Sudani Kusini ‘katika ukingo wa vita’ kulingana na kambi ya kikanda IGAD

Mvutano wa hivi majuzi nchini Sudani Kusini unaisukuma nchi hiyo maskini na isiyo na utulivu “karibu zaidi na ukingo wa vita,” Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Pembe ya Afrika, IGAD imeonya siku ya Jumatano.

Imechapishwa:

Dakika 2

Matangazo ya kibiashara

Mapigano mapya kaskazini mashariki yanatishia amani nchini Sudani Kusini, inasema IGAD. Wiki iliyopita, helikopta ya Umoja wa Mataifa iliyokuwa ikifanya kazi ya uokoaji kwa wanajeshi wa Sudani Kusini ililengwa kwa shambulio na kumuua mfanyakazi mmoja na jenerali wa Sudani Kusini. Watu kadhaa wa karibu na Makamu wa Rais Machar pia walikamatwa.

Mnamo Machi 4, “takriban wapiganaji 6,000 kutoka White Army,” kundi lenye silaha linalojumuisha vijana kutoka kabila la Nuer la Makamu wa Rais Riek Machar, lilichukua udhibiti wa kambi ya jeshi la Sudani Kusini, inabainisha IGAD, kundi linalojumuisha Djibouti, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Uganda, Somalia, Sudani na Sudani Kusini. Wakati Rais Kiir alisema wiki iliyopita kwamba nchi yake haitakumbwa tena na machafuko, IGAD inabaini kwamba “msururu wa matukio na ghasia za mzunguko zinaweka shinikizo kubwa kwa makubaliano ya mwaka wa 2018 na kusukuma Sudani Kusini karibu zaidi na ukingo wa vita.”

Matukio haya yanajumuisha “kiashiria muhimu cha uwezekano wa nchi kukabiliwa na ghasia,” inabainisha IGAD. “Ikiwa mivutano itaongezeka, hatari ya kuanza tena kwa uhasama ulioenea ni kubwa,” IGAD imeongeza, ikitoa wito wa kukomeshwa kwa uhasama. Sudani Kusini imeingia “katika hali ya kutisha ambayo inaweza kufuta miaka mingi ya maendeleo kuelekea amani,” Yasmin Sooka, mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu nchini humo, pia alibainisha siku ya Jumamosi.

Washington, kwa upande wake, iliamua kuwarejesha nyumbani wafanyakazi wake wasio wa muhimu kutoka nchini humo siku ya Jumapili kwa sababu “mgogoro wa kivita unaendelea.”

Hata hivyo, siku ya Jumatano, Wizara ya Mambo ya Nje ya Sudani Kusini ilisema katika taarifa yake kwamba hali imesalia “tulivu na salama” na kwamba nchi imesalia “wazi na salama,” haswa kwa “watalii.”

Uganda ilitangaza siku ya Jumanne kwamba imetuma vikosi maalum kuulinda mji mkuu Juba na kumuunga mkono Rais Kiir, hatua iliyokanushwa baadaye na Waziri wa Habari wa Sudani Kusini Michael Makuei Lueth.

Tangu kupata uhuru wake kutoka kwa Sudani mwaka 2011, nchi hiyo imekumbwa na ghasia ambazo zimeizuia kujikwamua kutoka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha umwagaji damu kati ya Rais Salva Kiir na Makamu wa Rais Riek Machar. Mzozo huu ulisababisha vifo vya karibu watu 400,000 na watu milioni nne kukimbia makazi kati ya mwaka 2013 na mwaka 2018, wakati mkataba wa amani ulipotiwa saini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *