo ni sawa na kuacha kisu katika jeraha. Wakati mtu aliyekukosea anaendelea tu na maisha yake, hutakuwa ukijipa mwenyewe fursa ya kupona.
Unaposamehe na kusahau, unawazuia wengine kukufungia kwenye gereza la hisia, hivyo unajiruhusu mwenyewe kuwa huru na kusonga mbele.
Unatunza ahadi
Ni jambo la kawaida kwa watu kuvunja ahadi pale wanapohisi ni sawa tu kufanya hivyo.
Bila shaka, kuahirisha ahadi ya kukutana na rafiki zako ili kutazama filamu kunaweza kuwa na madhara madogo zaidi ya kuvunja ahadi na mtoto wako ama miadi mikubwa yenye muda maalumu ya kibiashara.
Unawasaidia wengine
Njia moja kuu ya kuchochea hisia za wengine ni kuwasaidia. Watu wengi hawajali ikiwa wewe umesoma au hujasoma, watu hawajali umefanikiwa au la, bali wanathamini muda unaotenga katika ratiba yako yenye shughuli nyingi ili kuwasikiliza na kuwasaidia.
Unalinda hisia zako
Unatambua kwamba uwezo wa kutawala hisia una upande wa pili pale ambapo mtu mwingine anaweza kujaribu kuumiza hisia za wengine kwa ajili ya maslahi ya binafsi ama mipango yake.
Na hiyo ndiyo sababu unapaswa kuendelea kudumisha uwezo wa kuzitawala hisia zako ili kujilinda mwenyewe na kuwalinda wale wanaokuzunguka.