
Shambulio dhidi ya msafara wa magari ya misaada ya kibinadamu limesababisha vifo vya watu watano. lilitokea jioni ya Juni 2 karibu na mji wa El Fasher, katika jimbo la Darfur Kaskazini. Msafara huo ulitakiwa kupeleka msaada katika mji huo, ambao unazingirwa na kundi la wanamgambo wa Rapid Support Forces, uliposhambuliwa.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Msafara huo ulikuwa umejumuisha takriban malori kumi na tano kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani ,WFP, na UNICEF. Magari hayo yalikuwa yanasheheni msaada wa chakula na madawa kutoka Port Sudan na yalikuwa yameegeshwa katika mji wa Al Koma, yakisubiri idhini ya kusafiri hadi El Fasher, umbali wa kilomita 80, katika jimbo la Darfur, kusini magharibi mwa Sudani, yaliposhambuliwa.
Taarifa za awali zinataja watu watano miongoni mwa watu waliokuwa katika msafara wamagari hayo waliuawa, wengine kadhaa kujeruhiwa, na malori kadhaa kuharibiwa pamoja na mizigo yao. Pande zote mbili zinazopigana zinakanusha kuwa zilihusika na shambulio hilo baya. Wanamgambo wa RSF wa serikali wanadai msafara huo ulishambuliwa kimakusudi na jeshi. Jeshi, kwa upande wake, linashutumu Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) kwa kushambulia kwa kutumia ndege zisizo na rubani.
Msemaji wa UNICEF alijibu siku ya Jumanne, Juni 3. Kulingana na Eva Hinds, “malori hayo yaliwekuwa na Nembo ya mashirika ya Umoja wa Mataifa. Shambulio lolote dhidi ya msafara wa kibinadamu halikubaliki,” amesema. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ametoa wito wa “uchunguzi wa haraka,” akiongeza kuwa hawezi kubaini waliohusika na shambulio hilo la anga katika hatua hii.
Msafara wa takriban malori kumi na tano ulikuwa ukijaribu kuwafikia watoto na familia katika mji uliokumbwa na njaa wa El Fasher.