
Zaidi ya watu 200 wameuawa katika muda wa siku tatu katika mashambulizi ya wanamgambo kwenye vijiji viwili kusini mwa Khartoum, kundi la wanasheria wanaounga mkono demokrasia limesema siku ya Jumanne, huku wizara ya mambo ya nje ikitangaza idadi ya waliouawa kuwa mara mbili ya kiwango hicho.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Wizara ya Mambo ya Nje imesema mashambulizi ya Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) yamesababisha “mauaji ya watu 433, wakiwemo watoto wachanga”, na kulaani “mauaji ya kutisha”. Mashambulizi ya RSF katika Jimbo la White Nile kwenye vijiji vya Al-Kadaris na Al-Khelwat, yapata kilomita 90 kusini mwa mji mkuu Khartoum, yamewalazimu maelfu ya wakaazi kukimbia, mashahidi wameliambia shirika la habari la AFP. Tangu Jumamosi, RSF imefanya “mauaji, utekaji nyara, watu kutoweka na uporaji wa mali” dhidi ya raia wasio na silaha, kulingana na muungano wa wanasheria wanaoandika kumbukumbu za ukiukaji wa haki za binadamu tangu kuanza kwa vita.
Shambulio hilo, ambalo kundi hilo lilieleza kuwa ni “mauaji ya halaiki”, limesema mamia ya watu wamejeruhiwa na kutoweka, likiongeza kuwa baadhi ya wakazi walipigwa risasi au kufa maji walipokuwa wakijaribu kukimbia kuvuka mto Nile. Tangu vita vilipoanza Aprili mwezi 2023, jeshi na wanamgambo wameshutumiwa kwa uhalifu wa kivita. RSF, ambayo Marekani ilishutumu kwa mauaji ya kimbari mwezi Januari, inajulikana kwa mauaji ya kikatili, utakaso wa kikabila na unyanyasaji wa kijinsia. Vita hivyo vimesababisha vifo vya makumi ya maelfu, na kusababisha zaidi ya watu milioni 12 kuyahama makazi yao na kuunda kile ambacho Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji inakiita “mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu kuwahi kurekodiwa.”
Mapigano kati ya jeshi na wanamgambo yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, huku jeshi likijaribu kurejesha udhibiti kamili wa Khartoum kutoka kwa mikononi mwa RSF.Siku ya Jumapili UNICEF, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, lilionya kuhusu hali ya raia walionaswa katika “jinamizi la mauaji” ndani na karibu na mji mkuu. Lilitoa shahidi za kutisha za familia zilizotengana, watoto waliotoweka, waliowekwa kizuizini au kutekwa nyara, na unyanyasaji wa kijinsia. Siku ya Jumanne Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa alishutumu “kutokujali” kunakochochea ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu.
“Mashambulizi yanayoendelea na ya makusudi” dhidi ya raia, ikiwa ni pamoja na “mauaji ya kikatili, unyanyasaji wa kijinsia na ukiukwaji mwingine na unyanyasaji,akibainisha kushindwa kabisa” kwa pande zote mbili kuheshimu sheria ya kimataifa ya kibinadamu, alisema katika taarifa yake. Umoja wa Mataifa pia ulitoa wito wa kupanuliwa kwa mamlaka ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu na kurefushwa kwa vikwazo vya silaha – vinavyotumika tangu mwaka 2004 – kwa Sudani nzima, na sio tu kwa eneo kubwa la Darfur (magharibi).
Darfur, ambayo ni makazi ya karibu robo ya wakazi wa Sudani, imeshuhudia kuongezeka kwa ghasia katika wiki za hivi karibuni wakati RSF ikitaka kuimarisha udhibiti wake katika eneo hilo. Umoja wa Mataifa unasema maelfu ya familia zimekimbia mashambulizi ya RSF kwenye vijiji karibu na Al-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini na mji pekee mkubwa katika eneo hilo nje ya udhibiti wake. RSF ilianzisha mashambulizi makali wiki iliyopita kwenye kambi ya wakimbizi ya Zamzam iliyozingirwa na iliyokumbwa na njaa karibu na Al-Facher.