
Kuna hizi taasisi za ndani na nje ya nchi zinazokunja hela inayoeleweka zikidaiwa kuwatetea raia wa dunia yetu hii, zikiongozwa na ‘baba lao’ Umoja wa Mataifa, wenye vitengo vyake kadhaa kwa ajili ya kutetea haki za raia wa dunia hii.
Mstaafu wetu anapoona taasisi hizi zinavyosimamia haki za raia linapokuja suala la wastaafu, hujikuta akijiuliza kama zinatetea raia wa dunia yetu hii hii au raia wa sayari ya Pluto, kama wapo!
Tuangalie hili ‘baba lao’, Umoja wa Mataifa. Moja ya kanuni zake kuu kwa mataifa yaliyotaka kujiunga nalo ni ile ya kuitaka nchi husika kuwajali na kuwahudumia wazee wa nchi hiyo na kuhakikisha kuwa angalau baada ya miaka mitatu, hata minne, wanawapa nyongeza ya pensheni yao ili waweze kukabiliana na hali ngumu ya maisha kama raia wengine wote wa nchi.
Tatizo linaanzia hapa. Umoja wa Mataifa haujatamka wazi kwamba nchi ambayo haitekelezi kanuni muhimu sana hiyo kwa wazee wake, itachukuliwa hatua gani.
Kweli, linawatetea wanasiasa na kutoa kauli za kuwanyong’onyesha na kuwadhibiti wapenda kuomba misaada, lakini linaishia kwa haohao na halisemi kinagaubaga kwamba litaichukulia hatua gani nchi isiyotekeleza kanuni hii muhimu ya kuwajali wazee wa nchi yake, labda kama na lenyewe linaona wazee siyo raia.
Ndiyo maana mstaafu wa kima cha chini wa ‘Tanzatozo’ hii anakaa miaka 20 sasa akipokea Sh100,000 kwa mwezi bila nyongeza na hakuna hata anayekohoa.
Hii ni Siri-kali inayopitisha bajeti ya Sh500 bilioni na ushee kwa mwaka kuwanunulia magari ya V8 waheshimiwa wake, lakini haiwezi kuweka bajeti ya japo shilingi milioni 500 ya kuwapa nyongeza ya pensheni yao wala kuwapa matibabu ya bure wastaafu wake.
Kwa miaka 20 hatujasikia Umoja wa Mataifa na taasisi zinazodai kutetea haki za raia kuiuliza ‘Tanzatozo’ kuwa inawezekanaje wastaafu wa kima cha chini wanaishi kwa pensheni ya laki moja kwa mwezi bila nyongeza yoyote, huku nchi ikinunua magoli ya wacheza mpira kwa mamilioni, huku wastaafu wakipiga miayo kwa kupata pensheni isiyokuwa na nyongeza kwa miaka 20!
Labda wanataka wote waishie Kinondoni ndipo watangaze nyongeza ya pensheni ya wastaafu wasiokuwepo!
Kama vile hilo halitoshi kuwaumiza zaidi wastaafu, waheshimiwa wa Siri-kali sasa wana kazi ya kuwaundia kamati zisizofika mwisho na kutoa majawabu, za posho, marupurupu na marapurapu yake, kujadili na kuafikiana zimuongeze kiasi gani mstaafu wa kima cha chini wa nchi hii na kila mwaka kamati zinaundwa, lakini hazitoi majibu na mstaafu anabaki kung’aa macho akielekea Kinondoni fasta.
Waheshimiwa waache mizaha na maisha ya watu! Yaani miaka 63 ya Uhuru bado watu wanakaa vikao visivyoisha vya kuafikiana vimlipe kiasi gani mstaafu aliyeipa nchi hii Uhuru wake na kuijenga kwa damu na jasho lake mpaka kuifikisha hapa pa mwakilishi wa mstaafu kulipwa shilingi milioni…mama wee!.. kumi na nne kwa mwezi lakini mstaafu aliyelianzisha Taifa hili anapata ‘Laki si pesa’ kwa mwezi? Taasisi za haki za raia zipo wapi, au mstaafu siyo raia? Mmezibwa midomo?
Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine zinazodai kutetea raia zikae chini na kujiuliza, zinamtetea nini raia wa nchi hii iliyo mwanachama wake ambaye amekaa miaka 20 bila nyongeza ya pensheni yake na hali yake kuwa ngumu zaidi, lakini taasisi hizo zimeuchuna tu bila hata angalau kutoa tu kikohozi cha umbeya? Au yanakuwa yaleyale ya kwamba mradi nchi inatoa ada yake kunakohusika, basi wastaafu wake watajiju.
Wakati umefika sasa wa wastaafu kuwa na jambo letu wenyewe. Wafanyakazi wanakuwaga na jambo lao na waheshimiwa japo linaishia kuwa jambo tu. Sisi tujitofautishe. Ni wazi kuwa hizi taasisi zinazodai kuwatetea raia wa nchi hazifanyi inavyotakiwa. Zinajipa maujiko tu. Wakati umefika sasa wa ‘mtoto acha kupiga mayowe, waje watu waone wenyewe’, potelea mbali kwamba tulistaafu na miaka 60 ukijumlisha na miaka 20 ya kudai nyongeza ya pensheni wengine wetu wana miaka 80. Tuamke na uzee wetu.
Tujipange ili siku twende zilipo taasisi hizi na kuzihoji kwamba zinamtetea raia yupi wakati raia ambaye kutokana na kuipa nchi yake Uhuru wake na kuijenga kwa damu na jasho lake, ndiye raia namba moja wa nchi hii, lakini anapokea pensheni ya Sh100,000 kwa mwezi, huku taasisi zenyewe zipo tu, zikijipigia upatu kwamba zipo kusimamia haki za raia! Tukaziulize, raia wapi? Labda kama zimeishanong’onezwa kwamba tumeshahamia Burundi!
Tukisubiri mpaka kamati zichoke posho na marupurupu yake kama siyo marapurapu, na hatimaye ziweze kutamka kwamba zitawapa nyongeza ya Sh200,000 wastaafu wake, tutakuwa tumeula wa chuya kwa uvivu wa kuchambua tukiwa Kinondoni! Yule mwana mwema wa Msoga hakuhitaji kamati ili kujua awalipe nini wastaafu wake. Ni utashi tu.