Makamu wa kwanza wa rais wa Sudan Kusini, Riek Machar, ambaye ni hasimu wa muda mrefu wa rais Salva Kiir, ameripotiwa kukamatwa hapo jana na idara za usalama, hatua ambayo umoja wa Mataifa unasema uneiweka nchi hiyo katika njia ya kurejea kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Taarifa zinasema msafara wa magari zaidi ya 20 ya vikosi vya usalama vya Serikali, vilizingira na kuingia kwa nguvu katika makazi ya Machar mjini Juba, ambapo walimpa hati ya kukamatwa kwake kabla ya kuondoka nae, vyanzo vya karibu vimethibitisha.
Msemaji wa chama cha Machar anayehusika na uhusiano wa kimataifa wa chama hicho, Reath Muoch, kupitia ukurasa Wake wa Facebook, amelaani kile alichosema ukiukwaji wa wazi wa katiba ya nchi na mkataba wa amani wa mwaka 2018 uliofanywa na waziri wa ulinzi pamoja na mkuu wa idara ya usalama wa taiaf.
Muoch, amesema walinzi wa Machar walinyang’anywa silaha na kisha kukabidhi hati ya kukamatwa kwa Machar, bila hata hivyo serikali kueleza kiongozi huyo amekamatwa kwa tuhuma gani, ingawa anahusishwa na kundi la wapiganaji wa White Army ambao hivi karibuni walishambulia kambi za jeshi la serikali huko Nasir.

Tume ya umoja wa Mataifa nchini humo, imeonya kuhusu hatua hii ya Serikali ambapo imezitaka pande hasimu kujiepusha na vitendo vyovyote ambavyo vinaweza kuitumbukiza nchi hiyo katika vita nyingine ya wenyewe kwa wenyewe.
Mapigano ya mwaka 2013 kati ya vikosi vya Machar na rais Kiir, yalisababisha vifo vya zaidi ya watu laki 4 kabla yam waka 2018 kutiliana saini mkataba wa amani uliopelekea kuundwa kwa Serikali ya umoja wa Kitaifa, serikali ambayo hata hivyo tangu wakati huo imeshindwa kutekeleza vipengele muhimu vya mkataba huo.