
Dar es Salaam. Wakati baadhi ya watu wakiwekeza fedha kwenye kampuni za upatu, imeelezwa kuwa, ukuaji wa teknolojia unakuja na fursa nyingi, hivyo kuzijua halali na zisizo halali inachukua muda, huku wengine wakijikuta wanatapeliwa.
Akizungumzia hilo leo Jumatano Februari 26, 2025 mchumi Profesa Haji Semboja amesema, “tatizo kubwa hadi mtu kutapeliwa ni kutokana na elimu na ufahamu kuhusu huduma hii na kutoka ni ngumu, kwa kuwa teknolojia inakua kila siku, njia pekee ni kujiepusha ili kutokuwa muathirika.”
Hayo yanaelezwa zikiwa zimepita siku kadhaa tangu baadhi ya maofisa wa Kampuni ya Leo Beneath London (LBL) wakamatwe na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kuendesha biashara hiyo bila leseni.
Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), haijawahi kufanya mazungumzo wala kutoa leseni ya kuruhusu kampuni hiyo kufanya shughuli zake nchini.
Taarifa kwa umma iliyosainiwa na Gavana wa BoT, Emmanuel Tutuba Februari 24, 2025 inaeleza kuwa kwa sasa, hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi ya maofisa wa kampuni hiyo.
BoT inatoa taarifa hiyo wakati tayari watu 38 wamekamatwa kwa kujihusisha na kampuni hiyo katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Geita na Dar es Salaam.
Hata hivyo, baadhi ya waliowekeza fedha zao kwenye kampuni hiyo na kutarajia kuvuna wamekuwa na kauli tofauti.
Aron Kivuyo wa Arusha amesema aliwekeza kwenye kampuni hiyo sanjari na mkewe na watoto wake wawili zaidi ya Sh2 milioni kwa matarajio ya kupata faida ya Sh72,000 kwa siku kama walivyoambiwa.
“Kila mmoja aliwekeza Sh540,000 ambayo faida yake ilikuwa ni Sh18,000 kila siku kwa kutazama video 15 walizokuwa wakimtumia kila mmoja wetu, kila siku tuliingiza Sh18,000 kila mmoja isipokuwa Jumamosi na Jumapili.”
Kivuyo amesema, faida waliyokuwa wameingiza kwa wiki mbili (siku 10 za kazi) ni Sh180,000 kila mmoja.
“Wote tulikuwa tumeingiza 720,000 na pesa ambayo tuliwekeza wote wanne ni Sh2.16 milioni, tukiamini kampuni hiyo ni halali hadi tuliposhtuka pesa zao zimesitishwa.”
Amesema Februari 24 walitumiwa taarifa kwamba wanatakiwa kulipa kodi ya asilimia 50 kwenye pesa walizowekeza ili waweze kupata fedha zao.
“Meseji zilikuwa ni zao LBL wakituambia BoT inadai kodi kwenye pesa tulizowekeza hivyo ili tupate pesa zetu, tunatakiwa kulipa kodi ya asilimia 50 ya pesa tulizoziwekeza,” amesema.
Mkewe, Tumaini Kivuyo amesema hawajui hatima ya pesa zao, zaidi ya kuambiwa watume nyingine ili wapate pesa hizo.
Mwathirika mwingine, Jane Mahiga anadai aliwekeza Sh50,000 ambayo ndiyo ilikuwa pesa ndogo ya kuwekeza.
“Hii waliita P1, ambayo ukiwekeza ilikuwa unapata Sh3,500 kila siku kwa kuangalia movies 10 wanazokutumia kwa siku, sijavuna chochote naambiwa nilipe tena kodi ya BoT asilimia 50 ili niweze kupata pesa zangu nilizowekeza,” amesema Jane wa Pwani.
Upande mwingine unadai kuwa, kufungiwa kwa kampuni hiyo kumewaharibia ‘ajira’ yao iliyowaingizia kipato.
Shafii Shafii wa Dar es Salaam, amedai yeye ni mnufaika wa pesa za LBL tangu alipoanza kucheza Oktoba mwaka jana.
“Nilijiunga kwa Sh50,000 nikawa naigiza Sh3,500 kila siku kwa kuangalia movies 10 walizokuwa wakinitumia, baada ya mwezi mmoja, tayari nilirejesha pesa yangu nikawa napata ya kampuni.
“Kwa sisi tusiokuwa na ajira, hii ilikuwa ni kama ajira yetu, mimi nilikuwa napata pesa kila mwezi, kufungwa kwake kumeniathiri,” amesema Shafii ambaye ni mwanafunzi wa chuo.
Hata hivyo, Profesa Semboja akizungumzia athari za biashara haramu ya upatu mtandaoni, amesema yote yanatokea kutokana na ukuaji wa teknolojia na mawasiliano.
Ametolea mfano wa Deci ilivyolalamika kutapeli mamilioni ya pesa za watu waliowekeza.
“Hiki kinachoendelea ni mfumo uleule, mwanzoni mnapata, kisha mnahamasisha wengine kuingia, likishaingia kundi kubwa linapoteza,” amesema Profesa Semboja.
Akizungumzia kiini cha watu kutapeliwa kwa kucheza upatu haramu mitandaoni, amesema kuna mambo mengi nyuma yake.
“Siwezi kusema ni watu kutokuwa na kazi, maana tuna ardhi kubwa ya kilimo, kinachotokea ni ukuaji wa teknolojia tu, ambao unakuja na fursa mbalimbali, hivyo kuzijua zipi ni halali ni zipi sio halali inachukua muda na wengine kujikuta wametapeliwa,” amesema.
Amesema maendeleo ya teknolojia hadi kufikia hatua ya kufaidika au kaathirika yanategemea na akili ya mtu anavyoitumia fursa.