JINA lake halisi Suzana Ahmad Salum lakini ni maarufu mitandaoni kwa ‘Suzy Bale’.Wapenzi wa mitandao hasa Tiktok na YouTube wanamfahamu vyema kutokana na mbwembwe zake.
Mwenyewe anajiita ‘Malkia wa Uswazi’ ndio mwenye msemo wa neno ‘We Huogopi’ ambalo lilikuwa maarufu nchini tangu mwaka jana.
Mchekeshaji huyo alianza kazi zake mwaka jana lakini ilikuwa kama masihara tu mitandaoni alipokuwa anazungumza na baadhi ya watu wakaanza kumfuatilia.
Video yake ya kwanza ambayo ilipata umaarufu mkubwa ilikuwa ‘We Huogopi’ ambayo ndani yake alikuwa akielezea wimbo wa Billnass ambayo ilisambaa na kumpa umaarufu.
“Mimi sikuwa na simu ila nilipokuwa nazungumza kuna rafiki yangu alinirekodi na kuitupia Tiktok, sasa kama kesho yake nashangaa dada yangu ananipiga Suzy umekuwa maarufu mitandaoni unatafutwa hatari, nikajiuliza sijui nimeongea nini tena, nilijificha kwanza,” anasema Suzy Bale ambaye ni mama wa watoto watatu.

YANGA YAMPA KIWANJA
Ule msemo ‘We Huogopi’ ambao Yanga walikuwa wakiutumuia kuhamasisha kwenye mechi zao za Ligi ya Mabingwa Afrika ulimpa kiwanja.
“Ile ni kama familia yangu tunakutana na kufurahi, mimi nimepewa ekari ya shamba na Yanga kule Kibamba na meneja wangu naye kapatiwa kimya kimya.
“Siku hiyo wananiambia nikachukue sikukawia, meneja alinipigia nikamwambia nimepata simu kwahiyo nachukua bodaboda haraka utanikuta Kibamba stendi, nashukuru Mungu.”
Kwa sasa Malkia wa Uswazi anasimamiwa na meneja Luay ambaye pia anamsimamia mtangazaji Sakina Lyoka na hapa anafunguka alikutana naye vipi.
HALALI NJAA
Unaweza kuchukulia poa Suzy anavyozungumza, lakini maneno yake na ucheshi wake vinamfanya apate maokoto pindi anapoongea na watu.
“Nisiwe mwongo, mtu akikunwa na maneno yangu basi ananiambia chukua hii elfu 10 utakunywa soda, hivyo yaani kwa hiyo muda mwingine unakuta sina hela lakini umetoka kufanya interview labda chombo fulani mtangazaji anakupa hela ya maji ni kawaida kwa mapenzi yake.
“Mungu amrehemu Dida alinipa elfu 10 baada ya kumaliza mahojiano, Juma Lokole nikampa maneno yake nashangaa wallet inachomolewa akanipa hela.”

ANASOMESHA
Suzy anasema kazi yake ya kuchekesha imemfanya kupata ada za shule za watoto wake watatu.
“Mwanangu wa kwanza amemaliza kidato cha nne mwaka jana na nashukuru amepata ‘Division One’ kiukweli kazi yangu inafanya nisomeshe na najivunia kwa hilo.”
BUKU NANE KWA SIKU
Anasema kwa siku pesa yake kubwa ya matumizi kuanzia kula na usafiri inagharimu Sh8,000 au ikizidi sana Sh20,000.
“Nikiwa na hela natumia 20,000 mimi sio mchoyo, hiyo hela natoa kwa watu pia, naweza kumnunulia mtu hata maji ili mradi nimetoa na najua itarudi.”

KIINGEREZA FRESHI
“Mimi nimesoma Green Bird Secondary ingawa sikufanikiwa kumaliza shule, nilipata nafasi hadi ya kwenda China miezi sita. Nakutana na watu wazito kama hutaki kuamini ni wewe tu. Sijasoma sana lakini natumia akili ya kuzaliwa. Mimi napenda kujifunza vitu tofauti.
“Kuna siku tulitoka na meneja wangu kwenda kula, nikamsikia dada mmoja kaagiza chakula ‘Chicken Chips’, nikajiongeza nikasema ‘Chips Chiken’ nikimaanisha niwekee viazi vingi maana nikaona nikimuiga yule dada ataona mimi sili sana.”
AWATOLEA UVIVU WASANII
Malkia wa Uswazi anasema wasanii wanapaswa kuishi maisha yao halisi ili likitokea tatizo waweze kusaidiwa kwa haraka.
“Hapa wasanii wanapaswa kuwa makini na kujifunza kwenye hili sakata la Nicole Joyberry, unasema una maisha, lakini unabaki kusota ndani (rumande). Ni jambo la aibu sana wewe una maisha mazuri ya kifahari, sasa mtu anakusaidia vipi.
“Kuna maisha ya kuigiza mitandaoni na halisi yaonyeshe ili watu wajue jinsi gani ya kukusaidia unapopatwa na matatizo, mimi maisha hayo naogopa hatari.”

Anasema nje na kuchekesha mitandaoni kazi hiyo inampa madili mbalimbali ya kuigiza likiwemo la msanii Chuchu Hansy.
“Sasa hivi nafanya vyote zile clip zangu na nashukuru zimenisaidia kupata madili ya kuigiza, Chuchu Hansy pia amenitafuta tufanye kazi.”

AKUTANA NA ISHA MASHAUZI
Kama isingekuwa kuchekesha na kuigiza anasema ingekuwa ngumu kwake kuwa maarufu mitandaoni na kukutana na wasanii mbalimbali.
“Kina Diamond nimewahi kukutana nao miaka ya nyuma kabla sijatoka na kujulikana wakati ule Kinondoni alikuwa anakuja kufanya shoo, nimeonana naye sana lakini sio kwa ukaribu,” anasema.
“Wasanii kama Isha Mashauzi waliwahi kuja mtaani kwetu kunifuata, watu wakashangaa kumuona hawakutegemea, kuna Phina ambaye alitumia hadi msemo wangu, hana shida yule dada.”
ALI KAMWE NAYE
“Hana shida nikukutana naye ananipatia hadi pesa ya soda, niliibiwa jezi yangu ya Yanga ambayo alinikabidhi, tulipokutana kwenye msiba nikamwambia kaka yangu jezi nimeibiwa alisema atanipatia nyingine, hana shida.”
PACOME, AZIZ KI
Msanii huyo ambaye pia ni shabiki wa Yanga anasema anawakubali karibu wachezaji wote wa Yanga lakini Pacome Zouzoua na Aziz KI wanamkosha zaidi.
“Kiukweli mimi nafuatilia sana timu yangu inapocheza, wachezaji wote nawakubali lakini Aziz KI na Pacome wale kiboko wananikosha sana.
“Jamani wamuache Aziz wana kazi ya kumuongelea maneno mabaya mbona mabao yake anayofunga hawasemi, Aziz mdogo wangu hana roho mbaya halafu ashakuwa Mtanzania (shemeji yetu).”
NENO KWA HAMISA
“Unajua hakuna mtu anapenda mwenzie akifanikiwa, mimi nampongeza Hamisa Mobetto. Kwa kufunga ndoa na Aziz Ki amewaziba midomo wambea. Namshauri apunguze marafiki feki ambao hawana msingi.”