
Juba. Vikosi vya Sudan Kusini vimemkamata Waziri wa Mafuta na maofisa waandamizi wa jeshi wanaoshirikiana na Makamu wa Kwanza wa Rais, Riek Machar huku wanajeshi wakiizingira nyumba yake katika mji mkuu, Juba.
Naibu Mkuu wa Jeshi, Jenerali Gabriel Duop Lam, mshirika wa Machar, alizuiwa Jumanne iliyopita, huku Waziri wa Petroli, Puot Kang Chol akikamatwa Jumatano pamoja na walinzi wake na familia yake.
Machar, ambaye ushindani wake wa kisiasa na Rais Salva Kiir katika siku za nyuma ulilipuka na kusababisha vita vya wenyewe kwa wenyewe, mwezi uliopita alisema kutimuliwa kwa washirika wake kadhaa kutoka kwenye nyadhifa serikalini kulitishia makubaliano ya amani ya mwaka 2018 kati yake na Kiir.
Mpango huo ulikuwa umemaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano na zaidi ya watu 400,000 waliuawa. Waziri wa Maji, Pal Mai Deng, msemaji wa Chama cha Machar cha SPLM-IO, alisema kukamatwa kwa Lam, “kunaweka makubaliano yote ya amani hatarini.”
“Hatua hii inakiuka Mkataba Uliohuishwa wa Utatuzi wa Mzozo Sudan Kusini na kuidumaza Bodi ya Ulinzi ya Pamoja, taasisi muhimu ya mkataba inayowajibika kwa amri na udhibiti wa vikosi vyote. Kitendo hiki kinaweka makubaliano yote hatarini,” taarifa ya Deng ilisema.
“Pia, tuna wasiwasi mkubwa kuhusu kuwekwa kwa nguvu kwa SSPDF [wanajeshi wa Jeshi la Sudan Kusini] karibu na makazi ya… Machar,” aliandika. “Vitendo hivi vinaondoa imani na uaminifu miongoni mwa vyama.”
Msemaji mwingine wa Machar, Puok Both Baluang, alisema maofisa wengine wakuu wa kijeshi wanaoshirikiana na Machar wamewekwa katika kizuizi cha nyumbani.
“Hadi sasa, hakuna sababu yoyote iliyotolewa kwetu iliyosababisha kukamatwa au kuzuiliwa kwa maofisa (hawa),” Baluang aliliambia Shirika la Habari la Reuters.
Meja Jenerali Lul Ruai Koang, msemaji wa Jeshi la Sudan Kusini, alisema katika taarifa mwishoni mwa Jumanne kwamba hatatoa maoni yoyote kuhusu kukamatwa au wanajeshi wanaozunguka makazi ya Machar.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyozuka Desemba 2013 baada ya Kiir kumfukuza Machar pia viliwafukuza watu milioni 2.5 kutoka makwao na kuacha karibu nusu ya Taifa hilo lenye watu milioni 11 wakihangaika kutafuta chakula cha kutosha.
Mvutano huo unaonekana kuchochewa na kuongezeka kwa wasiwasi juu ya machafuko huko Upper Nile.
Jeshi la SSPDF limemshutumu Lam na wanajeshi wake kwa kufanya kazi na wale wanaojiita waasi wa White Army katika eneo hilo, ambao wengi wao wanatoka katika jamii moja ya kabila la Nuer.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilianza miaka miwili baada ya Sudan Kusini kuwa huru kutoka kwa Sudan.
Ter Manyang Gatwich, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Amani na Utetezi, alitoa wito wa kuachiliwa mara moja kwa wale waliokamatwa ili kuepusha kuongezeka zaidi kwa ghasia na umwagaji wa damu kutokana na kuzorota na kuwa kile alichokiita vita kamili.