
Dar es Salaam. Siku moja baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kumsamehe kada wake wa zamani, Dk Wilbrod Slaa na kupokewa tena kwenye chama hicho, wadau wa siasa nchini wamekishauri kuwasamehe pia wabunge wake wa viti maalumu (Uviko-19) ili kukiimarisha chama.
Wadau hao wamesema falsafa za 4R za Rais Samia Suluhu Hassan hasa ile ya maridhiano, siyo kwa ajili yake pekee, bali inatakiwa kutekelezwa na makundi mbalimbali katika jamii hasa vyama vya siasa.
Falsafa nyingine ni Ustahamilivu, Mageuzi na Kujenga upya Taifa.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanaeleza kuwa, mazingira waliyoondoka wabunge hao ni tofauti na Dk Slaa kwa kuwa walifukuzwa uanachama wakati Dk Slaa hakufukuzwa, hivyo mazingira ni tofauti.
Hata hivyo, duru za ndani ya chama hicho zinaeleza kuwa, baadhi yao wameandika barua kwa viongozi wao wakitaka kurejea kwenye chama.
Gazeti la Mwananchi limezungumza na mmoja wa wabunge hao ambaye amekiri kuandika barua kama viongozi wa chama walivyoelekeza siku za nyuma.
Wabunge hao 19 wa viti maalumu kupitia Chadema, waliingia kwenye mgogoro na chama chao baada ya uchaguzi wa mwaka 2020 wakati chama chao kikiwa kimegoma kuyatambua matokeo ya uchaguzi huo.
Viongozi wa Chadema walikana kuwasilisha orodha ya majina ya wabunge wake kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi huku wakiweka msimamo wa kutopeleka majina hayo, hata hivyo walishangazwa kuona makada hao wakiapishwa bungeni bila kuwa na taarifa.
Wabunge hao waliapishwa Novemba 24, 2020 na Spika wa Bunge wa wakati huo, Job Ndugai katika Viwanja vya Bunge, jambo lililoibua mjadala mpana huku wakiingia kwenye mgogoro na Chadema hadi walipovuliwa uanachama.
Wabunge hao ni aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), Halima Mdee na waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko pamoja na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.
Wengine ni Hawa Mwaifunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Agnesta Lambat, aliyekuwa Katibu Mwenezi, Asia Mohamed aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha Zanzibar na Katibu Mkuu wa Bawacha-Bara, Jesca Kishoa.
Wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Mtwara, Tunza Malapo.
Makada wengine ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.
Msamaha kwa wabunge 19
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Machi 24, 2025 Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Richard Mbunda amesema kama Chadema imemsamehe Dk Slaa, haina sababu ya kutofanya hivyo kwa wabunge wake 19.
Hata hivyo, amesema ni sahihi kwa Chadema kumsamehe Dk Slaa kwa kuwa bado ana ushawishi na uwezo wa kusaidia kukijenga chama hicho.
Amesema wengine wanamtazama kama msaliti kwa kuwa alikikimbia chama kikiwa vitani hasa nyakati ambazo kilikaribia kushinda uchaguzi wa mwaka 2015.
“Alikimbia akakiacha chama kikiwa vitani katika muda critical (mgumu) lakini wamemsamehe na kumrudisha,” amesema.
Dk Mbunda amesema kama chama hicho kimemsamehe Dk Slaa aliyeondoka na kula matunda nje, haoni sababu kina Mdee na wenzake wasisamehewe.
“Hakuna dhambi kama unaweza kumrudisha Dk Slaa aliyekiacha chama, akaenda kula matunda nje, utashindwaje kwa hawa ambao mara zote pamoja na kufukuzwa wamekuwa wakihubiri kuwa wao ni wanaChadema,” amesema.
Amesema kwa hatua hiyo, chama hicho kinapaswa kutengeneza maridhiano ya ndani, kinyume na hivyo kitakuwa na nafasi finyu katika chaguzi zijazo.
4R za Rais Samia zatajwa
Mkuu wa Chuo kikuu cha Zanzibar (Suza), Profesa Mohammed Makame amesema misingi na usimamizi wa chama na nidhamu, huwa vinajengwa na katiba ya chama na kanuni zake.
Profesa Makame amesema chama kumsamehe mwanachama kunategemea na makosa ambayo amefanya na mamlaka husika kusikiliza mashauri na kutoa uamuzi.
“Ukiagalia mlolongo mzima hadi kufukuzwa, hawa wabunge wanaamini walichokifanya ni sahihi na walikuwa wakitimiza wajibu wao, ndiyo sababu hawakurudi nyuma kwa kuwa, hawakuona kama kuna sababu hiyo, chama ndicho kiliwakataa,” amesema Profesa Makame.
Amesema kuwasamehe ni sahihi, kama Chadema itaamua hivyo, akigusia 4R za Rais Samia ambazo hazipaswi kubaki kwa Rais pekee.
“4R zinapaswa kutumika kwenye maeneo yote ili kudumisha umoja na ushirikiano, kipindi hiki cha uchaguzi, maridhiano ni jambo jema na kila chama kipo kujipanga kutengeneza uimara wa chama.
“Kama Chadema ikiona inafaa kuendelea na timu iliyokuwa nayo hapo kabla ni sahihi, wanachama wakisema waangalie upande mwingine ni sawa, kwani wao ndiyo wana uhuru,” amesema Profesa Makame.
‘Ni vigumu kuwasamehe’
Mhadhiri wa UDSM, Sabatho Nyamsenda amesema ni vigumu kuwasamehe wabunge hao kwa sababu hawajawa tayari kupoteza ubunge wao, pia, mazingira waliyoondoka ni tofauti na ya Dk Slaa.
“Hawa wabunge 19 bado wanashikilia nafasi, hawajataka kupoteza hiyo privilege (upendeleo), kuwasamehe na kuwarejesha kama ilivyokuwa kwa Dk Slaa ni vigumu kulingana na mazingira walivyoondoka,” amesema Nyamsenda.
Mwanazuoni huyo amesema Dk Slaa hakufukuzwa, alijiondoa mwenyewe baada ya kutokubaliana na chama chake kumsimamisha Edward Lowassa kwa nafasi ya mgombea urais, kwa kuwa alikuwa akimtuhumu kwenye majukwaa kwa ufisadi.
“Alivyoondoka Slaa ni tofauti na hawa wabunge 19, Slaa amerudi akiwa amelipa gharama kutokana na harakati alizozifanya, akavuliwa ubalozi, alifunguliwa kesi mara kadhaa tofauti na mazingira ya wabunge 19, hadi sasa wapo bungeni kama wabunge wa Chadema.
“Uwepo wao kwa mujibu wa Chadema wapo kwa kufoji, Chadema ilisema haikuwapitisha, nilimsikiliza Lissu (Tundu, mwenyekiti wa Chadema) akisema aliyefukuzwa ni tofauti na aliyeondoka,” amesema Nyamsenda.
Baadhi waomba kurejea Chadema
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika Februari 23, 2025, Lissu alitaja masharti ya wabunge hao kurejea Chadema ikiwamo kuomba msamaha kwenye kikao kilichowavua uanachama.
Alisema mahali pa kuanzia wakitaka kurudi sio kwa mwenyekiti, ni kwenye Baraza Kuu, tena kwa kuandika barua ya kuomba kurudishiwa uanachama kwa Katibu Mkuu ambaye katika ajenda za Baraza Kuu ataweka na hiyo kama ajenda na baraza litajadili.
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa, baadhi ya wabunge hao tayari wameandika barua za kuomba msamaha ili kurejeshewa uanachama wao.
Miongoni mwa wanaodaiwa kuandika barua ni Anatropia Theonest na Sophia Mwakagenda.
Mwananchi imezungumza na Anatropia ambaye amethibitisha kuandika barua ya kwenda Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema tangu mwezi uliopita.
Kuna watu wameandika barua kuomba kurejeshewa uanachama, mmoja wao ni Anatropia.
“Nilituma toka Februari 17, 2025 na Katibu Mkuu (John Mnyika) amekiri ameipokea,” alisema Anatropia, aliyewahi kuwania ubunge Jimbo la Kyerwa mwaka 2020.
Mbunge huyo alisema: “Nasubiria majibu na vikao vinahusika katika mchakato huu.”
Hata hivyo, alipotafutwa Katibu Mkuu, John Mnyika kwa njia ya simu kuulizwa kama amepokea barua za wabunge hao wakiomba kurejea Chadema, alidai yuko safarini, hivyo atumiwe ujumbe. Hata alipotumiwa ujumbe huo, hakujibu chochote.
Imeandikwa na Imani Makongoro, Bakari Kiango na Juma Issihaka