
El-Fasher, mji mkuu wa Darfur Kaskazini, ambao umezingirwa kwa karibu mwaka mmoja na RSF, ambao pia unakabiliwa na mapigano makali tangu jeshi la Sudan lilipoiteka tena Khartoum mwezi uliopita, unakabiliwa na hali mbaya ya kibinadamu.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Kwa vile serikali ya Sudani kwa mara ya kwanza imekiri kwa njia isiyo ya moja kwa moja kuwepo kwa njaa katika kambi ya wakimbizi ya Zamzam iliyo karibu, inatoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati ili kufungua njia salama za kupitsha misaada ya kibinadamu katika mji huo.
Baada ya kutwaa tena Khartoum, mji mkuu wa Sudani, mwishoni mwa mwezi Machi, jeshi la Sudani sasa linaangazia vita vya El-Fasher, mji mkuu katika jimbo la Kaskazini la Darfur. Wakati vikosi vya Jenerali Abdel Fattah Abdelrahman Burhan vinadai kuendelea kusonga mbele kwenye maeneo mbalimbali, vinabainisha kuwa hii ndiyo kesi hasa ndani na nje ya mji ambapo hali inasalia, kulingana na wao, “chini ya udhibiti.”
Siku ya Jumatatu, Aprili 7, ngome kadhaa za RSF zilizo karibu na El-Fasher zililengwa. Shambulio hilo lilisababisha vifo vingi: wanajeshi tisa waliuawa na magari matano kuharibiwa, ikiwa ni pamoja na msafara kutoka Nyala ambao pia ulilengwa na jeshi la anga la Sudani. Uvamizi huo unaripotiwa kusababisha vifo vya watu kadhaa, kwa mujibu wa taarifa ya jeshi, ambayo imesema walioweza kutoroka walikimbilia kusini, “na kuwaacha nyuma waliokufa na waliojeruhiwa.”
Katika kulipiza kisasi, RSF, kwa upande wao, ilishambulia kwa nguvu nyumba zilizoko magharibi mwa El-Facher na pia katika kambi ya watu waliohama makazi yao ya Abou Chouk. Kulingana na Mtandao wa Madaktari wa Sudan, shambulio hilo lilisababisha vifo vya takriban raia kumi, wakiwemo watoto wanne.
“Watu wanakabiliwa na hatari ya kufa polepole kutokana na kukosekana kwa aina yoyote ya misaada ya kibinadamu.”
Ni katika hali hiyo ambapo msemaji wa serikali ya Sudani ametoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati “kuokoa maisha ya wakazi wa El-Facher na miji jirani,” akisisitiza juu ya haja ya kuvunja kizuizi ambacho mji huo umekuwa chini ya karibu mwaka mmoja: “Ndege na magari lazima zifanye kazi chini ya maagizo ya Umoja wa Mataifa ili kuokoa maisha ya wakazi,” ameongeza. Katika hotuba yake, hatimaye ameutaka Umoja wa Mataifa kurekodi uhalifu wote uliofanywa na RSFhuko El-Fasher, ambapo hali ya kibinadamu inaendelea kuzorota.
Kulingana na Uratibu wa Kambi za Wakimbizi na Watu Waliohamishwa Sudan huko Darfur, hali ni “mbaya zaidi kuliko hapo awali” katika kambi tatu za watu waliokimbia makazi zinazozunguka mji mkuu wa Darfur Kaskazini: Zamzam, Abu Shuk na Assalam, ambapo shirka hilo lisilo la kiserikali limezindua wito wa dharura wa kusitishwa kwa mapigano siku ya Jumatatu kwa kuzingatia “hali ambayo haijawahi kutokea.” “Misaada haiwafikii tena waliokimbia makazi yao,” amesema msemaji wake, Adam Reggal, ambaye kulingana naye “maisha yamesimama kabisa. “Watu wanakabiliwa na hatari ya kufa polepole kutokana na kukosekana kwa aina yoyote ya misaada ya kibinadamu,” ameongeza.
Katika taarifa yake, Uratibu umeeleza kuwa katika kambi hizo tatu, masoko ni karibu tupu na kwamba wakazi wake wanakabiliwa na njaa, magonjwa na ukosefu wa maji ya kunywa huku wakiishi chini ya mabomu ya mara kwa mara. Ingawa wengi wangependa kukimbia kutokana na hali hii, wengi hawawezi kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa magari na mafuta, ingawa, kulingana na WHO, familia 530 zilifanikiwa kuondoka kwenye kambi ya Abu Chouk siku ya Jumatatu.
Mpango wa RSF kuwahamisha wakaazi wa El-Fasher?
Wakiwa tayari wamezingirwa na RSF, wakaazi wa El-Fasher, kwa upande wao, wanakabiliwa na shinikizo lingine, ambalo ni wapiganaji wa vikosi vya kijeshi vya Muungano wa Waanzilishi wa Sudan ulioundwa na familia ya Daglo na washirika wake mwezi Februari mwaka huu huko Nairobi. waasi hawa wanawahimiza kila mara kuondoka mjini: “Msiwe ngao ya binadamu ya jeshi, usalama wenu hauhakikishwi mjini,” tunaweza kusoma kwa mfano katika taarifa kwa vyombo vya habari inayosambazwa huko El-Fasher, ambayo lengo lake ni kuwasukuma watu kukimbia “ili kuhifadhi maisha yao.”
Kwa kujibu, gavana wa Darfur, Minni Minnawi, alishutumu kuwepo kwa mpango ulioandaliwa na RSF na wanamgambo wao kuwaondoa raia katika mji huo na katika kambi ya Zamzam. Kulingana na yeye, magari ya kukodi yangepatikana kwa watu wanaotaka kuondoka. Akitoa wito kwa wakazi wasikate tamaa, amesema kuwa ofa hii kwa hakika italenga kuwakamata wanaopenda na kupora mali zao kama inavyoonekana kwingineko nchini.