Suluhisho takwimu sahihi za maji ardhini lapatikana

Dodoma. Wizara ya Maji imenunua vifaa vya kisasa vya kuchunguza miamba inayohifadhi maji katika kina kirefu, hatua ambayo itaondoa changamoto ya kutopatikana kwa takwimu sahihi zinazohusu kiasi na ubora wa maji.

Vifaa vilivyonunuliwa ni tisa vya kuchunguza mipasuko kwenye matabaka ya miamba kwa njia ya nguvu ya sumaku (Magnetometer) na vifaa vinavyotumika kuchunguza uwepo wa maji kwenye matabaka ya miamba kwa kutumia njia ya umeme (Terrameter).

Vingine ni vifaa tisa vya kupima kina cha maji kwenye visima virefu (Deeper) na vifaa vinavyotumika kuchunguza mikondo ya maji, aina ya matabaka ya miamba kwa ajili ya kudebuni na kujenga kisima (borehole logger).

Kifaa kingine kilichonunuliwa ni kinachotumika  kufanya mawasiliano wakati wa utafiti wa wataalamu Accessories (GPS na Walk talkie).

Vifaa hivyo vya kisasa vya utafiti wa maji chini ya ardhi  vimenunuliwa kupitia fedha za Uviko-19 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani ambapo Sh5.2 bilioni zimetumika kununua vifaa hivyo.

Akizungumza wakati akiwakabidhi wakurugenzi wa mabonde vifaa hivyo leo Mei 9, 2025, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema kuna rasilimali za maji chini ya ardhi zenye mita za ujazo bilioni 21 lakini bado hazijanufaisha Watanzania.

Amesema raslimali hizo bado hazijanufaisha Watanzania kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kukosekana kwa vifaa vya kisasa na umakini wa wataalamu.

Ametoa mfano wa taarifa ambazo hazikuwa sahihi alizozipata kutoka kwa wataalamu wake juu ya kutokuwepo kwa maji chini ya ardhi katika eneo la Kilindi mkoani Tanga na Liwale mkoani Lindi lakini walipopeleka timu nyingine maji yalipatikana.

 “Sasa kwa kuletewa vifaa hivi vya kisasa maana yake ni kwamba Wizara ya Maji sasa haina kisingizio. Tumepata vifaa vya kisasa vitakavyotueleza ili uyapate maji unatakiwa kwenda kilometa ngapi ardhini,”amesema.

Amewataka wakurugenzi wote wa mabondeya maji  kuvitumia vifaa hivyo katika shughuli iliyokusudiwa ili Watanzania waone manufaa ya jitihada zinazofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan za kumtua mama ndoo kichwani

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mwajuma Waziri amesema japokuwa hawajafikia teknolojia zilizopo duniani lakini kupitia vifaa hivyo wataalamu watakwenda kufanya utafiti utakaoleta matokeo.

“Kupitia vifaa hivi tutaendelea kuwamantor (kuwatamia) wataalamu wetu. Kuna wataalamu waliokwenda nchini China wamerudi kwa hiyo, tunategemea vifaa hivi vitakwenda kutumika ipasavyo,”amesema.

Mwajuma amesema pia wataendelea kuwajengea watalaamu uwezo wa kutosha ili vifaa hivyo viweze kutoa matokeo yanayotarajiwa.

Awali, Mkurugenzi wa Rasilimali za Maji ya Wizara ya Maji, Dk George Lugomela amesema vifaa hivyo vina uwezo wa kuchunguza miamba inayohifadhi maji kwa ufanisi hadi kina cha urefu wa mita 1,000.

“Jumla ya mabonde nane yatapata vifaa hivi nayo ni ya Tanganyika, Victoria, Wami-Ruvu, Rukwa, Ruvuma, Rufiji na Bonde la Kati) ambayo yatapata mgawo wa kifaa kimoja kimoja,”amesema.

Naye Mkurugenzi wa Bonde la Ruvuma na Pwani ya Kusini, Jumanne Mpemba amesema awali walikuwa wakishindwa kupata takwimu za miamba kwa sababu ya kukosekana kwa vifaa vya kisasa.

“Kwa vyombo hivi tunakwenda kufanya mageuzi mapya ya kupata takwimu ya miamba chini ya ardhi…Awali ilikuwa ni vigumu kupata kiasi cha maji yaliyopo chini ya ardhi na mwamba unahimili kiasi gani,”amesema.

Aidha, amesema kwa kutumia vifaa hivyo watawezesha kujua ubora wa maji, kiasi cha chumvi na asidi iliyopo katika maji kabla ya uchimbaji wa kisima.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *