
Sudan imetangaza kusitisha uingizwaji wa bidhaa zote kutoka Kenya, baada ya nchi hiyo jirani mwezi Februari kutoa jukwaa kwa wanamgambo wa RSF, kuzindua mkataba wa uundwaji wa serikali mbadala ili kuongoza katika maeneo wanayodhibiti.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Hatua hiyo ilitangazwa siku ya Alhamisi na Waziri wa biashara wa Sudan Omar Ahmed Mohamed Ali, kwa mujibu wa Shirika la taifa la Habari, SUNA.
Waziri huyo amesema, kwa mujibu wa uamuzi wa kikao cha Baraza la Mawaziri, Sudan imeamua kusitisha uingizwaji wa bidhaa kutoka Kenya, kupitia mipaka ya ardhi na angani.
Uamuzi huu wa Sudan unakuja, baada ya kuishtumu Kenya kwa kuruhusu wanamgambo wa RSF ambao wamekuwa wakipambana na jeshi tangu Aprili mwaka 2023 kuendeleza shughuli zake jijini Nairobi.
Sudan inasema hatua hiyo itaendelea kwa muda usiojulikana na inalenga kulinda maslahi ya taifa na usalama wa taifa hilo lililo kwenye vita.
Majani ya chai, vyakula mbalimbali na dawa ni baadhi ya bidhaa ambavyo huingia nchini Sudan kutoka nchini Kenya.
Serikali ya Kenya ambayo imeendelea kusisitiza kuwa haina upande kwenye mzozo wa Sudan, haijazungumzia hatua hii.
Awali, Wizara ya Mambo ya nje ya Kenya, ilieleza kuwa, hatua ya Kenya kutoa jukwaa kwa RSF ni katika kuunga mkono juhudi za kusuluhisha mzozo unaoendelea kwa njia ya mazungumzo kama inavyoshinikizwa na Umoja wa Mataifa na Afrika.