Sudani: Mashambulio ya wanamgambo yaua sita Darfur Kaskazini

Mashambulizi ya mizinga katika soko lililojaa watu wengi na kambi ya watu waliokimbia makazi yao katika jimbo la Darfur nchini Sudani yameua watu sita siku ya Jumapili, wafanyakazi wa kujitolea wa afya wamesema.

Imechapishwa:

Dakika 1

Matangazo ya kibiashara

Kambi hiyo ya Abu Shouk, iko pembezoni mwa mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini, El-Fasher, ambayo Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vimekuwa vikizingira tangu mwezi Mei mwaka jana kama sehemu ya vita vya karibu miaka miwili dhidi ya jeshi la Sudani.

Mashambulio ya mabomu “yamesababisha vifo vya raia sita wasio na silaha hadi sasa, na majeruhi zaidi bado hawajaripotiwa,” limesema kundi la kukabiliana na dharura la eneo hilo, moja ya mamia ya makundi ya kujitolea kote Sudani, iliyokumbwa na vita, yayosaidia kuwahamisha waliojeruhiwa, kusaidia wafanyikazi wa afya na kudumisha huduma za afya.

“Shambulio hili… lililenga soko lililojaa watu wakati raia walikuwa wakinunua bidhaa muhimu kwa ajili ya mfungo wa mweziwa Ramadan,” kundi hilo limeongeza, likilaumu RSF.

Mfungo wa mwezi wa Ramadhani, ulioanza nchini Sudani siku ya Jumamosi, unakuja wakati nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika ikiendelea kukabiliwa na vita, njaa na kuhama kwa watu.

Mnamo mwezi Disemba, tathmini iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa ilisema njaa ilikuwa imetanda katika Abu Shouk na kambi nyingine mbili katika eneo la El-Fasher, Al-Salam na Zamzam, na inatarajiwa kuenea katika maeneo mengine matano, ikiwa ni pamoja na mji wenyewe, ifikapo mwezi Mei.

RSF wamechukua udhibiti wa karibu eneo lote kubwa la magharibi la Darfur.

Hata hivyo, walishindwa kuchukua udhibiti wa El-Fasher, ambapo jeshi na vikosi washirika viliwarudisha nyuma mara kadhaa.

Vita nchini Sudani hadi sasa vimeua makumi ya maelfu ya watu, kuwahamisha watu zaidi ya milioni 12 na kuleta mamilioni ya wengine kwenye ukingo wa njaa kubwa.

Siku ya Jumatano, Shirika la Mpango wa Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilisema kuwa mapigano makali katika kambi ya Zamzam yamelilazimisha “kusimamisha kwa muda ugawaji wa chakula cha kuokoa maisha na msaada wa lishe” katika kambi hiyo.