
Serikali ya Sudan imesema siku ya Jumatatu itachukua “hatua za lazima” katika kukabiliana na kile ilichokiita usaidizi wa “kutowajibika na chuki” wa Kenya kwa ajili ya kuanzishwa kwa serikali pinzani na vikosi hasimu vya Rapid Support Forces (RSF) dhidi ya jeshi la kawaida.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Tangu mwezi Aprili 2023, mkuu wa jeshi Abdel Fattah Abdelrahman Burhan na kamanda wa RSF Mohamed Hamdan Daglo, ambao zamani walikuwa washirika, wamekuwa wakishiriki katika mapambano ya madaraka ambayo yameitumbukiza nchi hii katika vita vikali.
Siku ya Jumatatu wizara ya mambo ya nje ya Sudani ililaani vikali uidhinishaji wa viongozi wa Kenya wa hati ya kisiasa iliyotiwa saini mwishoni mwa juma mjini Nairobi na RSF na makundi washirika ya kisiasa na yenye silaha, ambayo walisema yanalenga kuanzisha “serikali ya amani na umoja” katika maeneo yanayodhibitiwa na waasi nchini Sudani.
Wizara hiyo ilishutumu “mfano hatari” katika “ukiukaji wa sheria ya kimataifa”, ambayo ni “tishio kubwa kwa usalama na amani ya kikanda”. Miongoni mwa makundi yaliyotia saini wa mkataba huo na RSF ni vuguvugu la Ukombozi wa Watu wa Sudan-Kaskazini la adui wao wa zamani, Abdelaziz al-Hilu, ambaye anadhibiti sehemu za kusini mwa nchi. Umoja wa Mataifa umeonya juu ya kuongezeka kwa “mgawanyiko” wa nchi.
Siku ya Jumapili jioni, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya, Musalia Mudavadi, alikaribisha kwenye mtandao wa kijamii wa X “kutiwa saini kwa makubaliano ya amani na kuundwa kwa serikali ya umoja” kati ya wadau nchini Sudani. Kwa kujibu, wizara ya Sudani kinyume chake inakosoa maendeleo ambayo “itapanua wigo wa vita na kurefusha muda wake”. Pia ilionya juu ya kudorora kwa uhusiano kati ya nchi hizo mbili na Kenya, haswa katika maswala ya kiuchumi.
Serikali ya Sudani tayari iliishambulia Kenya kwa kuandaa mpango huo, ikimrudisha nyumbani balozi wake Nairobi siku ya Alhamisi na kumshutumu Rais William Ruto kwa kutenda kulingana na “maslahi yake ya kibiashara na ya kibinafsi na wafadhili wa kikanda wa wanamgambo,” dokezo la wazi kwa Falme za Kiarabu?
Falme za Kiarabu zimekuwa zikishutumiwa mara kwa mara na Umoja wa Mataifa na Marekani kwa kusambaza silaha kwa FSR, jambo ambalo wanalikanusha. Mwezi uliopita, Kenya na Falme za Kiarabu zilitia saini makubaliano makubwa ya kiuchumi.
Jeshi la Sudani na washirika wake kwa sasa wanasonga mbele dhidi ya RSF katika mji mkuu Khartoum na katikati mwa nchi. Mzozo huo umesababisha vifo vya makumi ya maelfu, na kusababisha zaidi ya watu milioni 12 kuyahama makazi yao na kusababisha maafa ya kibinadamu. Wapiganaji kutoka kambi zote mbili wanatuhumiwa kwa uhalifu wa kivita, na FSR inashutumiwa rasmi kwa “mauaji ya kimbari” na Washington.