
Mapigano makali yaliendelea siku ya Jumanne Machi 4 huko Nasir, mji mdogo kaskazini-mashariki mwa Sudan Kusini, kati ya jeshi la Sudani Kusini na vijana kutoka kundi lenye silaha la White Army, wanamgambo wa kijamii walio karibu na mpinzani Riek Machar. Lakini wakati kiongozi huyo anakanusha kuhusika na ghasia hizi, mkuu wa majeshi yake, Luteni Jenerali Gabriel Duop Lam, amekamatwa siku ya Jumanne katika makao makuu ya jeshi huko Juba.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Na mwanahabari wetu mjini Juba, Florence Miettaux
Kutumwa kwa vikosi vya usalama pia kuliripotiwa katika mitaa ya Juba na haswa karibu na makazi ya Makamu wa Rais Riek Machar.
Jeshi la Sudani Kusini halijatoa tamko lolote rasmi kuhusu matukio ya Nasir au kukamatwa kwa Gabriel Duop Lam. Akiwasiliana na RFI, Puok Both Baluang, msemaji wa Riek Machar, amethibitisha kukamatwa kwa mkuu wa jeshi la upinzani “kwa sababu zisizojulikana”.
Gabriel Duop Lam amekuwa nambari mbili katika jeshi la Sudan Kusini tangu mwaka 2022. Chini ya mipango ya usalama ya mkataba wa amani wa mwaka 2018, upinzani na serikali wameunda kamandi ya pamoja, kwa nia ya kuunda jeshi la umoja wa kitaifa.
Mapigano yanaweza kuharibu mpango wa amani
Kulingana na msemaji wa Riek Machar, Koang Gatkuoth na Wesley Welebe, majenerali wengine wawili wa upinzani, pia wako kizuizini. Pia amesema kuwa “idadi kubwa” ya vikosi vya usalama ilizingira makazi ya makamu wa kwanza wa rais wa Sudani Kusini Jumanne jioni na kutoa wito kwa wadhamini wa makubaliano ya amani kuingilia kati kutatua mgogoro huo.
Kulingana na mwanaharakati wa mashirika ya kiraia Ter Manyang Gatwech wa Kituo cha Utetezi wa Amani (CPA), Gabriel Duop Lam alikamatwa kwa sababu jeshi la Sudani Kusini linashutumu vikosi vya Riek Machar kuunga mkono kundi la wanamgambo la White Army huko Nasir. Edmund Yakani, kutoka shirika lisilo la kiserikali la CEPO, anaonya juu ya “kuongezeka kwa msuguano na mivutano kati ya pande zilizotia saini makubaliano ya amani.” Kulingana na Edmund Yakani, mapigano huko Upper Nile “yanahatarisha kuharibu mkataba wa amani.”