
Ziara ya Rais wa Uganda Yoweri Museveni nchini Sudani Kusini ilimalizika Ijumaa. Ziara ambayo Mkuu wa Nchi alikutana na mwenzake Salva Kiir na wadau wengine wa kisiasa wa Sudani Kusini pamoja na kundi la wazee wa busara wa Umoja wa Afrika. Museveni ameondoka Juba bila kukutana na Riek Machar. Wasiwasi kuhusu kurejea kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe unaendelea, hasa kwa vile Museveni, mshirika wa Salva Kiir, amethibitisha kumuunga mkono kikamilifu.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Juba, Florence Miettaux
Magari ya kivita na maelfu ya wanajeshi wa Uganda walilinda uwanja wa ndege na barabara za kimkakati mjini Juba wakati wa ziara ya Yoweri Museveni mjini Juba, mji mkuu wa Sudani Kusini. Kwa mara ya kwanza, wakaazi wamefahamu uwepo wa wanajeshi wa Uganda nchini Sudani Kusini wakimuunga mkono Salva Kiir. Uwepo unaoongeza hofu ya kuongezeka kwa mzozo.
Yoweri Museveni ni mmoja wa wadhamini wa mkataba wa amani wa mwaka 2018, uliotiwa saini hasa na Salva Kiir na mpinzani wake Riek Machar. Katika ziara hii, alikutana na mwenzake Salva Kiir na wadau wengine wa kisiasa wa Sudani Kusini pamoja na kundi la wazee wa busara wa Umoja wa Afrika. Lakini rais wa Uganda inaonekana hakuona vyema kukutana na Makamu wa Rais Riek Machar, ambaye bado yuko chini ya kifungo cha nyumbani licha ya wito mwingi wa kuachiliwa kwake na kurejeshwa kwa mazungumzo ili kutatua mgogoro huo.
Maelezo machache yametolewa kuhusu maudhui ya majadiliano kati ya Yoweri Museveni na watu hao waliokutana. Uwepo wa wawakilishi wa chama cha Riek Machar katika mkutano na wanasiasa wa Sudan, ambao umetajwa na ofisi rais wa Sudani Kusini kwenye Facebook, unapingwa. Akiwasiliana na RFI, msemaji wa chama cha makamu wa rais, amesema kuwa “hakuna mwanachama wake aliyeruhusiwa kukutana na Yoweri Museveni.”
Kwa upande wake, kundi la wazee wa busara wa Umoja wa Afrika kimeendelea na mashauriano yake siku ya Jumamosi kwa siku yao ya mwisho ya ujumbe huko Juba. Wanatarajiwa kujaribu mkutano mwingine na Makamu wa Rais Riek Machar, mkutano ambao hadi sasa haujaidhinishwa na serikali ya Sudani Kusini.