
Vikosi vya RSF nchini Sudan, vimesababisha unyanyasaji mkubwa wa kijinsia kwa wanawake na wasichana katika kipindi cha miaka miwili ya vita ya wenyewe kwa wenyewe, ili kudhalilisha, kudhibiti na kuhamisha jamii kote nchini.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 3
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa ripoti mpya ya shirika la kutetea haki za kibinadamu la Amnesty International, iliyotelewa Alhamisi, Aprili 10, 2025, ukatili wa RSF, ikiwa ni pamoja na ubakaji, ubakaji wa magenge na utumwa wa kingono, ni sawa na uhalifu wa kivita na uhalifu unaowezekana dhidi ya ubinadamu.
“Mashambulio ya RSF kwa wanawake na wasichana wa Sudan yanaudhi, yanapotosha na yanalenga kuleta udhalilishaji mkubwa. RSF imelenga raia, hasa wanawake na wasichana, kwa ukatili usiofikirika wakati wa vita hivi,” alisema Deprose Muchena, Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International wa Athari za Haki za Kibinadamu za Kikanda.
Ripoti hii kwa jina “Walitubaka sisi wote” imenakili wanajeshi wa RSF wakiwabaka wanawake na wasichana 36 na genge la vijana wenye umri wa miaka 15, pamoja na aina nyinginezo za ukatili wa kingono, katika majimbo manne ya Sudan kati ya Aprili 2023 na Oktoba 2024.
Ukiukaji huo ni pamoja na kumbaka mama huku akinyonyesha mtoto na utumwa wa kingono wa siku 30 wa mwanamke mmoja huko Khartoum, pamoja na kupigwa vikali, kuteswa hata kwa kukatwa na wembe wenye ncha kali, na mauaji.
Shirika la Amnesty International, linatoa wito kwa ulimwengu kuchukua hatua kukomesha ukatili wa RSF kwa kuzuia utiririshaji wa silaha nchini Sudan, kushinikiza uongozi kukomesha unyanyasaji wa kijinsia, na kuwawajibisha wahalifu wakiwemo makamanda wakuu, kama avyaoeleza hapa Naibu mkurugenzi wa shirika hilo katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, Flavia Mwangovya.
Flavia Mwangovya- Shirika la Amnesty International
Katika ripoti hii mpya, Amnesty iliwahoji watu 30, wengi wao wakiwa ni manusura na jamaa za walionusurika katika kambi za wakimbizi za Uganda, na wote walionusurika na mashahidi waliwatambua wapiganaji wa RSF kuwa wahalifu. Amnesty International inasema RSF haikujibu ombi lao la kutaka izungumzie madai haya.
Kila aliyenusurika katika unyanyasaji wa kijinsia ambaye alihojiwa na shirika hili alielezea jinsi shambulio hilo lilisababisha madhara makubwa ya kimwili au kiakili, na kuwa na athari mbaya kwa familia zao. Huko Nyala, Darfur Kusini, wanajeshi wa RSF walimfunga mwanamke kwenye mti kabla ya mmoja kumbaka huku wengine wakitazama.
“Ilikuwa siku ya kutisha zaidi maishani mwangu,” alisema. Huko Madani, Gezira, askari watatu wa RSF walimbaka mwanamke mbele ya bintiye mwenye umri wa miaka 12 na shemeji yake. Ilikuwa ya kufedhehesha sana,” mwanamke huyo alisema. Ninahisi kuvunjika.”
Madaktari wa kike walisema wanajeshi wa RSF waliwabaka ikiwa hawakuweza kuwaokoa wanajeshi waliojeruhiwa. Katika kisa kimoja kama hicho, muuguzi alisema askari 13 walimteka nyara huko Khartoum Kaskazini na kumlazimisha kuwatibu wanaume waliojeruhiwa vibaya kabla ya kumbaka na kundi la watu, na kumwacha akiwa amepoteza fahamu.
“Hofu ya unyanyasaji wa kingono wa RSF ni mkubwa, lakini kesi zilizonakiliwa kati ya wakimbizi zinawakilisha sehemu ndogo ya ukiukaji ambao RSF imeweza kufanya, mwitikio wa kimataifa kwa mateso ya wanawake na wasichana wa Sudan umekuwa wa kulaumiwa” alisema Deprose Muchena, Mkurugenzi Mkuu wa Amnesty International wa Athari za Haki za Kibinadamu za Kikanda
Kama wakimbizi, wote walionusurika walisema kipaumbele chao kilikuwa kupata matibabu kwa majeraha na magonjwa yanayoletwa na RSF au kwa hali ya kiafya iliyokuzwa wakiwa utumwani. Hata hivyo, kupunguzwa kwa programu muhimu zinazofadhiliwa na USAID kumepunguza matarajio ya kupata huduma kamili ya afya.
Vita nchini sudan vilizuka Aprili 2023, kati ya Jenerali Abdel Fattah al Burhan na Hamdan Dagalo huku makumi ya maelfu wakiuawa na mamilioni wakihamishwa makwao, wakati huu pande zote mbili zikilaumiwa kutekeleza vitendo vya uhalifu.