TAAMULI HURU: Rais Samia kielelezo cha uwezo wa mwanamke katika uongozi

Jumamosi iliyopita ilikuwa ni Siku ya Wanawake Duniani, japo siku yenyewe imeipita, hizi ni salaamu zangu za Siku ya Wanawake Duniani kwa wanawake wote wa Tanzania. Kwa Tanzania, Maadhimisho rasmi ya kitaifa yamefanyikia Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha, mgeni Rasmi akiwa ni Rais Samia.

Kwa vile kuna watu wameamua, Oktoba 2025, twende na mwanamke, natoa wito, tusiende na mwanamke tu, bali twende na wanawake, tuchague wabunge wanawake na madiwani wanawake, tufikishe ile 50/50 ya Beijing, kisha tuvifute viti maalumu.

Nikimuangalia na kumsikiliza Rais Samia, tangu ameshika urais wa Tanzania, kiukweli ameutendea haki kustahili kupewa maua yake. Ameleta mwamko na msisimko mkubwa wa ajabu wa ukombozi wa mwamke.

Wanawake wengi wa Tanzania, sasa sio tu wanajituma na wanajibeba, bali sasa wanawake wanajiamini, wanajitambua, wanatembea vifua mbele, tena kuna baadhi wa wababa ndani ya nyumba zetu, tunakoma ila hatusemi tu.

Zamani tulikuwa kwa vile ni sisi tunanunua chakula, na tumekilipia bei ya jumla, tulikuwa tukitaka kula, tunajilia tu tunavyotaka, sasa hivi sio hivyo tena, ukitaka kula sio unajichukulia na kujilia, sasa ni lazima uombe chakula, upakuliwe ndipo ule.

Hivyo, hiyo mitano tena ikikamilika, hapo Oktoba 2025, kutakuwa hakuna sababu kabisa ya wanawake wa Tanzania kuendelea kubebwa kwa viti maalumu, wengi wanabweteka. Rais Samia hakubebwa, ifike mahali wanawake wote muache kubwetekea kubebwabebwa, sasa mjibebe kama Rais Samia.

Kwa miongo kadhaa, wanawake wamekuwa wakinyanyaswa, kubaguliwa, kudhalilishwa na kudharauriwa kwa sababu tu ya jinsia yao, lakini urais wa Rais Samia kama Rais mwanamke wa kwanza, umeleta ukombozi mkubwa kwa wanawake wa Tanzania.

Ili kuwatendea haki wanawake kupata haki sawa na wanaume, ukabuniwa utaratibu maalumu wa upendeleo kwa wanawake, unaoitwa “affirmative action”, hivyo mkutano wa kimataifa wa wanawake duniani, uliofanyinyika jijini Beijing nchini China, ukatangaza ili kuleta usawa wa kijinsia duniani, nafasi za wanawake kwenye uongozi lazima zifikie 50/50 kwa wanawake na wanaume.

Ili kufikia lengo hilo, Tanzania tukaanzisha nafasi za upendeleo za wanawake katika maeneo mengi, vikiwemo nafasi za viti maalumu bungeni na kwenye udiwani.

Miongoni mwa nafasi ambazo hazikuwahi kufikiriwa kushikwa na mwanamke ni nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia CCM. Japo CCM ilimteua Rais Samia kuwa makamo wa rais, hakuna mtu yeyote aliyewahi kufikiria kuwa kuna siku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaweza kufariki akiwa madarakani.

Hivyo, ilipotokea JPM kafariki akiwa madarakani, na kwa mujibu wa Katiba, Makamu wa Rais, ndiye anapaswa kuapishwa kuwa Rais. Kwa vile Makamu wa Rais ni mwanamke, kulitokea kizungumkuti ambacho hakikutangazwa, na watu kujiuliza sasa itakuwaje?

Kulipotokea kifo cha JPM, kulitokea kizungumkuti fulani kwa sababu Makamu wa Rais alikuwa ni mwanamke, watu wakiulizana itakuwaje? Za chini ya kapeti zinasema, taarifa ilipomfikia Mkuu wa Majeshi (CDF), Venance Mabeyo, ndipo akawaamuru wahusika Katiba ifuatwe, ndipo Makamu Rais Samia, akapelekewa taarifa na kutangazia hukohuko Tanga. Uthibitisho wa kizungumkuti hiki, ni baada tu ya Rais Samia kuapishwa kuwa Rais, kazi ya kwanza ni pangua pangua ya Ikulu.

Hii inamaanisha, kama lisingetokea lile tukio la Mach 17, 2021, Tanzania isingepata Rais mwanamke. Naomba niwaibie jambo jingine kuhusu urais wa mwanamke, lisingetokea lile tukio, yaani JPM angeendelea mpaka 2025, amini nakuambia, CCM isingemsimamisha mgombea mwanamke kwenye urais. Hivyo, nikisema Tanzania tumepata Rais mwanamke kwa kudra tu za Mwenyezi Mungu, lakini baada ya Samia kuwa Rais, akashauri uchaguzi wa mwaka 2025, twende na mwanamke, na Watanzania tumchague Rais mwanamke na kukamilisha usawa wa kijinsia.

Kwa vile uchaguzi wa 2025, Watanzania tunakwenda kumchagua Rais mwanamke, naomba tutangaze mwaka huu uwe wa ukombozi kwa mwanamke. Wanawake wenye sifa kutoka vyama vyote, wajitokeze kwa wingi kugombea kumuunga mkono Rais Samia, na vyama viteue wagombea wanawake kwa wingi kwenye majimbo yote ya ubunge, udiwani, uwakilishi na shehia, kisha Watanzania tuwapigie kampeni ya nguvu, tuwachague hata kupitiliza hiyo 50/50.

Na baada ya kufanikiwa kuchagua rais mwanamke, wabunge, wawakilishi na madiwani wa kutosha kupitiliza hata hiyo 50/50, najua kazi ya kwanza ya Bunge jipya ni kufanya mabadiliko madogo ya Katiba kwa hati ya dharura, kuiingiza Dira ya Maendeleo 2025, kama haitaingizwa Bunge la Aprili, hivyo tuitumie fursa hiyo kuvifuta rasmi viti maalumu, kwa sababu usawa wa kijinsia utakuwa umekamilika kwa Rais Samia kuwawezesha wanawake kujibeba, hakuna tena sababu ya kuendelea kubebwa bebwa na mbeleko ya viti maalumu, maana kuendelea kuwepo kwa viti hivi, kunapelekea wanawake kuendelea kubweteka.

Kwa kuwa Rais Samia ni mwanamke na ameweza kuwa Rais wa Tanzania kwa kujibeba, Urais wa Samia 2025, uwe ni ukombozi wa mwanamke, hakuna tena kubebwa, wanawake mjibebe!

Heri ya Siku ya Wanawake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *