SUPER SUB: Nyota wanaoweza kubadili mchezo wa dabi

JOTO la mpambano wa kusisimua wa Dabi ya Kariakoo, kati ya Yanga dhidi ya Simba linaendelea kupamba moto kwa mashabiki wakati wakihesabu siku mbili kabla ya mchezo unaopigwa keshokutwa, Jumamosi hii, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.

Mchezo huo huenda ukatoa taswira ya vita ya ubingwa msimu huu kutokana na pengo la pointi lililopo baina yao, japo Yanga inaingia ikiwa na rekodi nzuri baada ya mchezo wa kwanza kushinda kwa bao 1-0 likiwa ni la kujifunga la Kelvin Kijili Oktoba 19, 2024.

Timu zote zinaingia zikiwa na matokeo mazuri katika michezo ya mwisho ambapo Yanga iliifunga Pamba Jiji mabao 3-0 kwenye Uwanja wa CCM Kirumba – Mwanza, sawa na Simba iliyoifumua Coastal Union pia 3-0 katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Wakati pambano hilo la 114 kwa timu hizo kukutana tangu 1965 likisubiriwa, Mwanaspoti linakuletea nyota ambao wanaweza kubadilisha mchezo wakitokea benchi kutokana na viwango ambavyo wamekuwa wakivionyesha.

STEVEN MUKWALA (SIMBA)

Raia huyo wa Uganda alianza vizuri maisha yake ndani ya Simba, lakini alijikuta akikosa nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara ya mara nyuma ya mshambuliaji mwenzake, Leonel Ateba anayeaminiwa zaidi na kocha Fadlu Davids.

Licha ya kuanzia benchi mara kwa mara, ila mchezo uliopita dhidi ya Coastal Union aliotupia hat-trick katika ushindi wa timu hiyo wa mabao 3-0, huenda ukamfikirisha Fadlu na kumuanzisha au ikawa silaha yake akitokea benchi.

Akiwa na kikosi hicho katika Ligi Kuu amefunga mabao manane na kuasisti mara mbili, ikiwa ni idadi sawa na nyota mwenzake, Ateba wakizidiwa na Jean Ahoua (Simba), Prince Dube na Clement Mzize (Yanga) wenye 10 katika msimamo wa wafungaji Bara.

Nyota huyo ametua Simba huku akikumbukwa zaidi msimu uliopita ambapo alifunga mabao 14 akiwa na kikosi cha Asante Kotoko ya Ghana nyuma ya kinara mshambuliaji wa Berekum Chelsea, Stephen Amankonah aliyefunga 16. Pia alikuwa mchezaji bora wa Ligi Kuu Ghana Desemba 2023 akiwa na Asante Kotoko aliyojiunga nayo Agosti 2022 akitokea URA ya kwao Uganda, na katika msimu wake wa kwanza alifunga mabao 11 na kuasisti matano.

Akiwa URA, Mukwala alicheza kwa misimu mitatu kuanzia 2020 ambapo ule wa kwanza 2019-2020 aliibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu Uganda akifunga mabao 13 na 2020-2021 akafunga 14 kisha 2021-2022 akatupia kambani 13.

CLATOUS CHAMA (YANGA)

Chama aliyeichezea Simba kwa mafanikio kabla ya msimu huu kujiunga na Yanga, hapati nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosi cha kwanza kutokana na nyota wengine kama Pacome Zouzoua, ingawa ni mchezaji anayeweza kubadilisha mchezo.

Yanga iliyofundishwa na makocha watatu msimu huu akianza Miguel Gamondi, Sead Ramovic na Miloud Hamdi, lakini Chama ameshindwa kupenya mbele ya wote, ingawa amefunga mabao matatu katika Ligi Kuu Bara na kutoa asisti mbili.

Ubora wake hauhitaji maelezo kwani hata mchezo wa Februari 23, mwaka huu dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma alitokea benchi na kufunga mabao mawili yaliyoipa ushindi mnono Yanga wa mabao 5-0.

DEBORA FERNANDES (SIMBA)

Denora aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Mutondo Stars ya Zambia alianza vizuri Msimbazi, lakini ghafla upepo umebadilika na kushindwa kupenya kikosi cha kwanza mbele ya viungo wenzake, Fabrice Ngoma na Yusuph Kagoma.

Kwa sasa Debora sio mchezaji anayefikiriwa tena kikosi cha kwanza kutokana na ubora ambao Ngoma na Kagoma wanaendelea kuuonyesha, ingawa ni mkali hata akitokea benchi kwani anaweza kuleta tofauti na msimu huu kafunga bao moja la Ligi Kuu.

JONATHAN IKANGALOMBO (YANGA)

Mashabiki wa Yanga watakuwa na hamu ya kuendelea kumuona winga mpya, Jonathan Ikangalombo baada ya kuanza kukitumikia kikosi hicho katika mchezo uliopita wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Pamba Jiji uliopigwa Februari 28.

Ikangalombo maarufu kama Ikanga Speed aliyesajiliwa dirisha dogo la Januari, mwaka huu, akitokea AS Vita ya kwao DR Congo alicheza dakika 21 za mwisho wa mchezo huo na kuonyesha kiwango bora jambo linalosubiriwa kuona akiendeleza.

LADACK CHASAMBI (SIMBA)

Chasambi ni miongoni mwa nyota wa Simba wanaoweza kutokea benchi na kuleta tofauti katika mchezo kutokana na uwezo wa kufunga mabao na kuchangia upatikanaji wa mabao kwa wengine, huku namba zake zikiendelea kumbeba kikosini.

Msimu huu pekee katika Ligi Kuu Bara amehusika katika mabao matano baada ya kufunga moja na kuasisti manne, jambo linaloonyesha anaweza kubadilisha mchezo akitokea benchi kutokana na kutokuwa na uhakika zaidi wa kuanza.

MAXI NZENGELI (YANGA)

Huenda ukashangaa Maxi Nzengeli kuanzia benchi, lakini sio mara ya kwanza na inategemea namna kocha anavyotaka kumtumia kutokana na aina ya mfumo anaotaka kuutumia au kwa kuangalia ubora wa mpinzani anayecheza naye siku husika.

Nzengeli anayeweza kucheza eneo kubwa la uwanja mara nyingine huanzia benchi na hilo limetokea mara nyingi, huku kwenye michezo ya hivi karibuni likitokea Februari 23 katika mchezo dhidi ya Mashujaa ambao Yanga ilishinda mabao 5-0.

Hadi sasa nyota huyo amekuwa mhimili mkubwa na hucheza mara kwa mara kutokana na uwezo anaouonyesha kikosini, ambapo msimu huu pekee katika ligi amehusika na mabao 11 baada ya kufunga manne na kuasisti mengine saba.

VALENTINO MASHAKA (SIMBA)

Valentino aliyejiunga na Simba msimu huu akitokea Geita Gold amekosa nafasi ya kupenya kikosi cha kwanza mbele ya nyota wenzake, Ateba na Mukwala wanaofanya vizuri zaidi, ingawa kila akicheza anaonyesha kiwango bora. Msimu huu amefunga mabao mawili katika Ligi Kuu Bara, huku akionyesha kiwango bora wakati akiichezea timu ya vijana ya Tanzania (U-20) iliyokuwa inawania tiketi ya kufuzu fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon kupitia ukanda wa Cecafa.

PACOME ZOUZOUA (YANGA)

Kama ilivyokuwa kwa Maxi Nzengeli ndivyo ilivyo pia kwa Pacome, kwani ni mchezaji wa kikosi cha kwanza, ingawa kuna muda anaanzia benchi, lakini ikitegemea na jinsi Kocha Miloud Hamdi atakavyoingia na mbinu zake juu ya mchezo huo wa watani.

Nyota huyo hata akianza au akitokea benchi ni miongoni mwa viungo wanaoipa jeuri Yanga wakati mchezo huo ukisubiriwa na hii ni kutokana na namba nzuri alizonazo, ambapo hadi sasa amefunga mabao saba ya Ligi Kuu na kutoa asisti mara sita.

Uwepo wa Pacome, Clatous Chama, Stephane Aziz KI, Mudathir Yahya na Maxi Nzengeli unaifanya timu hiyo kuwa na ubora wa viungo wanaotishia mpinzani yeyote, hivyo kazi itabaki kwa benchi la ufundi kuamua yupi aanze au atokee benchi.

KENNEDY MUSONDA (YANGA)

Licha ya Musonda kukosa nafasi ya kucheza kutokana na ubora wa washambuliaji wengine kama Prince Dube na Clement Mzize wanaoongoza wakiwa na mabao 10 Ligi Kuu hadi sasa, lakini ni mshambuliaji hatari anayeweza kutokea benchi na kubadilisha  mchezo.

Musonda ni mshambuliaji mzoefu na anakumbukwa katika dabi ya Novemba 5, 2023 alipoifungia Yanga bao la mapema dakika ya 3 wakati kikosi hicho chenye maskani mitaa ya Twiga na Jangwani kikiwafumua watani zao Simba kwa mabao 5-1.

Raia huyo wa Zambia ni miongoni mwa washambuliaji bora na licha ya kutopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara,  msimu huu amefunga mabao matatu Ligi Kuu Bara, huku akisaidia upatikanaji wa lingine moja. Hata hivyo, licha ya rekodi nzuri kwa mastaa hao ambao wamekuwa wakionyesha iwe wanaanzia au kutokea benchi, lakini dabi siku zote ni mchezo unaotoa taswira tofauti, kwani huenda ikatokea tu mchezaji asiyetegemewa akaibuka na kufanya vizuri.