Suzan Lyimo na kilio cha wazee kuachiwa wajukuu

Miaka ya hivi karibuni bibi na babu wamekuwa wakikwepa kuishi na wajukuu, huku baadhi ya sababu zikitajwa ni maisha kuwa magumu, lakini wenye watoto wao kushindwa kuwagharimia matumizi yao.

Jambo hili linaungwa mkono na Mwenyekiti wa Baraza la Wazee la Chadema (Bazecha), Susan Lyimo, ambaye hivi karibuni alifanya mahojiano na Mwananchi na kuzungumzia mambo mbalimbali kuhusu yanayowasibu wazee, ambapo pia aligusia suala la kusukumiwa wajukuu kuwalea.

 Suzan anasema mtu anapofika uzee inapaswa uwe ni muda wake wa kupumzika, lakini kwa hali ilivyo sasa watoto wamekuwa wakiwasukumia ulezi wa watoto wao ambao wamekuwa wakizaa, jambo ambalo sio sawa.

Mtazamo huo wa Suzan unakuja kukiwa na asilimia 30 ya watoto barani Afrika wanaokuwa chini ya malezi ya bibi na babu, kama inavyofafanuliwa katika ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Watoto (UNICEF) ya mwaka 2022.

 Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hali hiyo inachangiwa na sababu mbalimbali, ikiwemo vifo vya wazazi vinavyosababishwa na magonjwa, uhamiaji wa wazazi kutafuta ajira na changamoto za ndoa.

 Katika maelezo yake, Mwenyekiti huyo wa Bazecha anasema ifike mahali kijana awe wa kike au wa kiume anapoamua kufika hatua ya kuwa na mtoto ahakikishe anamlea mwenyewe.

“Hii ya wazazi kulea watoto wao wenyewe ina faida nyingi, ukiacha kuwapunguzia ugumu wa maisha wazee, lakini pia inakusaidia kuzisoma tabia za mtoto wako na pale unapoona kuna upungufu iwe rahisi kumrekebisha na kumlea katika malezi mema.

“Hivyo nawasihi wazazi kulea watoto wao wenyewe, siyo baadaye anakuja kuharibikiwa unaanza kumtupia baba au mama yako lawama kuwa alimlea vibaya,” anasema Suzan.

Faida nyingine za wazazi kulea watoto wao wenyewe, anasema itasaidia katika suala zima la ulinzi wao na hii ni kutokana na watu dunia ya sasa kuharibika.

Katika hili anasema wazazi wanapaswa kuelewa kuwa ulinzi wa mtoto unaanza na wewe mwenyewe, kwa kuwa kumekuwepo na matukio mengi dhidi ya ukatili kwa watoto, ikiwemo kubakwa, kulawitiwa, kupigwa ambayo yanahusisha ndugu wa karibu, wakiwemo babu.

“Tulipofikia dunia ya leo kila mtu akae na mtoto wake, na hata ikitokea ni kwenda kuwasalimia wazee basi uende nao au utafute mtu unayemuamini kuongozana naye.

“Wanapoamua kuzaa, wawe wamejiandaa kwa malezi, kwa kuwa hali inaonyesha kwamba wengi huwapeleka watoto kwa bibi na babu zao ili kuepuka gharama za malezi. Unampelekea mama au baba yako mtoto, halafu huna matumizi yoyote unayotuma, unataka huyu mzazi aishije na mtoto wako, mkitaka kuzaa hakikisheni mmejipanga na kulea na siyo kuwabebesha wazazi mzigo.

Wakati Suzan akieleza hayo, wapo wanaoamini kwamba wazee kupata nafasi ya kulea wajukuu ni msaada kwao na wengi wao wanapenda kushiriki kwenye jukumu la malezi ya wajukuu zao.

Walichosema wanasaikolojia wachumi

Wakizungumzia hoja hizo za Suzan, mchambuzi wa masuala ya Uchumi na Jamii, Oscar Mkude anasema watu kupeleka watoto kwa babu au bibi zao ni matokeo ya hali mbaya ya kiuchumi miongoni mwa watu.

“Wengi wanaofanya hivi kuwapeleka watoto kwa bibi zao ni wanaoishi mjini ambapo bado wanajitafuta na kwa kuwa mtoto anahitaji uangalizi wa karibu naye hela ya kuajiri mfanyakazi wa nyumbani hana, anaona njia rahisi ni kumpeleka mtoto akalelewe kwao,” anasema Mkude.

Anasema athari za maisha ya namna hii ni kwamba wazee sasa wamegeuka kuwa tegemezi la watoto wakati walipaswa wao ndio wawategemee watoto.

“Unakuta mtu kaenda mjini akidhani atapata ajira, mambo yanakuwa ndivyo sivyo kwa sababu zamani ilikuwa kama umesoma ajira njenje, tofauti na sasa watu wanazunguka na digrii zao mtaani na mkazo ukitiliwa kwenye kujiajiri na hapo ndio wengine wanajikuta wakiangukia kwenye ajira za ajabu ilimradi tu waweze kuyamudu maisha mjini.

Jingine anasema inawafanya wazee kutafuta vibarua vya kufanya ili kuweza kumlea mjukuu, jambo ambalo sio sahihi kwa kuwa anashindwa kufurahia uzee wake baada ya kumaliza majukumu ya kulea watoto ambao wanapaswa kujitegemea.

Athari nyingine kubwa anayoiona Mkude anasema siku za mbele watu wataogopa kuzaa kwa kuhofia wataleaje watoto na hivyo zile takwimu za uzalianaji kushuka ambazo zina athari si tu kiafya, bali pia kiuchumi.

 “Hilo la kutozaliana kwa wingi athari zake zimeanza kuonekana kwa nchi za Ulaya, ambapo imefika mahali wanatafuta hadi wafanyakazi kutoka nje ya nchi ambapo nao kwa sasa wameshtuka na kuona wafanyakazi hao wakizaliana huko, baadaye inaweza kuua asili ya taifa lao,” ameeleza mchambuzi huyo.

 Lakini pia imefika mahali mtoto akiwa mjini mzazi wala hataki kujua mtoto wake anafanya kazi gani na mwishowe kusababisha wengine kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya, kujiuza nk.

Mwanasaikolojia John Ambrose wa taasisi ya Bodymind Insight, anasema kuna athari za kisaikolojia ambazo mzee na mtoto wanaweza kuzipata.

Ambrose anazitaja athari hizo kuwa ni pamoja na bibi au babu kuumia wanaposhindwa kuwapa mahitaji ya kisasa ambayo mtoto alikuwa akilelewa na wazazi wake.

Jingine kushindwa kupata muda mzuri wa kupumzika na kutolea mfano wao wamezoea kulala saa mbili usiku, lakini wajukuu utakuta wanataka kuangalia TV mpaka saa sita usiku.

“Pia umri wa wazee hauhitaji kufanya kazi za kufikiria sana, hivyo unapomuachia mtoto amlee inamaana unampa mzigo wa kufikiria zaidi namna ya kumlea,” anasema mwanasaikolojia huyo.

Je, kuna sheria ya kuwabana wanaowapeleka watoto kwa wazee?

Mwananchi ilitaka kujua kama kuna sheria yoyote inayowabana wazee kutupiwa watoto kuwalea.

Kamishna Msaidizi Ustawi wa Jamii anayeshughulikia wazee kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Makundi Maalumu, Tullo Masanja, anasema hakuna sheria maalumu, isipokuwa mzee kama ataenda kushtaki katelekezewa mtoto itatumika ile sheria ya kumhudumia mtoto.

 Hata hivyo, anasema pamoja na kukosekana kwa sheria hiyo, Serikali inaendelea kusisitiza umuhimu wa wazazi kulea watoto wao kwa kuwa kadiri umri unavyoenda kwa mzee anapaswa kupunguziwa majukumu.

“Kisaikolojia mzee kashatoka katika umri wa kulea, naye sasa anatakiwa elelewe, kwa hiyo mnaokwenda kuwatupia watoto wenu wawalee muache hiyo tabia na ni vema muwapeleke tu kipindi cha likizo ambacho huwa na muda mfupi wa kukaa, lakini siyo kuwaachia moja kwa moja wawalee,” anasema Masanja.